Maambukizi VVU yawatikisa vijana

21Nov 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Maambukizi VVU yawatikisa vijana

IMEELEZWA kuwa zaidi ya asilimia 50 ya maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI nchini yapo kwa kundi la vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 35.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, kuhusiana na maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Uwekezaji, Dorothy Mwaluko, alisema umri huo ni kwa mujibu wa Sera ya Vijana ya mwaka 2007.

Alisema maambukizi mapya nchini bado ni tishio, hivyo kuna wajibu wa kutekeleza mikakati yote ya kuhakikisha yanatoweka.

“Takwimu zinaonyesha watu takribani 72,000 wanapata maambukizi mapya kwa mwaka, hiyo ina maana kuwa kwa mwezi watu 6,000, watu 200 hupata kwa siku na kwa saa moja ni watu wanane.

“Kwa takwimu hizi ni lazima tutekeleze mikakati kwa namna mbili, moja kwa kundi lililoambukizwa kwa kuzingatia 90 tatu ili wafubaze virusi na kuendelea kufanya kazi kwani mtaji wa maskini ni nguvu na sio virusi,”alisema.

Alitaja kundi la pili la kuliwekea mikakati ni la wale wasioambukizwa kwa kuweka jitihada ili wasiambukizwe.

“Ili vijana wetu wasiambukizwe ni lazima vijana waongozwe na kauli ya kusema,mwili wake wa huyo kijana ndio maisha yake na maisha yake ndio nguvu ya ujenzi wa taifa lake,” alisisitiza.

Kuhusu maadhimisho ya siku hiyo, Mwaluko alisema kitaifa yatafanyika mji wa Moshi mkoani Kilimanjaro kuanzia Novemba 25 siku ambayo itazinduliwa rasmi kwa kufanya matembezo ya hisani kwa ajili ya kutangaza na kuhamasisha uchangiaji wa mfuko wa UKIMWI (AIDS Trust Fund).

Pia alisema kuanzia Novemba 25 hadi Disemba Mosi, kutakuwa na maonyesho ya shughuli za wadau wa kudhibiti UKIMWI na virusi vya UKIWMI nchini  yakijumuisha na utoaji wa elimu mbalimbali katika viwanja vya Mandela.

Alisema Novemba 26 na 27 kutakuwa na kongamano la kisayansi la kitaifa la kutathimini hali na mwelekeo wa udhibiti wa virusi vya UKIMWI na UKIMWI ikifuatiwa na mdahalo wa vijana Novemba 28 kwa ajili ya kuzungumzia masuala mabalimbali yanayohusiana na afua ya UKIMWI na Virusi vya UKIMWI.

Habari Kubwa