Maandamano ya CUF yapigwa `stop'

27Jan 2017
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
Maandamano ya CUF yapigwa `stop'

POLISI visiwani humu wamepiga marufuku maandamano ya Chama cha Wananchi (CUF) kuwakumbuka wanachama wake waliokufa na kujeruhiwa katika msuguano wa kisiasa uliotokea Januari 26/27, mwaka 2001.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mwembe Madema visiwani humu, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Hassan Nassir, alisema Jeshi la Polisi litaimarisha ulinzi katika maeneo yake yote ya mkoa kuhakikisha jambo hilo halifanyiki.

Alisema matembezi hayo yalikuwa yameandaliwa na Umoja wa Vijana wa CUF (JuviCuf) na yalikuwa yaanzie katika Ofisi zao za Mwembetanga na kumalizikia Ofisi za Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) katika Mtaa wa Kinazini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

"Marufuku kukusanyika vikundi katika maeneo tofauti vinavyoashiria kuwapo kwa matembezi ya jumuiya hiyo," alisisitiza Kamanda Nassir.

Aidha, aliwataka wananchi watulie na kuendelea na shughuli zao za kimaisha, lakini hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayeshiriki kwa namna moja ama nyingine katika matembezi hayo.

Maadhimisho ya kuwakumbuka watu waliopoteza maisha na kupata ulemavu yalikuwa yakifanyika Januari 26/27 kila mwaka, lakini yalisita baada ya kupatikana maridhiano na kuzaliwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na viongozi wa CUF kuwa sehemu ya viongozi wa Serikali ya Zanzibar.

Hata hivyo, Serikali ya Umoja wa Kitaifa imekwama kuundwa baada ya CUF kususia uchaguzi wa marudio na kupoteza viti vyote vya uwakilishi na udiwani wakipinga kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka juzi.

Habari Kubwa