Maajabu mawili ya namba tisa matokeo Kidato II

16Jan 2017
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Maajabu mawili ya namba tisa matokeo Kidato II

MKOA wa Mtwara umeboronga katika matokeo ya mtihani wa taifa wa upimaji wa kidato cha pili baada ya shule zake tisa kuwa miongoni mwa 10 zilizoshika mkia kwenye mtihani huo.

Aidha, katika mtihani huo uliofanyika kuanzia Novemba 14 hadi 25, mwaka jana, kuna wasichana tisa katika orodha ya wanafunzi 10 kwa ufaulu.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Dk. Charles Msonde, akitangaza matokeo ya mtihani jijini Dar es Salaam jana, alizitaja shule za mkoa huo zilizofanya vibaya na idadi ya watahiniwa kwenye mabano kuwa ni:

Chingungwe (45), Malocho (60), Naputa (110), Chanikanguo (62) na Mtiniko (150).

Nyingine ni Michiga (73), Msimbati (56), Salama (57) na Lukokoda (44).

Shule inayokamilisha '10 Bora' ya zilizofanya vibaya zaidi katika mtihani wa taifa wa kidato cha pili mwaka jana ni Nywelo ya mkoani Tanga.

SHULE 10 BORA
Dk. Msonde alizitaja shule 10 zilizofanya vizuri katika matokeo hayo kuwa ni St. Francis Girls (Mbeya), Kilimanjaro Islamic (Kilimanjaro), Kaizirege Jonior (Kagera), Canossa (Dar es Salaam), Twibhoki (Mara), Tengeru Boys (Arusha), Marian Boys (Pwani), Precious Blood (Arusha), Thomas More Machrina (Dar es Salaam) na Shamsiye (Dar es Salaam).

Aliwataja watahiniwa 10 bora kitaifa na shule zao kwenye mabano kuwa ni Teckla Haule (Canossa), Joseph Kalabwe (Kwema Modern), Mirabel Matowo(Canossa), Hamida Kihiyo (St. Aloysius Girls), Rachel Sogoja (Heritage), Clare Hamissi, Roselyn Kissaka, Joy Kimambo, Venastra Mringo na Babymaisara Kimazi wote wa Feza Girls.

Katibu Mkuu huyo aliwataja wasichana 10 bora kitaifa na shule wanazotoka kwenye mabano kuwa ni Haule na Matowo (Canossa), Kihiyo (St. Aloysius Girls), Sogoja (Heritage), Hamissi, Kassaka, Kimambo, Mringo, Kimazi wote wa Feza Girls na Janeth Nandi wa Marian Girls.

Wavulana 10 bora kitaifa na shule zao kwenye mabano kwa mujibu wa Dk. Msonde ni Joseph Kalabwe (Kwema Modern), John Bugeraha, Evance Minishi, Isack Julius, Avith Kibani, Emmanuel Dismas, Harry Mshana, Salim Mchomvu wote wa Marian Boys, Lorian Njian wa Kaizirege Junior na Omega Logata wa Marian Boys.

Dk. Msonde alisema mtihani huo ulilenga kutoa tathmini endelevu ya wanafunzi inayolenga kubainia maarifa, ujuzi na mwelekeo waliopata wanafunzi baada ya kipindi cha miaka miwili ya elimu ya sekondari.

“Upimaji huu huchangia asilimia 10 ya alama endelevu ya mwanafunzi kwa kila somo kwenye mtihani wa kidato cha nne,” alifafanua.

Alisema tathmini hiyo inawasaidia wanafunzi kuongeza bidii katika ujifunzaji wa maendeleo ambayo yameonyesha kuwapa shida watakapokuwa wakiendelea na masomo yao ya kidato cha tatu.

Aliongeza kuwa mtihani huo pia huwasaidia walimu kuboresha mbinu za ufundishaji wa mada mbalimbali ambazo wanafunzi hawakufanya vizuri.

MKUU WA MKOA ANENA
Akizungumzia kuingiza shule tisa katika orodha ya 10 zilizoshika mkia, Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendegu, amefichua kilichosababisha kuboronga kwenye mtihani wa upimaji kitaifa kwa kidato cha pili.

Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana, Halima alibainisha sababu kubwa ni walimu kushidwa kutimiza wajibu wao, kufanya kazi kwa mazoea na utoro kwa ajili ya shughuli za kilimo, kuchezwa na kuolewa kwa wanafunzi.

“Sababu kubwa ya mkoa wetu kuboronga ni waliopewa jukumu la kufundisha watoto wetu kutokutekeleza wajibu wao, na badala yake kufanya alimradi siku ziende,” alifafanua.

Alisema mkoa ulifanya ufuatiliaji wa ndani na kubaini matatizo ya elimu na kuitisha kikao cha wadau wa elimu kuona namna ya kuokoa jahazi.

“Katika kikao cha wadau tuliangalia tuna tatizo kubwa la utoro, miundombinu na tukaangalia mtawanyiko wa walimu, uwezo wao na utendajikazi kwa maana ya uwajibika na wanaohusika moja kwa moja kwenye usimamizi wa elimu katika ukaguzi na ufuatiliaji,” alibainisha.

Mkuu huyo wa mkoa alisema utoro wa wanafunzi unasababishwa na wazazi kuwachukua watoto wao kwenda nao shambani maeneo ya mbali kama Lindi kwa ajili ya kilimo cha ufuta.

“Jingine ni tamaduni ambazo wameishi nazo kwa muda mrefu, hawaoni umuhimu wa mtoto kwenda shule, hakuna msisitizo shule inaonekana kama burudani na siyo lazima kama maeneo mengine. Pia Mimba za utotoni ni tatizo kubwa, lakini tunapambana navyo.”

Dendegu alisema kuwa matokeo hayo yalitarajiwa baada ya kufanya tathimini ya ndani, na kuchukua hatua za kinidhamu kwa ambao wameshindwa kutimiza wajibu wao.

Mkuu huyo wa mkoa alisema aliagiza kuvuliwa madaraka kwa walimu wakuu 63 kutokana na udanganyifu, baada ya kubaini kuwa wanafunzi waliofaulu darasa la saba wanapoendelea kidato cha kwanza wanashindwa kufanya vizuri kwenye masomo yao.

Alisema walimu hao walivuliwa madaraka na viongozi husika walipaswa kufuata hatua za kisheria na ikifika Januari 30, mwaka huu, atafuatilia utekelezaji wake.

“Tulibaini wanashiriki kudanganya, mwanafunzi anaonekana amefanya vizuri amepata ufaulu wa juu kumbe amefanyiwa mitihani,” alifafanua.

Dendegu alisema wameanza na shule za msingi kwa kuwa mwanafunzi akishindwa kufanya vizuri msingi hata sekondari hataweza kufaulu.

Kuhusu shule za sekondari zilizofanya vibaya, alisema watafuatilia kwa kina sababu zilizosababisha hayo na kuchukua hatua kwa walioshindwa kutimiza wajibu wao.

Aidha, alisema watafuatilia changamoto zilizopo katika mkoa huo, na kwamba uwepo wake siyo sababu ya wanafunzi kwa kuwa wapo wanaosoma chini ya mti na kufaulu huku akijitolea mfano wa jinsi alivyofaulu alivyosoma shule ya kawaida.

UFAULU WAONGEZEKA
Katibu Mkuu huyo alisema jumla ya wanafunzi 435,075 waliaondikishwa kufanya mtihani huo mwaka jana, asilimia 50.82 wakiwa ni wasichana, 410,519 sawa na asilimia 94.36 walifanya mtihani huo wakati wanafunzi 24,556 sawa na asilimia 5.64 hawakufanya kwa sababu za utoro na ugonjwa.

Kwa mujibu wa Dk. Msonde wanafunzi 372,223 sawa na asilimia 91.0 wamepata ujuzi na maarifa ya kuwawezesha kuendelea na kidato cha tatu. Kati yao, 189,161 ni wasichana sawa na asilimia 90.27 na wavulana 183,067 sawa na asilimia 91.80.

Mwaka 2015 wanafunzi 324,068 sawa na asilimia 89.12 walipata alama za kuwawezesha kuendelea na masomo ya kidato cha tatu.

Aidha, Dk. Msonde alisema wanafunzi 36,737 sawa na asilimia 8.98 wameshindwa kupata alama za kuwawezesha kuendelea na kidato cha tatu.

Alisema watahiniwa 178,115 sawa na asilimia 43.55 wamepata daraja la kwanza hadi la tatu. Kati yao, 78,466 ni wasichana sawa na asilimia 37.45 na wavulana ni 99,649 sawa na asilimia 49.97.

SAYANSI BADO MAUMIVU
Katika matokeo hayo, wanafunzi wamefanya vibaya katika masomo ya sayansi huku Hisabati likiwa na ufahulu wa asilimia 21.55 ambao wa chini zaidi kulinganishwa na masomo mengine.

Masomo mengine na kiwango cha ufahulu kwenye mabano ni Fizikia (28.13%), Kemia (45.76%), Jiografia (53.87%), Baiolojia 63.09%), Historia (73.56%), Kiingereza (77.21), Uraia (83.87%), huku somo la Kiswahili likiongoza kwa kuwa na ufaulu wa asilimia 90.06.

Hata hivyo, Dk. Msonde alibainisha kuwa ufaulu wa masomo ya Uraia, Historia, Jiografia, Kiswahili, Fizikia, Kemia na Baiolojia umepanda huku somo la Kiingereza likiendelea kushuka.

“Tathmini ya awali ya matokoo ya upimaji kitaifa imebaini masomo ya Hisabati, Fizikia na Kemia ufahulu uko chini ya wastani, hivyo jitihada za makusudi zinahitajika kuendelea kufanyika ili kuinua kiwango cha ufaulu wa masomo haya,” alisisitiza.

Aliongeza kuwa Necta itafanya uchambuzi wa kina wa matokeo kwa kila somo na kutoa machapisho ya uchambuzi yatakayowasilishwa kwa wadau wa elimu, zikiwamo shule za sekondari kwa lengo la kuwawezesha walimu kutumia taarifa za uchambuzi katika kuboresha ufundishaji na ujifunzaji shuleni.

Aliwataka walimu na wanafunzi kuendeleza juhudi katika ufundishaji na ujifunzaji katika masomo waliyofanya vizuri ili waendelee kuimarika zaidi katika masomo hayo wanapokuwa kidato cha tatu.

“Kwa masomo ambayo hayakufanyika vizuri, walimu wafanye juhudi za makusudi kuhakikisha ufundishaji na ujifunzaji wa masomo hayo unaimarishwa katika kidato cha tatu ili kuinua ufaulu wa wanafunzi katika masomo hayo kabla ya kuingia kidato cha nne,” alisema.

Dk. Msonde pia aliwataka wamiliki wa shule, walimu wakuu na walimu wahakikishe ufundishaji na ujifunzaji unaimarika katika masomo yote shuleni ili kuwawezesha wanafunzi kuwa mahiri katika masomo yote na kuinua ufaulu wao.

MDAU ANENA
Mdau wa elimu, Benjamini Mkonya, alisema mkoa wa Mtwara umefanya vibaya kwa kuwa unapokea walimu waliopewa adhabu ya uhamisho kwa sababu ya makosa kama ulevi, kuwapa mimba wanafunzi.

Kwa mujibu wa Mkonya walimu wengi wa mkoa huo na Simiyu au Katavi ni wale ambao walikuwa na vyeti feki katika operesheni ya kuondoa wenye vyeti feki.

“Serikali inapaswa kufanya uwekezaji mkubwa katika mikoa ya pembezoni," alisema Mkonya.

"Tunashukuru Rais (John Magufuli) alipeleka barabara ya lami, aliyepita naye alipeleka viwanda kama Dangote, kukiwa na mchanganyiko wa watu watahamasika kusoma na kuthamini elimu,” alifafanua.

Kuhusu kuporomoka kwa masomo ya sayansi, alisema tatizo lipo kwenye kutukuza siasa na kwamba elimu haiendi kwa vipaumbele vya taifa kama viwanda ambavyo vinafanya nchi inajulikana kimataifa na ambavyo vinaletwa na sayansi.

“Unakuta mwalimu wa sayansi anavyolipwa ni mshahara wa kukatisha tamaa, wanasoma Tanzania lakini wanaenda kufanyakazi mahali wanaheshimiwa kama Botswana, Malawi, Namibia na Afrika Kusini. Tanzania haina walimu wa sayansi,” alibainisha.

Mkonya alisema tatizo jingine ni ukosefu wa maabara na zilizopo ni asilimia 20 ikiwa na maana kuwa katika kila shule 100 zenye maabara ni 20.

“Masomo ya sayansi na hesabu hayafundishwi kikamilifu kwa sababu za uwekezaji na rasilimali watu."

Habari Kubwa