'MAANDAMANO' Polisi watoa nuru kufanyika nchini

23Sep 2016
Na Waandishi Wetu
Nipashe
'MAANDAMANO' Polisi watoa nuru kufanyika nchini

KILIO cha baadhi ya vyama vya siasa kudai mikutano ya hadhara na maandamano kiko mbioni kusikilizwa baada ya jana Jeshi la Polisi kuahidi kuwa litaviruhusu baada ya kufanya tathmini ya kina katika siku za karibuni kuhusu hali ya usalama.

Kamishna wa operesheni na mafunzo , Nsato Mssanzya (pichani)

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa jeshi hilo, Nsato Mssanzya, alisema wameondoa zuio la vyama vya siasa kufanya mikutano ya ndani baada ya kuridhishwa na hali ya kiusalama iliyopo sasa nchini.

Mssanzya alidai kuruhusiwa kwa mikutano ya ndani hakujatokana na msukumo wowote kutoka nje ya jeshi hilo, isipokuwa kuridhisha kwa jeshi hilo kuhusu hali ya kiusalama hasa katika shughuli za kisiasa nchini.

“Tulipozuia mikutano hiyo ya ndani awali, ni baada ya kubaini baadhi ya vyama vinatumia mikutano hiyo ya ndani kuelezea ajenda za kuchochea wananchi wasitii sheria za nchi, kupandikiza chuki na kuhatarisha hali ya usalama,” alisema Mssanzya.

Alisema wakati mikutano hiyo ya ndani ikiendelea, vyama ambavyo vitajadili ajenda zisizohusu chama husika pamoja na kuchochea kuvunja sheria za nchi, vitachukuliwa hatua za kisheria.

“Waliokiuka zuio la awali na kufanya mikutano hiyo, walikamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria, Jeshi la Polisi tulifanya uchunguzi na kukabidhi mahali husika, hatua gani zilichukuliwa zinakihusu chombo (husika), sisi tulishafanya kwa upande wetu,” alisema.

Alisema zuio la kufanyika kwa maandamano na mikutano ya hadhara limebaki palepale, isipokuwa kwa mikutano inayofanyika katika majimbo ikiongozwa na wabunge hadi pale jeshi hilo litakapofanya tathmini pana zaidi ya hali ya usalama nchini.
Kamishna Mssanzya aliwataka wananchi pamoja na vyama vyote vya siasa nchini vitoe ushirikiano kwa jeshi hilo kwa kuheshimu sheria za nchi na kushirikiana na jeshi hilo kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unaimarika.

Agosti 24, Jeshi la Polisi lilipiga marufuku vyama vya siasa kufanya mikutano ya ndani ikiwa ni takribani miezi miwili baada ya Rais John Magufuli kutangaza kupiga marufuku maandamano na mikutano yote ya kisiasa hadi mwaka 2020.
Juni 23, Rais alipiga marufuku shughuli za kisiasa hadi mwaka 2020 na kusema wabunge na madiwani ndiyo wanaopaswa kufanya mikutano na shughuli nyingine za kisiasa, lakini kwenye maeneo yao walikopigiwa kura na si kwingineko.

CCM WALONGA
Msemaji wa CCM, Christopher Ole-Sendeka, alipotafutwa na Nipashe kuzungumzia suala hilo, alipongeza uamuzi uliofanywa na Jeshi la Polisi akiamini utavisaidia vyama vya siasa nchini kujijenga zaidi.

"Polisi wamefikia hatua hiyo baada ya kujiridhisha kwamba hali ya usalama nchini ni nzuri. Awali mikutano ilikuwa kama jukwaa la kuandaa maandamano," alisema.

KAULI YA UPINZANI
Wakati CCM wakieleza kufurahishwa na uamuzi huo, Mwenyekiti Mwenza wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), James Mbatia, alisema hawajaupokea kwa furaha.
"Polisi hawana mamlaka ya kupinga kufanyika kwa mikutano ya ndani ya vyama vya siasa," alidai Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR - Mageuzi.

Habari Kubwa