Maalim Seif ajitosa urais wa Zanzibar

06Jul 2020
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Maalim Seif ajitosa urais wa Zanzibar

MWENYEKITI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, amechukua fomu ya kuwania urais wa Zanzibar kupitia chama hicho ikiwa ni mara ya sita kuwania nafasi hiyo tangu mwaka 1995, alipokuwa Chama cha Wananchi (CUF).

Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Seif Sharif Hamad, akichukua fomu za kuomba kuteuliwa kuwa mgombea wa urais Zanzibar kutoka kwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu katika ofisi za Vuga mjini Unguja jana. PICHA: RAHMA SULEIMAN

Akizungumza jana baada ya kuchukua fomu hiyo majira ya saa 4:00 asubuhi katika ofisi za chama hicho Vuga, alisema endapo atapata ridhaa ya kuwaongoza Wazanzibari ndani ya miaka mitano ataleta maendeleo ya haraka kwa siku 100.

Maalim Seif alikabidhiwa fomu hizo na Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu na kusindikizwa na wafuasi wa chama hicho.

Alisema ameamua kuchukua fomu za urais ili chama chake cha ACT -Wazalaendo wamfikirie kuwa mgombea wa chama hicho na kuahidi kuwa endapo atachaguliwa ataleta maendeleo ya haraka.

Alisema lengo kuu la kujitokeza kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo ni kuiletea maendeleo Zanzibar ndani ya kipindi kifupi na kuwastaajabisha Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla.

“Endapo chama changu kitanipa ridhaa ya kupeperusha bendera ya urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2020 na wananchi watanichagua kuongoza Zanzibar, nitaleta maendeleo ya haraka kwa siku 100 tu,” alisema.

Alisema kwa sasa anasubiri chama kifanye kazi yake kwa kuchagua mgombea ambaye atapeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu.

“Huu si wakati wa kufanya kampeni ndugu zangu waandishi wa habari hivyo, niache nikasome kilichokuwa humu na kuwaachia kazi yake chama changu kukaa na kumchagua yeyote atakayefaa kupeperusha bendera ya chama hichi,” alisema Maalim Seif.

Pia, aliwaomba wanachama ambao wana sifa wajitokeza kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo ya urais wa Zanzibar na nafasi nyingine za uwakilishi, ubunge na udiwani.

Naye Katibu Mkuu wa chama hicho, Shaibu alisema kwamba tangu uchukuaji fomu uanze katika chama chao Julai mosi, wanafarijika kuona wanachama wengi wamejitokeza kuitikia kwa wingi kuchukua fomu kwa nafasi mbalimbali.

“Leo ni mwendelezo wa uchukuaji fomu ambapo umeitikiwa kwa wingi na wanachama wetu ambao wamejitokeza kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya udiwani, uwakilishi, ubunge kwa Zanzibar na Tanzania Bara,” alieleza Shaibu.

Pia, alisema ACT –Wazalendo itahakikisha zoezi zima la kuomba nafasi mbalimbali litaendeshwa kwa kuzingatia demokrasia, haki na uwazi na chama watakuwa wakali kwa mtu yeyote atakayejishirikisha katika utoaji wa rushwa.

Maalim Seif akipitishwa kugombea nafasi hiyo atachuana na wagombea wengine wa vyama vingine vya siasa huku mpinzani mkubwa akiwa ni kutoka Chama Cha Mapinduzi.

HASHIMU JUMA ISSA AHITOSA CHADEMA

Kwa upande wa Chama cha Demokrasiana Mandeleo (CHADEMA), visiwani Zanzibar, aliyechukua fomu ya kuomba kupeperusha bendera ni Hashimu Juma Issa.

Alichukua fomu hiyo jana kwenye Ofisi ya Makao Mkuu Zanzibar, alikabidhiwa na Mkuu wa Idara ya Oganaizesheni na Uchaguzi wa CHADEMA Zanzibar, Kado Salmini Mwalimu.

Haya hivyo, Hashimu hakuzungumza chochote kabla na baada ya kuchukua fomu hizo kuhusiana na mipango, mikakati na mambo anayotarajia kuifanyia Zanzibar ikiwa chana chake kitamteua kugombea na baadaye kuchaguliwa na Wazanzibari kuwa rais wa nane.

Habari Kubwa