Maalim Seif atema nyongo

20Mar 2019
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Maalim Seif atema nyongo

ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amepokewa rasmi ACT-Wazalendo na kueleza mambo mbalimbali yakiwamo yanayomhusu Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba.

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, akionyesha kadi namba moja ya Chama cha ACT Wazalendo, baada ya kukabidhiwa rasmi na Kiongozi wa ACT, Zitto Kabwe (wa pili kushoto), jijini Dar es Salaam jana. PICHA: HALIMA KAMBI


Maalim Seif (75), juzi alitangaza kujivua uanachama wa CUF na kujiunga na Chama cha ACT-Wazalendo muda mfupi baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, kubariki uamuzi wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa wa kumtambua Prof. Lipumba kuwa Mwenyekiti wa CUF.


Mapokezi rasmi ya Maalim Seif yalifanyika jana kwenye ofisi za ACT-Wazalendo jijini Dar es Salaam yakishuhudiwa na mamia ya wafuasi wa Maalim Seif waliotangaza kujiengua CUF.


Katika mapokezi hayo, kulikuwa na burudani za ngoma huku bendera za ACT-Wazalendo zikipepea katika mtaa mzima maeneo ya Kijitonyama, ziliko ofisi za chama hicho kinachoongozwa na Zitto Kabwe.


Akizungumza baada ya Zitto kumkabidhi kadi namba moja iliyolipwa ada ya miaka 10, Maalim Seif alisema sasa ni mwanachama rasmi wa ACT-Wazalendo, akiahidi kukisaidia chama hicho kichanga kujijenga.


“Tena mmesema nichukue kadi namba moja, mama yangu weeeee," Maalim Seif alisema baada ya kupewa nafasi ya kuzungumza.


Kadi aliyopewa mwanasiasa huyo mzoefu, awali ilichukuliwa na aliyekuwa Mshauri wa ACT-Wazalendo, Albert Msando. Wakili huyo alijiuzulu uanachama wa chama hicho mwaka 2017.


Katika mkutano huo wa kumkaribisha rasmi ACT-Wazalendo, ambao wanachama wengine 21 wa CUF walichukua kadi za chama hicho kipya, Maalim Seif alisema kuanzia sasa hataki malumbano na hata kulisikia tena jina la Prof. Lipumba.


“Mambo ya Lipumba msinitajie kabisa. Sitaki kulumbana na Lipumba, Lipumba kwangu mimi mwisho," Maalim Seif alisema na kushangiliwa na wanachama wa ACT-Wazalendo waliohudhuria mkutano huo.

Alisema walipokuwa CUF, walijitahidi kujenga taasisi ndiyo maana wakati mwingine alikuwa akiondoka na kukaa nje ya nchi kwa miezi sita, lakini shughuli za chama zilikuwa zinaendelea.


“Aondoke Maalim Seif au afe, hapatakuwa na kitu kitakachoharibika," alisema.

"Nakiri tupo hapa katika kuijenga taasisi ya ACT-Wazalendo, siyo kumtegemea mtu.
Tusisahau wananchi nao wana mapenzi yao, kama watu wana imani na Maalim Seif, kwa nini hawana imani na Dk. Ali Mohamed Shein? 

"Tujiulize 'kwa nini Maalim Seif?' Jibu ni rahisi ni kwamba sijikwezi, ninatembelea watu vijijini, ninakula na kulala nao, ndiyo maana watu wakaniona ni mwenzao, hiyo ndiyo siri ya uongozi nendeni kwa wananchi."


MALI ZA CUF


Katika mkutano huo, Maalim Seif aliulizwa na waandishi wa habari kuhusu bendera za CUF kushushwa kwenye majengo ya ofisi za chama hicho maeneo mbalimbali nchini na kusema kuwa huko kunaitwa "kushusha tanga na kupandisha tanga ili safari iendelee".


“Sisi rasilimali yetu ni wanachama wetu, CUF ni maskini sana, hakina fedha lakini kinatisha kwa sababu ya rasilimali watu," alisema.

Maalim Seif aliongeza: "Majengo karibu yote ya CUF si ya chama, wanachama wenyewe wamejitolea au kukodisha majengo yao au kukiazima chama. Sasa kama mwanachama huyo alikuwa CUF na anahamia ACT-Wazalendo, kwa nini aendelee kupeperusha bendera ya CUF?


“Kuna majengo matatu kwa Zanzibar na Bara ambayo yana majina ya CUF -- makao makuu Buguruni, ofisi ya Mtendeni na Kilimahewa ambayo hatujayagusa, tumechukua vitu vyetu mapema. Kama wanaamini chama hujengwa na bendera na majengo, wayachukue, sisi tunaamini chama ni watu."


Alimshukuru Zitto na uongozi wa ACT-Wazalendo kwa kuwapokea ili waongeze nguvu katika ujenzi wa chama hicho na demokrasia nchini.


"Hamkuwa najisi, mkasema milango ipo wazi tuje, tunajua haukuwa uamuzi wa viongozi pekee, bali pia wanachama, namshukuru Venance Msebo kwa kugomboa kadi namba moja ambaye amesema nipewe mimi na amelipa ada ya miaka 10," alisema.


KUZUNGUKA UKAWA

Alisema wameingia kwenye chama hicho baada ya kuzunguka vyama vinne vinavyounganishwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).


“Tumekwenda Chadema, NLD na NCCR Mageuzi, lakini kwa sababu ACT-Wazalendo walishapeleka maombi kujiunga Ukawa, tumekichagua chama hiki ili roho zetu ziridhike. ACT-Wazalendo ni chama makini na kina misingi imara," alisema.


Maalim Seif alidai chama hicho kinafanya siasa na si propaganda na kwamba kimejipambanua ndiyo maana wameona hapo ndipo eneo la kwenda.


Alimsifia Zitto kwa kumwelezea kuwa ana ujasiri wa kipekee, hatoi matamko bila kufanya utafiti na akishaufanya, haogopi kusema hadharani na si kiongozi wa kujikomba kwa wakubwa.


"Ndugu zangu mjiepushe na jambo moja, mtachokozwa hasa kwenye mitandao ya kijamii. Msikubali kuchokozeka wala msijibizane nao, nguvu zao ni pale mnapowajibu. Uhalali wao ni majibizano, tutawale mitandao kwa fikra, wengi wenu mnawaza hayo ni maneno ya mtu mzima," alisema.


HATIMA WABUNGE CUF


Alisema wabunge wa CUF wanaomuunga mkono wana uhuru wao wa kutafakari faida na hasara za kuhama kwa sasa pamoja na hasara na faida za kutohama chama kwa sasa.


Maalim Seif aliyewahi kushika nafasi za juu za uongozi serikalini, aliulizwa kama atawania tena urais katika Uchaguzi Mkuu mwakani, akasema wakati wa kuzungumzia suala hilo haujafika.


Kiongozi wa ACT-Wazalendo (Zitto) alisema uamuzi wa Maalim Seif ni somo kwa viongozi wa vyama kuona umuhimu wa kujenga demokrasia na imani ya watu wanaowapa dhamana na wanakuwa tayari kufanya lolote ili wafike walikokubaliana.


Kuhusu kadi ya Maalim Seif, Zitto alisema: "Baadhi ya viongozi wetu waliochukua kadi za 'premier' (za hadhi ya juu) huko nyuma, walikumbwa na dhoruba. Jana (juzi) tulipokuwa tunazikusanya, kiongozi mmoja akasema zipo kadi ambazo zinatakiwa kukombolewa kutokana na viongozi wake kwa sasa kutokuwapo.


"Kadi ya Maalim Seif imekombolewa na mwanachama ambaye ni Mwenyekiti wa Mambo ya Nje, Venance Msebo," alisema. 


Uamuzi wa Maalim Seif kujiunga na ACT-Wazalendo pia ulipongezwa na Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma), Hashimu Rungwe, aliyehudhuria mkutano huo.


Zitto aliwataja baadhi waliojiunga na chama chake na nafasi zao CUF ni Juma Duni Haji (Makamu Mwenyekiti wa CUF (mgombea Mwenza wa urais wa Ukawa 2015), Joran Bashange (Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara) na Nassor Mazrui (Naibu Mkuu wa CUF Zanzibar).


Wengine ni Abubakar Bakary (Jaji mstaafu na mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi), Hamad Hamad (Mjumbe Baraza Kuu la Uongozi Taifa), Kulthum Mchuchuli (Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Sheria) na Mbarala Maharagande (Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi).


Pia wamo Ismail Ladhu (Mkurugenzi wa Mambo ya Nje), Omari Shehe (Mkurugenzi wa Mpango na Uchaguzi), Mustafa Wandwi (Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama), Bonifasia Mapunda (mjumbe wa Baraza Kuu Taifa) na Najma Khalfan (mjumbe wa Baraza Kuu Taifa).


KAULI YA LIPUMBA


Wakati Maalim Seif akichukua uamuzi huo, Mwenyekiti wa CUF, Prof. Lipumba, amewataka wabunge wa chama hicho kuungana na wanachama kukijenga chama.


Alidai kitendo cha Maalim Seif kutangaza kuhamia ACT-Wazalendo ni uharibifu wa chama chao na atakwenda kuharibu huko alikohamia.


Akizungumza na waandishi wa habari jana, alidai kuwa: "Ubinafsi wa Maalim Seif usitufarakanishe. Leo (jana) hii anahama, anakwenda ACT, anawaambia wabunge nao wamfuate.


"Kama alivyowatosa wawakilishi, anataka wao (wabunge) pia, kuonyesha tu ubabe kwamba hawezi kufanyakazi na Lipumba, wabunge msikubali, tuungane kukijenga chama."


Prof. Lipumba pia aliwaomba wanachama wa CUF hususani wa Zanzibar kuendelea kukiunga mkono chama hicho.


"Wito wangu ni kwa wanachama hususani Zanzibar, waendelee kutuunga mkono. Tumetoka mbali katika kudai haki ya nchi yetu, sisi ndiyo tulikuwa mstari wa mbele kudai haki ya katiba mpya, utawala bora na kupambana na rushwa. Wasikubali kushikiwa akili na Maalim Seif, wakaacha haki yao ya kudai haki."


BOBALI AJIUNGA 


Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF), jana alitangaza katika mkutano huo wa Prof. Lipumba na waandishi wa habari kuwa, ameamua kuunga mkono juhudi za kukijenga chama hicho.


Bobali ambaye alikuwa miongoni mwa wabunge wa CUF wanaomuunga mkono Maalim Seif, alisema amekubaliana na uamuzi wa Mahakama Kuu, hivyo haoni sababu kuhama chama.


"Kimsingi, tulikubaliana uamuzi wa mahakama uheshimiwe. Tulikubaliana tunakwenda kutafuta haki na baada ya uamuzi tutakwenda kukijenga chama," alisema na kuongeza:


"Sikujua kama upande niliokuwa, ulikusudia ukishindwa, unahama chama, na kama ningejua, nisingekuwa sehemu ya mgogoro."

Mbunge huyo aliwaomba radhi wanachama wote wa CUF na kutoa wito kwa wabunge wenzake, madiwani na wenyeviti waungane kukijenga chama hicho.


"Huko kwingine wanakokimbilia hakuna mwelekeo, yamefanyika maamuzi ya hasira tu," Bobali alisema.

*Imeandaliwa na Beatrice Shayo na Romana Mallya