Maalim Seif akabidhiwa kada namba moja ACT Wazalendo

19Mar 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Maalim Seif akabidhiwa kada namba moja ACT Wazalendo

Mwanachama mpya wa ACT Wazalendo, Maalim Seif Hamad amesema amehemewa na mapokezi ya kindugu ambayo ameyapata ikiwa ni mara ya kwanza kukanyanga katika ofisi za chama hicho.

KIONGOZI WA ACT WAZALENDO ZITTO KABWE ALIPOMKABIDHI KADA YA UANACHAMA MWANACHAMA MPYA WA CHAMA HICHO MAALIM SEIF SHARIFF HAMAD, JIJINI DAR ES SALAAM, PICHA ROMANA MALYA

Maalim Seif amesema anamshukuru mwenyekiti wa chama hicho kwa kukubali kuwapokea ili waongeze nguvu.

"Hamkuwa najisi mkasema milango ipo wazi tuje, haukuwa uamuzi wa viongozi pekee bali pia wanachama, namshukuru Venance Msebo kwa kukomboa kadi namba moja akasema nipewe mimi na amelipa ada ya miaka 10, " amesema Maalim Seif.

Maalim Seif amesema pamoja na wanachama wengine waliojiunga leo wameridhika na utendaji wa ACT Wazalendo, wamekwenda vyama vingine vinne ChADEMA, NLD na NCCR Mageuzi lakini kwa sababu ACT Wazalendo walishaoeleka maombi kujiunga ukawa, hivyo wamekichagua hiki ili roho zao ziridhike.

Aidha Maalim Seif amesema walipokuwa CUF walijitahidi kujenga taasisi ndio maana alikuwa akiondoka nchini miezi sita chama kinaendelea.

"Naamini ACT Wazalendo tupo katika kujenga taasisi siyo kutegemea mtu msisahau wananchi wana wapenzi wao, kama watu wanaimani na Maalim Seif kwa nini hawana imani na Shein? Maalim Seif hajajikweza, anatembelea watu katika vijiji vyao anakula na kulala nao na hiyo ndio siri ya kiongozi," amesema Maalim Seif.

Kwa upande wake Kiongozi Mkuu wa Chama hicho na Zitto Kabwe, amesema alichokifanya Maalim Seif ni somo la kuona umuhimu wa kujenga demokrasia na imani ya watu wanaowapa dhamana ambao wanakuwa tayari kufanya lolote ili wafikie walilokubaliana.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Mwenyekiti wa Chama cha Umma, Hashimu Rugwe, ambaye alikuja kwa niaba ya vyama 10 vilivyoungana pamoja katika kudai demokrasia.