Maalim Seif aacha CUF ruzuku bilioni 1/-

01Apr 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Maalim Seif aacha CUF ruzuku bilioni 1/-

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, amesema anawashukuru waliokwenda mahakamani kuzuia chama hicho kulipwa ruzuku kwa kuwa sasa kina malimbikizo ya ruzuku yanayofikia Sh. bilioni moja.

Miaka miwili iliyopita, wanachama na wabunge wa CUF waliokuwa wanamuunga mkono aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, walifungua kesi Mahakama Kuu wakiiomba iizuie serikali kutoa ruzuku kwa chama hicho hadi pale mgogoro wa uongozi utakapomalizika.

Tayari Maalim Seif ameshatangaza kukihama chama hicho, akijiunga na Chama cha ACT-Wazalendo kinachoongozwa na Zitto Kabwe.

Wakati Maalim Seif akitimkia ACT-Wazalendo, Prof. Lipumba mwishoni mwa wiki aliweka wazi kuwa anawashukuru waliofungua kesi kortini kuzuia ruzuku ya CUF kwa kuwa sasa kuna malimbikizo makubwa ya ruzuku kutokana na zuio hilo.

Prof. Lipumba (66), aliweka wazi kuwa kwa sasa wameruhusiwa kuitumia ruzuku hiyo iliyokuwa imezuiwa awali na Mahakama Kuu baada ya kufunguliwa kwa kesi ya kupinga kutolewa kwake.

“Tena tunawashukuru wale waliozuia ruzuku kwa sababu wamezuia ruzuku pakawa na malimbikizo, sasa yale malimbikizo yakawa yamekuwa makubwa, nadhani ilikuwa karibu (shilingi) bilioni," Prof. Lipumba alisema.

Maalim Seif na wenzake walifungua maombi namba 80 ya mwaka 2017 katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wakiiomba itoe zuio kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kutoa ruzuku kwa CUF hadi pale kesi zote za chama hicho zitakapokwisha.

Ombi hilo lilikubaliwa na Jaji Wilfred Dyansobera kwa maelezo kwamba fedha hizo ambazo hutolewa na serikali, zisitolewe kwa chama hicho kwa kuwa kuna mgogoro wa kiuongozi.

Maalim Seif alitangaza kuihama CUF na kujiunga na ACT-Wazalendo muda mfupi baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutoa uamuzi wa kumtambua Prof. Lipumba kuwa Mwenyekiti halali wa CUF na kuhitimisha rasmi mgogoro wa kiuongozi uliodumu kwa takriban miaka mitatu ndani ya chama hicho.

Mgogoro huo ulianza Agosti 2015, Prof. Lipumba alipoandika barua ya kujiuzulu nafasi yake ndani ya CUF akieleza kutofurahishwa na uamuzi wa vyama vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kumpa nafasi Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kuwania nafasi chini ya mwamvuli wa umoja huo.

Mbali na CUF, Ukawa uliundwa na vyama vingine vitatu vya siasa ambavyo ni Chadema, NLD na NCCR-Mageuzi na Prof. Lipumba alikuwa miongoni mwa wenyeviti wenza wa umoja huo.

Habari Kubwa