Maalim Seif aliponza Jeshi la  Polisi

01Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
ZANZIBAR
Nipashe
Maalim Seif aliponza Jeshi la  Polisi

NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, amelitaka Jeshi la Polisi litafakari uwapo wake baada ya kuruhusu mwanachama mpya wa ACT-Wazalendo, Maalim Seif Shariff, kufanya mikutano ya kisiasa visiwani Zanzibar kinyume cha maagizo yaliyotolewa.

Maalim Seif Shariff.

Masauni alitoa kauli hiyo juzi jioni wakati wa uzinduzi wa mradi wa maji kwenye eneo la nyumba mpya za polisi zilizoko Mahonda, Unguja.

Alisema katika kipindi cha hivi karibuni alikuwa akifuatilia mitandao ya jamii na kushuhudia Maalim Seif akipokewa kwa maandamano maeneo ya Tumbatu.

"Nilipoulizwa nikaambiwa ameweka magunia, ndiyo majibu yaliyotolewa, huyu mzee siyo kiongozi wa chama chochote cha siasa, maelekezo yaliyotolewa na yanayoendelea kusimamiwa hadi sasa ambayo alitoa Amiri Jeshi Mkuu wa Nchi (Rais John Magufuli), akayazungumza Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi (Kangi Lugola) na mimi nikayasisitiza.

"Kutokana na kazi kubwa ambazo serikali zetu mbili ya Muungano na ya Mapinduzi Zanzibar zinazifanya, wananchi sasa hivi wanahitajika kufanya shughuli za maendeleo na waliopewa dhamana ya wananchi kusimamia kutekeleza waliyoahidi.

"Tunatarajia mikutano ya hadhara ifanywe na viongozi waliochaguliwa kihalali na wananchi katika majimbo yao, hayo ndiyo maelekezo ya serikali.

"Amiri Jeshi Mkuu alishaagiza, Waziri alishaagiza na mimi naibu wake niliongezea nguvu. Leo (juzi) nataka kuacha maswali hapa, bahati mbaya kamishna wa polisi hayupo hapa, lakini ujumbe utamfikia. Ninauliza - je, mnamwogopa, mnadharau na kukebei maelekezo ya viongozi?" Masauni alihoji.

Kiongozi huyo alisema lazima nchi iongozwe kwa misingi ya nidhamu na askari wa Jeshi la Polisi walijifunza jambo hilo na kuapa.

"Haiwezekani maelekezo ambayo yanalenga kujenga misingi ya amani na utulivu katika nchi na maendeleo yachezewe. Haya ndiyo maswali nimeacha mjitathmini, mnipatie majibu.  Sidhani kama jambo hilo litabaki kama lilivyo hivi sasa, ninazungumza kwa upendo," alisema.

KONGAMANO LAVUNJIKA

Wakati Masauni akitoa maelekezo hayo, kongamano la maridhiano ambalo lilifanyika jana visiwani Zanzibar lilivunjika majira ya saa sita mchana kutokana na Maalif Seif aliyekuwa kiongozi wake, kutakiwa kuripoti kwa Jeshi la Polisi.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa ACT-Wazalendo, Salim Bimani, aliiambia Nipashe jana kuwa wakati wakiwa wanaendelea na kongamano hilo, walifika maofisa wa Jeshi la Polisi na kuwataka walivunje.

Alidai maofisa hao pia walimtaka Maalim Seif kufika Kituo cha Polisi Madema kwa ajili ya mahojiano.

"Wakati Maalim Seif akijiandaa kwenda polisi, akapigiwa simu kuwa asiende tena," Bimani alisema.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharib Unguja, Thobias Sedeyoka, alidai jeshi hilo halijavunja wala kuzuia kongomano hilo.

"Sisi Jeshi la Polisi hatujazuia wala kuvunja kongamano maana hiyo ni mikutano yao ya ndani, labda walikuwa washamaliza muda wao wa kufanya kongamano lakini wasisingizie kuwa tumevunja," alisema,

Kongamano hilo lilikuwa maalum kuadhimisha siku ya maridhiano. Julai 31, 2010 wananchi wa Zanzibar walipiga kura ya maoni kuchagua mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa uanze kutekelezwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Habari Kubwa