Maalim Seif atamba kumaliza kazi Pemba

20Sep 2020
Na Mwandishi Wetu
Pemba
Nipashe
Maalim Seif atamba kumaliza kazi Pemba

MGOMBEA urais wa Zanzibar (ACT-Wazalendo), Maalim Seif Sharif Hamad, amekamilisha awamu ya kwanza ya ziara yake ya mikutano ya kampeni katika majimbo ya Visiwa vya Pemba na sasa anaelekeza nguvu zake Unguja.

Awamu hiyo ya kwanza iliisha juzi, akifanya mikutano mitano ukiwamo wa ufunguzi wa kampeni.

Ofisa Habari wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Abeid Khamis Bakar, alisema jana kuwa Maalim Seif mbali na kufanya kampeni za majukwaani, alizuru kwenye maeneo ya wananchi na kujionea shughuli zao za kimaisha.

Alisema mgombea wao huyo alitembelea maeneo ya kilimo cha mboga, mwani, wavuvi, wafugaji wa kuku na wafanyabiashara.

“Wananchi wengi walionekana kuvutiwa na kitendo chake hicho cha kutembelea maeneo yao kwa kuwa ni njia ya kuelewa matatizo ya wananchi na kupanga pamoja njia za kuyatatua.

"Maalim Seif aliwaomba wananchi wampigie kura Oktoba 28 na yeye atahakikisha matatizo yanayowakabili anayatua ndani ya miezi sita ya mwanzo ya uongozi wake," Bakari alisema.

Katika taarifa yake, Bakari alisema Maalim Seif amedai kushangazwa na hatua ya serikali ya kujali zaidi mapato kutoka kwa wafanyabiashara, lakini haiwatengenezei mazingira mazuri ya ufanyajibiashara.

Maalim Seif pia alikumbusha umuhimu wa wasimamizi wa uchaguzi kutenda haki katika uchaguzi huo ili kuepusha migogoro itokanayo na uchaguzi.

Habari Kubwa