Maambukizi VVU mapenzi ya jinsia moja juu

14Mar 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Maambukizi VVU mapenzi ya jinsia moja juu

KIWANGO cha maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa makundi maalum ikiwamo ngono ya jinsia moja, wanawake wanaofanya biashara ya ngono na wanaojidunga dawa za kulevya ni zaidi ya mara tatu ya jamii ya kawaida.

Mkurugenzi wa ufuatiliaji na tathmini, Dk. Jerome Kamwela, alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza na wadau wa Tume ya Udhibiti wa Ukimwi Nchini (Tacaids).

Alisema utafiti uliofanyika mwaka 2016, unaonyesha kuwa wanaume wanaojihusisha na ngono ya jinsia moja (mashoga) kiwango ni asilimia 22.2 ya kiwango cha kawaida.

“Kiwango cha maambukizi ni watano kati ya 100 basi wanawake wanaofanya biashara za ngono ni 26 kati ya 100,”alisema.

Alisema wanaojidunga dawa za kulevya ni asilimia 15 ya maambukizi ya kawaida katika jamii.

Alisema kiwango kikubwa kwa mujibu wa utafiti mbalimbali nchini, kinaonyesha maambukizi makubwa pia ni katika makundi ya wafanyakazi wanaohama hama, madereva wa masafa marefu na wafungwa,  karibu asilimia tisa wanaishi na VVU.

Alisema waliofikiwa katika utafiti kwa wanaume wanaojihusisha na ngono ya jinsia moja ni 49,000, asilimia 18 walibainika kuwa wanaishi na VVU hata hivyo waliowahi kupima afya zao ni 387.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tacaids, Dk. Leornad Maboko, alisema tathmini iliyofanywa nchini mwaka 2016/17, inaonyesha watu 81,000 nchini wanapata maambukizi kwa mwaka ambayo ni sawa na wastani wa watu 225 kwa siku.

 

Habari Kubwa