Maalim Seif atoa masharti kukubali matokeo

22Oct 2020
Thobias Mwanakatwe
Dar es Salaam
Nipashe
Maalim Seif atoa masharti kukubali matokeo

MGOMBEA urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT- Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema atakubali matokeo ya uchaguzi hata kama atashindwa ikiwa uchaguzi utakuwa huru na wa haki.

Maalim Seif alitoa masharti hayo jana alfajiri wakati akihojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kuhusiana na mambo mbalimbali kuelekea uchaguzi mkuu.

Alisema hayo baada ya kuulizwa kama atakubali matokeo yakionyesha ameshindwa kwa mara nyingine.

"Nimewaambia ikiwa uchaguzi utakuwa huru na wa haki, mimi sina tatizo kumpongeza Dk. Hussein Mwinyi (mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi- CCM)," alisema.

Hii ni mara ya sita kwa Maalim Seif kugombea urais wa Zanzibar.

Akizungumzia suala la wagombea wa ACT-Wazalendo ambao wameenguliwa kugombea katika nafasi mbalimbali, alisema chama kilifuata njia za kisheria kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC). Alisema kutokana na hatua hiyo, baadhi walirejeshwa na wengine hawakurejeshwa.

"Tulikata rufaa (rufani) kwa ZEC kwa wale wa Baraza la Uwakilishi wengine wamerejeshwa. Tunakwenda kwenye uchaguzi maeneo mengine ACT- Wazalendo haina wagombea," alisema.

Maalim Seif alisema wagombea wa nafasi ya uwakilishi ambao hawajarejeshwa itakuwa imeshatoka lakini kwa nafasi ya ubunge sheria inaruhusu baada ya uchaguzi wanaweza kufungua kesi mahakamani.

Kuhusu vipaumbele vyake ikiwa atapewa ridhaa ya kuwa rais, alisema kitu cha kwanza atakachokifanya ni kuunganisha wananchi wa Zanzibar ili kuleta maendeleo.

Maalim Seif pia alisema atainua hali ya maisha ya wananchi ambayo hivi sasa wanakabiliwa na hali ya umaskini kiasi kwamba hata mlo kwa siku umekuwa wa taabu.

Habari Kubwa