Maajabu maisha ya Uwanja wa Fisi

10Dec 2018
Sabato Kasika
DAR ES SALAAM
Nipashe
Maajabu maisha ya Uwanja wa Fisi

KAMA ilivyo kwenye majiji mengine duniani, Jiji la Dar es Salaam limegawanyika katika maeneo ya makundi tofauti ya watu wenye uwezo mkubwa kiuchumi, wa kati na walalahoi ambao vitongoji vyao hujulikana kama `maeneo ya uswazi’.

eneo la uwanja wa fisi.

Uwanja wa Fisi ni eneo maarufu lililopo Manzese, linalosifika kwa wakazi wake wengi kuishi maisha ya hali ya chini ya kutegemea vyakula vinavyouzwa kwa bei rahisi na wakati mwingine kuuziwa bidhaa zilizopita muda wa matumizi.

Wafanyabiashara na wakazi wa eneo hilo wanatumia akili kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa na watu wanaishi sawa na watu wengine wenye vipato vizuri vinavyowawezesha kula kuku, nyama, wali, mkate uliopakwa siagi na vingine vingi.

Asilimia kubwa ya wakazi wa eneo hilo ni watu wenye vipato vya chini na wanaoishi katika lindi la umaskini. Kutokana na hali hiyo wanajikuta wakishindwa kumudu gharama za maisha kama chakula, mavazi na nyumba za kuishi, lakini maisha yanaendelea kwa mtindo huo waliouzoea.

Mazingira hayo yanawafanya kutumia akili na kupata mahitaji yao kulingana na uwezo wao kifedha.

Mahitaji ya kila siku

Uchunguzi uliofanywa na Nipashe katika eneo hilo na maduka yanayouza bidhaa mbalimbali vikiwamo vyakula, umebaini kuwa vitu vinavyouzwa huendana na uwezo wa kifedha wa wakazi wenyewe ili kuhakikisha kila mmoja anapata anachohitaji.

Bidhaa kama chumvi, sukari, majani ya chai, mafuta ya kula, mafuta ya taa na vitu vingine vinafungwa kwenye vifuko vidogo kwa ujazo unaolingana na vile vya karanga, huku kila kimoja kikiwa na bei yake.

Kifuko cha sukari chenye ujazo huo kinauzwa Sh. 150, huku majani ya chai na chumvi vikiuzwa kwa Sh. 50, kiwango ambacho kinaelezwa kuwa wakazi wengi wa eneo hilo wanaweza kukimudu.

Mmoja wa wafanyabiashara wa duka la vyakula katika eneo hilo, Shaban Bata, alieleza kuwa analazimika kufunga bidhaa hizo katika ujazo huo kwa kuwa wateja wake wengi hawana uwezo wa kununua katika kiwango cha robo kilo, nusu au kilo moja na kuendelea.

"Nina uzoefu na maisha ya huku ndio maana ninafanya hivyo, kwa kuwa unaweza kukuta kwa siku unapata wateja wawili wenye uwezo wa kununua nusu kilo, kwanini nisiuze kulingana na uwezo wao?” Bata alieleza.

Alisema hata unga wa mahindi, ngano, mchele na maharage, wengi wao hununua katika kipimo cha robo kilo na nusu kilo, huku mafuta ya kula na ya taa akiuza kwenye vipimo vidogo vya Sh. 100 hadi 200, ambavyo anaamini wanaweza kuvimudu.

"Ukiuza vipimo vya kuanzia kilo moja na kuendelea huwezi kupata wateja, huku wamezoea kununua kwa bei ya chini," alisema.

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Hassan Juma, alisema pamoja na umaskini, bei hizo anaweza kuzimudu mradi maisha yaende kwa vile vitu vinauzwa kulingana na uwezo wa mteja.

Revina Mwinjuma, mkazi mwingine wa eneo hilo, alisema ni vigumu mtu mwenye hali ya chini kuhama eneo hilo kwenda kuishi sehemu nyingine kwa kuwa atashindwa kumudu maisha kama ilivyo katika eneo hilo.

"Huku kwetu mtu anaweza kwenda sokoni na kuokota mchele, mahindi, maharage ambavyo humwagika wakati magari yakishusha mzigo na kuja kupepeta nyumbani na kupata chakula kwa ajili ya familia. Maisha kama haya utayapata wapi zaidi ya huku?” Mwinjuma alihoji.

Alisema hata mboga zinauzwa kwa bei nafuu kuanzia vichwa vya kuku, miguu, shingo, utumbo na vichwa vya dagaa ambavyo baadhi ya familia zimekuwa vikichukua na kwenda kuvipika.

"Hivyo vyote vinauzwa kwa bei nafuu kuanzia Sh. 100 hadi 150 kwa kichwa cha kuku, mguu na fungu la utumbo, lakini vichwa vya dagaa mtu anaweza kupata bure kutoka kwa mamalishe," alisema.

Mariam Salum, mmiliki wa nyumba ya vyumba vinne katika eneo hilo, alisema kodi za vyumba zina unafuu katika eneo hilo na wapangaji wanalipa kila mwezi badala ya mwaka kama ilivyozoeleka kwenye maeneo mengine.

"Nyumbani kwangu ninapangisha chumba Sh. 30,000 kila mwezi, nikichukua kwa mwaka ninaweza kujikuta sina kitu, hivyo ni bora nilipwe kwa mwezi, nikikusanya kwa wote ninaweza kufanya jambo la maana," alisema.

Kwa eneo hilo chumba cha Sh. 30,000 ni chenye umeme, lakini chumba ambacho hakina umeme kinaanzia Sh. 10,000 hadi 15,000 kwa mwezi.

Ulevi na usalama

Katika eneo hilo, unywaji wa pombe ni jambo la kawaida. Baadhi ya wakazi wa Uwanja wa Fisi wakati wote wanakuwa wamelewa, kuanzia asubuhi hadi usiku pombe za kila aina zinanyweka.

Wakati wote katika eneo hilo unauziwa pombe ya kienyeji na viwandani, tena kwa bei chee.

Chupa moja ya bia huuzwa kati ya Sh. 1,000 hadi 1,500, tofauti na maeneo mengine ambayo vinywaji hivyo vimekuwa vikiuzwa kwa bei ya juu kati ya Sh. 2,000 hadi 2,500.

Sababu ya kuuzwa kwa bei hiyo inaelezwa kuwa ni kutokana na bia hizo kuisha muda wa matumizi, lakini zinachangamkiwa na walevi wa eneo hilo bila kujali hatari wanayoweza kuipata kiafya.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Muungano ambao Uwanja wa Fisi uko ndani ya himaya yake, John Mkude, alisema amejitahidi kwa kiasi kubwa kuhakikisha wakazi wake hawanyweshi vitu vilivyopitwa na wakati.

"Kwa kiasi fulani bia zilizopitwa na wakati zimeanza kupungua kwa kuwa tumekuwa tukifuatilia kwa karibu ingawa ninasikia bado wapo wanaoendelea kuziuza kwa kificho," alisema Mkude.

Alieleza kuwa baada ya kuwabana wauzaji wa pombe hizo, sasa wameibuka na mtindo wa kuuza konyaji katika vipimo vidogo ili kuhakikisha kila mteja anamudu bei hiyo.

"Unakuta mtu ananunua chupa kubwa ya konyagi kwa Sh. 9,000 kisha anauza katika vipimo vidogo vya Sh. 300 hadi 500, akimaliza chupa nzima anakuwa amepata faida kubwa," alisema.

Mkude aliongeza kuwa aina hiyo ya ulevi imeshika kasi baada ya serikali kupiga marufuku ufungaji wa pombe katika viroba ambao miaka ya nyuma ulikuwa umeshamiri na kusababisha pombe kuuzwa kiholela.

"Ninatamani siku moja eneo hili libadilishwe ili tuondokane na vitendo vya ovyo ambavyo vimekuwa vikitendeka huku," alisema.

Alibainisha kuwa biashara ya ukahaba imeshamiri eneo hilo na vitendo hivyo vinafanyika vichochoroni na wakati mwingine vinafanywa mchana.

Alisema kuna watoto wa kike wenye umri wa kuanzia miaka 15 na wanawake watu wazima wamekuwa wakijihusisha na biashara hiyo na baadhi yao wamepanga vyumba maalum kwa ajili ya biashara hiyo.

"Watu wanaishi kwa kutegemea miili yao na bei zao ni nafuu kabisa kuanzia Sh. 500 hadi 5,000 inategemea na mtu mwenyewe anayejiuza," alisema mmoja wa wakazi wa Uwanja wa Fisi ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.

Alisema wa bei ya chini wengi wao ni wavuta bangi na ndio ambao wamekuwa wakifanyia biashara hiyo uchochoroni au kwenye 'gheto', huku wakishuhudiwa na wenzao.

"Wapo wale ambao wana vyumba vyao, mteja anaingia anamaliza haja yake kulingana na jinsi walivyokubaliana kisha anaondoka zake, lakini hao wasichana wanaovuta bangi na wavulana wao humalizana sehemu yoyote na muda wowote, hasa vichochoroni," alisema.

Kauli ya Makonda

Mkuu Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, aliwahi kutembelea eneo hilo na kuahidi kutafuta wafadhili watakaonunua nyumba za eneo la Uwanja wa Fisi ili kufuta biashara ya ngono katika eneo hilo.

"Hatuwezi kuacha kuona vijana wetu wakipotea na kupotoka kimaadili kwa watu kujenga majengo na madanguro, ambayo yanahamasisha biashara ya ngono katikati ya makazi, hivyo nitatafuta wawekezaji wa kununua eneo hili, ili kuondoa biashara hiyo,” alisema Makonda katika ziara yake hiyo.

Habari Kubwa