Maambukizi mapya VVU vijana yatisha

02Dec 2021
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
Maambukizi mapya VVU vijana yatisha

MAAMBUKIZI mapya kwa vijana kati ya miaka 15 hadi 24 yamezidi kuongezaka huku wasichana wakiwa vinara katika janga hilo, imebainika.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza Aisha Hassan (kushoto), alipotembelea banda la kundi la Timiza Malengo linalofadhiliwa na Asasi ya Vijana Tanzania (TAYOA), katika maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani jijini Mbeya, jana. Wa (tatu kulia) ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama. PICHA: OWM

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Ajira, Uratibu wa Bunge, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, alisema hayo jana katika maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani ambayo kitaifa yalifanyika jijini hapa.

Mhagama alisema taarifa za utafiti zinaonyesha kuwa maambukizi mapya ya VVU yanawakabili zaidi vijana wenye umri huo na kwamba yamefikia asilimia 40 huku asilimia 80 kati ya hao ni vijana wakike jambo ambalo ni hatari kwa nguvu kazi ya taifa.

Alisema ili kukabiliana na tatizo hilo, serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ukiwamo wa kudhibiti Ukimwi wa mwaka 2018/19 na 2022/23. Mpango huo unalenga kupunguza maambukizi mapya ya VVU, kupunguza vifo vitokanavyo na VVU  na kuhakikisha watu wanaoishi na maambukizi ya VVU wanaendelea kutumia dawa.

Waziri Mhagama alisema kwenye mkakati huo, serikali imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali katika utekelezaji ikiwa ni pamoja na kubadili tabia kwa vijana ili kudhibiti maambukizi mapya.

“Lakini pia tuna mipango maalumu ya kudhibiti maambukizi kwenye mikoa ambayo ina maambukizi makubwa ambayo yako juu ya kiwango cha kitaifa ikiwamo Njombe, Iringa, Mbeya, Kagera na Geita ambayo ipo juu ya kiwango cha kitaifa,” alisema Mhagama.

Alisema kwa sasa kuna baadhi ya mikoa ambayo imebainika kuwa na kasi kubwa ya maambukizi ikiwamo Geita, Simiyu, Manyara na Dodoma.

Pia alisema serikali ina mipango maalumu ya kudhibiti maambukizi mapya kwenye maeneo yenye shughuli maalumu za uzalishaji kama vile migodi na uvuvi kwa kusambaza kondomu pamoja na kutoa elimu ya kujikinga.

WANAOVUJISHA SIRI WAONYWA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan aliziagiza mamlaka zinazohusika kuwachukulia hatua za kisheria watumishi wa afya wanaovujisha siri za watu wanaoishi na maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU) wanaokwenda kupata huduma kwenye vituo vya afya kwa kuwa ni kinyume cha maadili ya kazi yao.

Pia aliagiza vyombo vya sheria kuwachukulia hatua kali watu wote wanaoendeleza vitendo vya unyanyapaa kwa watu wanaoishi na VVU kwa kuwa vitendo hivyo vinasababisha watu kuogopa kupima na kutumia dawa.

Alisema vitendo hivyo vya unyanyapaa na uvujishaji wa taarifa za watu wanaoishi na maambukizi ya VVU, vinakwaza na kufifisha juhudi za serikali na wadau kupambana na janga hilo la Ukimwi.

“Vitendo na kauli za unyanyapaa na ubaguzi kwa watu wanaoishi na maambukizi ya VVU vinavyoendelea hasa maeneo ya vijijini havikubaliki. Naagiza mamlaka zinazohusika kuchukua hatua dhidi ya watu wanaoendeleza vitendo hivyo,” alisema Majaliwa.

Waziri Mkuu alisema Tanzania imekuwa ikipambana na maambukizi ya VVU kwa muda wa miaka 38 na kwamba kutokana na mapambano hayo mafanikio mbalimbali yamepatikana ikiwemo kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu namna ya kujikinga na maradhi hayo.

Pia alisema Tanzania imeongeza idadi ya watu wanaojitokeza kupima kutoka asilimia 61 ya watu wanaokadiriwa kuishi na VVU mwaka 2016 mpaka asilimia 83 mwaka 2019.

Sambamba na hilo, alisema serikali imeongeza wigo wa upimaji kwa kuanzisha utaratibu wa wananchi kujipima na kwamba vifaa vya kujipimia vinapatikana kwenye maeneo mbalimbali.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), Dk. Leonald Maboko, alisema kwenye maadhimisho hayo walikusanya zaidi ya Sh. Milioni 156.4 kwa ajili ya kutunisha Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi.

Alisema fedha hizo zilikusanywa kwa njia kuu mbili ambazo ilikuwa kuchangia fedha taslimu pamoja na uuzwaji wa fulana maalumu zilizokuwa zimeandaliwa kwa ajili ya maadhimisho hayo.

Pia alisema fedha zilizopatikana kupitia michango ya fedha taslimu ni Sh. milioni 147.6 na kwenye mauzo ya fulana zilipatikana Sh. milioni tisa.

Habari Kubwa