Maalim Seif: Kampeni zangu zimeenda vizuri

26Oct 2020
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
Maalim Seif: Kampeni zangu zimeenda vizuri

CHAMA cha ACT-Wazalendo jana, kilifunga kampeni zake katika viwanja vya Mnazi Mmoja Mjini Zanzibar, maelfu ya wananchi na wafuasi wa chama hicho walifurika viwanjani hapo.

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema kampeni zake zimeenda vizuri, hivyo endapo atakuwa rais, wananchi wategemee mambo mazuri ikiwamo kuboresha maisha yao.

Alieleza kuwa ataongeza mishahara ya watumishi wote na Zanzibar itanawiri.

"Nitaondoa uenevu, udhalilishaji na ukandamizaji,” alisema Maalim Seif, ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho.

Alieleza kuwa anashangaa Zanzibar kuendeshwa kijeshi, kila kona jeshi limetawala. Hata hivyo, hatutoa ufafanuzi wa kauli hiyo.

Maalim Seif alieleza kuwa hawatosusia uchaguzi mwaka huu, licha ya hujuma mbalimbali zinazofanywa dhidi yao.

Katika mkutano huo chama hicho kilipitisha bakuli la kuchangia chama, jumla ya shilingi milioni tatu zilipatikana viwanjani hapo kwa kutunisha mfuko kwa ajili ya uchaguzi.

Awali, hamasa na shauku, shangwe na nderemo za wafuasi hao ziliibuka wakati Naibu Katibu wa chama hicho Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, kuingia kiwanjani hapo majira ya saa 9:00 za jioni baada ya kuachiliwa akidaiwa kutekwa na watu wasiojulikana.

Mazrui alidai kutekwa majira ya asubuhi eneo la Sateni Mjini Unguja wakati akielekea ofisini kwake Vuga.

Akizungumza katika mkutano huo, alisema siku ya jana ilikuwa ni ngumu sana kwake, lakini ameridhika kwa sababu ni ukombozi wa Wazanzibari.

"Nilipofika eneo la Sateni majira ya saa mbili ilikuja gari aina ya Prado ikatugonga na kupiga risasi juu na kuekewa bastola sita katika uso wangu na kubebwa, kufunikwa uso wote na kukabwa koo,” alidai.

Alieleza kuwa saa saba mchana alitupwa katika pori la Bweleo na wale wanaosambaza kuwa hajatekwa ni waongo.

Alisema kila raia anahaki ya kushiriki katika siasa bila ya ubaguzi na ni haki ya kila mwananchi.

Akizungumza katika mkutano huo, Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, Juma Duni Haji, aliendelea kusema msisitizo wao kuwa wataenda kupiga kura Oktoba 27 ambayo ni siku ya kupiga kura ya mapema ambayo hupiga watu maalum kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi.

Alisema wanataka kuleta mabadiliko ya utawala kwa sababu wameshateseka sana katika kutaka mabadiliko.

Habari Kubwa