Maalim Seif: Lowassa kavunja moyo upinzani

19Mar 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Maalim Seif: Lowassa kavunja moyo upinzani

MWENYEKITI wa ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema kitendo cha Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, kurudi Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeuvunja moyo upinzani.

MWENYEKITI wa ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, picha mtandao

Machi Mosi, 2019, Lowassa alitangaza kurejea CCM akitokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alikokaa takribani miaka mitatu.

Lowassa alijiondoa CCM mwaka 2015, baada ya vikao vya juu vya chama hicho kukata jina lake katika mchakato wa uteuzi wa mgombea wake wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika uchaguzi wa mwaka 2015, Lowassa aliwania kiti cha urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) akipambana na John Magufuli ambaye alimshinda kwa kupata kura 8,882,935 sawa na asilimia 58.46, huku Lowassa akijipatia kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.97 ya kura zote.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Maalim Seif alisema: “Sisi upinzani tumevunjika moyo kwa kitendo chake cha kuhama Chadema na kwenda CCM, ambayo alikuwa akiipinga.

“Unaweza kufahamu Lowassa siyo kama Maalim Seif. Maalim Seif kazoea upinzani na mateso yake yote anavumilia, yeye alikuwa Waziri Mkuu na marupurupu yote kwa hiyo lile alilotegemea kulipata katika Ukawa hakulipata. Vile vile tunasikia Chadema haikumtendea vyema,” alisema.

Hata hivyo, Maalim Seif alisema kuondoka kwa Lowassa Chadema ana sababu nyingi, hivyo hawezi kumhukumu.

AFUNGUKA KIKWAZO NA LIPUMBA

Maalim Seif ambaye kabla ya kuhamia ACT-Wazalendo, alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), alikiri kuwa yeye ndiye aliyekataa kupatanishwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Prof. Ibrahim Lipumba, walipoingia katika mgogoro mkubwa baacha ya uchaguzi mkuu wa 2015.

“Sikumsusia, tukionana tunasalimia vizuri ila kufanya naye kazi haiwezekani, sina kinyongo naye, lakini siwezi kufanya kazi na mtu ambaye kanisaliti.

“Kama kanichoma mkuki mchana, usiku atafanya nini?” Alihoji Maalim Seif na kuongeza: “Simpi tena nafasi nyingine.”

Habari Kubwa