Maalim Seif aivuruga CUF

19Mar 2019
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Maalim Seif aivuruga CUF

ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amekitikisa chama hicho baada ya kujivua uanachama na kujiunga na Chama cha ACT-Wazalendo.

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kuhusu kujiunga na chama cha ACT-Wazalendo. Kushoto ni aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui. PICHA: MPIGAPICHA WETU

Maalim Self aliyewahi kushika nafasi za juu katika uongozi serikalini, alitangaza uamuzi huo jana, jijini Dar es Salaam, muda mfupi baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kubariki uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa kumtambua Prof. Lipumba kuwa Mwenyekiti wa CUF.

Mara tu baada ya mwanasiasa huyo kutangaza uamuzi huo mbele ya waandishi wa habari, bendera za CUF zilionekana zikishushwa katika ofisi mbalimbali za CUF nchini.

Visiwani Zanzibar, kunakoaminika kuwa ngome kuu ya CUF, ofisi ya makao makuu ya chama hicho iliyoko Mtendeni, ilifungwa, huku bendera za chama hicho pia zikishushwa muda mfupi baada ya Maalim Seif kutangaza uamuzi wa kujiunga na ACT-Wazalendo.

Hali kama hiyo ilionekana mjini Tanga ambako uongozi wa CUF Wilaya ya Tanga uliagiza kushusha bendera chama hicho na kupandisha za ACT-Wazalendo katika ofisi zao zote wilayani humo.

Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Tanga, Rashid Jumbe, alisema jana kuwa uongozi wao umeamua ofisi za wilaya na kata zote 27 wilayani mwake washushe bendera za chama hicho na kupandisha za ACT-Wazalendo.

Alidai tayari agizo hilo limeshatekelezwa na kuanzia leo, kila aliyekuwa kiongozi wa CUF atakuwa na jukumu la kupokea wanachama wa CUF na kuwapa kadi za ACT-Wazalendo.

"Zoezi la leo (jana) ni kushusha bendera zote za CUF wilaya nzima na kesho (leo) ni kazi ya kupokea wanachama wa CUF kwenye ofisi na matawi yote na kuchora nembo za ACT na kufuta za CUF, Jumbe alisema.

Baadhi ya wanachama wa CUF wilayani hapa pia walionekana wakichana na wengine kuchoma moto kadi za uanachama wa chama hicho muda mfupi baada ya Maalim Seif kutangaza kukihama CUF.

Jumbe aliahidi kuzungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo ili kutoa idadi kamili ya wanachama wa CUF walioamua kumfuata Maalim Seif ACT-Wazalendo.

SABABU ZA KUHAMA

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, alisema ameamua kuondoka CUF kwa kuwa hana tena muda wa kulumbana.

"Natangaza kwamba mambo ya malumbano yamekwisha, sasa ni mapambano ya kujenga siasa, malumbano hatuna haja nayo tena," Maalim Seif alisema na kuongeza:

"Ninakiri kwamba nimetumia muda mrefu sana kuijenga CUF, na ni kweli nyumba ukiizoea, kuihama ni tabu, lakini tukumbuke kwamba hata wakati mwingine tunazaa watoto tunaowapenda lakini Mwenyezi Mungu anawachukua na maisha yanaendelea."

Maalim Seif alisema kuwa kabla ya kufikia uamuzi huo wa kutimkia ACT, alitembelea baadhi ya vyama na kuwauliza kama vilikuwa tayari kumpokea.

"Kabla ya kuchukua maamuzi haya, tulitembelea baadhi ya vyama ili kuwaambia ikitokea sisi tumehama CUF, wako tayari kutukaribisha na kwa masharti gani, kuna mmoja alituambia kwamba yuko tayari kutukaribisha, lakini masharti je, tunaweza? "Baada ya hapo tulikaa na kuchambua, tukaona kwamba ACT-Wazalendo masharti yao siyo magumu na tulisoma katiba yao, tukaona kwamba inatufaa.

“Sasa malumbano yamekwisha, sasa hivi ni kujenga, kama wanataka kuchukua ofisi na mali zao waende wakachukue, lakini ofisi nyingi za CUF ni za watu binafsi, walituazima majengo, sasa ni uamuzi wa wenye majengo na si letu tena," Maalim Seif alisema.

Mwanasiasa huyo mzoefu alisema yuko tayari kuwa mwanachama wa kawaida ndani ya ACT na haangalii nafasi aliyokuwa nayo ndani ya CUF.

"Sisi tumetafuta mahali ambapo tunaamini tutaendeleza mapambano ya siasa, hatuangalii vyeo, niko tayari kuwa mwanachama wa kawaida mradi mapambano ya kisiasa yaendelee.

"Wale wanaohama vyama na kutaka vyeo hawana nia ya kupambana kisiasa. Kwetu sisi kuhama na nyazifa zetu haina shida. "Kauli yangu kwa wanachama wa CUF na Watanzania wote, kwamba wakati ni sasa wa kushusha tanga na kupandisha tanga, safari iendelee, mzigo wa CUF tumeutupa, hatuna habari tena na chama hicho, mambo yamekwisha na sasa ni kusonga mbele.

 

 

HATIMA WABUNGE CUF

Alipoulizwa kuhusu hatima ya wabunge wanaotokana na chama cha CUF wanaomuunga mkono, Maalim Seif alisema wataendelea kuwa wanachama wa chama hicho.

"Wabunge wataendelea kuwa wanachama wa CUF, tumewaachia wao isipokuwa wakiamua kujiunga na ACT-Wazalendo ni wao, kama wataamua kubaki hukohuko pia ni sawa, sisi hatuna uamuzi juu yao," Maalim Seif alisema.

Aliongeza kuwa yuko tayari kushirikiana na vyama vingine katika kuendeleza mapambano ya kisiasa nchini. “Tuko tayari kushirikiana na vyama vyote makini, kama ni Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi) au hata kama utabadilika, mradi ni vyama makini, tutashirikiana navyo," Maalim Seif alisema.

CUF imekuwa katika mgogoro wa uongozi tangu mwaka 2015, Prof. Lipumba alipoandika barua ya kujiuzulu nafasi ya uenyekiti wa chama hicho akieleza kutofurahia uamuzi wa Ukawa kumpa nafasi Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuuwakilisha kusaka kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu uliopita.

Hata hivyo, mtaalamu huyo wa uchumi alirejea kwenye chama hicho baada ya uchaguzi huo na kutangaza kutengua barua ya kujiuzulu kwake, huku uamuzi wake ukipata baraka za Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini. Ukawa uliundwa na vyama vinne ambavyo ni Chadema, CUF, NCCR – Mageuzi na NLD.

*Imeandaliwa na Elizabeth Zaya (DAR), Rahma Suleiman (ZANZIBAR) na Dege Masoli (TANGA).