Maalim Seif amtaka Membe kutowachanganya wanachama

21Oct 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Maalim Seif amtaka Membe kutowachanganya wanachama

MWENYEKITI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, amemtaka mgombea urais wa chama hicho, Bernard Membe, kutowachanganya wanachama wao kuhusu watakayempigia kura kwa nafasi ya urais.

MWENYEKITI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad

Na Frank Maxmillian, TUDArco

Amesema viongozi wa chama hicho katika moja ya vikao vyao, walikubaliana wanachama wampigie kura mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, na kwa Zanzibar wanachama wa CHADEMA wampigie mgombea urais wa ACT-Wazalendo, Maalim Seif.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, kiongozi huyo alidai kusikitishwa na alichozungumza Membe juzi na kwamba kupitia mkutano mkuu wa taifa waliamua kushirikiana na Membe alipokuja katika chama aliambiwa na akakubali kushirikiana katika kampeni.

Juzi, Membe alizungumza na waandishi wa habari na kusema ataendelea na kampeni zake katika ngwe ya mwisho huku akiwakata wapigakura kumchagua wanayeona anafaa.

Maalim Seif alisema baada ya kuona kampeni zinasuasua, walikutana na kushauriana na Membe ambaye aliomba muda wa kutafakari na baadaye walikubaliana kushirikiana na Lissu, lakini ushirikiano wake (Membe) haukuwa mkubwa.

“Nasikitika sana leo (jana) mjumbe (Membe) wa kamati hiyo hiyo anakuja kukana makubaliano yetu,” alisema.

“Alilosema Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, si lake na mimi (Maalim Seif) nililosema si langu bali ni uamuzi rasmi wa chama. Mimi ni Mwenyekiti wa Chama, Kamati Kuu na Halmashauri ya Uongozi na moja kati ya majukumu yangu ni kusimamia uamuzi wa chama, ulifanywa tokea kikao cha kwanza kabisa,” alifafanua.

ABAINISHA KASORO

Aidha, alisema kwa upande wa Zanzibar kuna njama za wazi zilizobainishwa mapema juu ya kuleta kasoro kwenye uchaguzi na yasiposhughulikiwa mapema haitaridhia.

Alisema wananchi wengi watakosa haki yao ya kikatiba ya kupiga kura kutokana na wengi kutoandikishwa na kwamba haki ya kikatiba imeporwa kwa zaidi ya wananchi 1,000.

Aliongeza kuwa wakati wa uteuzi wa wagombea kupitia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) wanachama wa ACT-Wazalendo wanane na 12 wawakilishi walienguliwa.

“Tunavyoambiwa lengo kura ya mapema ni kuwawezesha watu wenye majukumu ya usalama pamoja na ulinzi na usimamizi wa uchaguzi kupata muda wa kusimamia ulinzi na usalama siku ya uchaguzi mkuu, sasa hawa wanaopiga kabla Oktoba 27 hawataruhusiwa kuwapigia Serikali ya Muungano,” alisema Mwenyekiti Seif.

Vile vile, alisema katika uchaguzi kumekuwa na vitendo vya kuvunjwa kwa haki za kibinadamu vinavyofanywa na baadhi ya watu kutokana na kukithiri kwa vitisho kiasi cha baadhi ya watu kukimbilia porini.

Kwa mujibu wa Maalim Seif, kuna njama za kumdhibiti baada ya kupiga kura yake ikiwamo kukosa mawasiliano ya simu na viongozi wenzake.

Habari Kubwa