Mabadiliko ya tabianchi yalivyoathiri upatikanaji huduma ya maji,...

24Nov 2022
Gwamaka Alipipi
Aliyekuwa CHEMBA
Nipashe
Mabadiliko ya tabianchi yalivyoathiri upatikanaji huduma ya maji,...
  • *Kisima cha msikiti chaokoa wananchi na mifugo
  • *Wakulima wakimbia mashamba, wahamia dukani

NI mwendo wa takribani dakika 10 kwa kutumia usafiri wa pikipiki kutoka mjini Chemba kukifikia Kijiji cha Paranga kilichoko Kata ya Paranga, Halmashauri ya Chemba mkoani Dodoma.

Wafugaji wa kata ya Paranga, wilayani Chemba, mkoani Dodoma, wakinywesha maji mifugo huku wananchi wakiwa wamepanga foleni wakisubiri kuchota maji hayo, mapema wiki hii. PICHA: GWAMAKA ALIPIPI.

Kwa muda wote wa safari hiyo fupi kutoka mjini, kinachoshuhudiwa ni nyasi zilizokauka, miti iliyopukutisha majani na ardhi iliyopasuka huku kukiwa na kadhia nyingine ya watoto wanaoswaga punda, wanaovuta mikokoteni iliyosheheni madumu ya maji.

 

Nipashe inapozungumza na wenyeji, mara moja inabaini kwamba kinachojiri dhidi yao ni matokeo ya athari za mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira, shida zilizoyakumba maeneo mengi nchini.

 

Katika udadisi wake kuhusu undani wa madhila hayo kwa wananchi, Nipashe pia inashuhudia mkusanyiko wa wananchi walioweka foleni ya kuchota maji, huku mifugo nayo ikinyeshwa maji hayo hayo yanayotolewa na msikiti unaoitwa Masjidi Nuru Paranga.

 

Ikirejewa mipango na mikakati ya kitaifa, kinachoshuhudiwa Chemba kinakinzana na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Juni 1999-2025, inayoelekeza serikali kuhakikisha inapunguza walau nusu ya watu wanaoishi katika umaskini na kuwafanya waishi katika uchumi wa kati kufikia mwaka 2025.

 

Pia ni hali iliyo kinyume cha Sera ya Maji inayotumika kwa sasa nchini, ikiitaka serikali kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya majisafi ndani ya mita 400 kutoka kwenye makazi yao.

 

Logo Tuji, mfugaji kutoka Kijiji cha Paranga mwenye mifugo zaidi ya 80 aliyekutwa eneo hilo la kisima cha msikiti akiwa na mifugo yake, anasema: “Hali ni mbaya sana. Isingekuwa msikiti huu, sijui tungenywesha nini mifugo yetu. Kama unavyotuona hapa, tunaweka foleni kupata huduma, jua linawaka sana, hakuna mvua."

 

Shakira Ramadhani, mama wa watoto wanne na mkazi wa Kata ya Paranga, ambaye alikutwa na Nipashe kisimani huko, akisubiri mifugo imalize kunywa ndipo achote maji, anasema analazimika kuweka foleni na mifugo kwa sababu hakuna sehemu nyingine anayoweza kupata maji kwa ajili ya matumizi ya familia yake.

 

“Ukitaka kuyafuata maji inakupasa uamke alfajiri sana, utembee umbali wa kilometa 10. Ukirudi unachoka sana na majukumu mengine ya familia yanakusubiri, hivyo kuepukana na adha hiyo tunalazimika kuweka foleni na mifugo,” anasema Shakira.

 

Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Kuruthumu Skana anasema uhaba wa mvua umemwathiri kiuchumi kwa kuwa ameshindwa kuzalisha chakula kwa ajili ya familia yake.

 

Anasema hali hiyo imemlazimu ajishughulishe na upondaji wa kokoto, mwenyewe akizipa jina la 'karasha'. Pia anasema amelazimika kufanya vibarua sehemu mbalimbali ili kupata fedha kwa ajili ya kulisha familia katika kipindi hiki cha ukame.

 

"Mimi ni mkulima wa mahindi na alizeti, mwaka huu sijaambulia chochote. Nilipanda Januari mwishoni lakini mazao yameishia katikati. Maji nayo hakuna, ukiagiza dumu la lita 20 gharama yake ni Sh. 250. Ni gharama kubwa sana huku kwetu maana maisha yetu kama unavyoona ya kuungaunga," Kuruthumu analalama.

 

Mkazi mwingine Maria Loyababu anaendelea kusimulia kinachowasibu kipindi hiki, akitamka: "Upatikanaji wa chakula na maji ni wa tabu sana mwaka huu, jua linawaka sana, ukame umeongezeka, huwa ninalima ekari moja ya mahindi lakini yamekauka.

"Nina watoto saba. Ninaiomba serikali itupatie msaada wa chakula au kutuuzia kwa bei nafuu zaidi ili hata sisi tuliomo kwenye TASAF (Mpango wa Maendeleo) tumudu kukinunua".

 

Mkuu wa kaya hiyo, Damian Kolo anasema ugumu wa kupata maji na chakula unamkwamisha kufanya shughuli zingine za maendeleo.

 

"Kwa sasa tunatumia muda mwingi kusaka maji badala ya kujikita kwenye shughuli zingine za maendeleo. Tunafikia hatua ya kutooga hata kwa siku mbili hadi tatu maana upatikanaji wa maji ni mgumu," anafafanua.

 

Mmoja wa wakulima wa kijiji hicho, Walfa Salum anasema amelazimika kuachana na kilimo na kufungua duka la bidhaa za matumizi ya nyumbani baada ya kulima msimu uliopita na kuambulia patupu kwenye mavuno.

 

“Sasa nimeamia dukani, kilimo kimekataa kabisa, hakuna mvua wala maji ya kumwagilia mazao. Mwaka mwaka jana sijapata hata debe la mahindi, yote yamepotelea shambani, nilipanda ekari mbili lakini yamepotelea shambani," anasema Walfa, mama wa watoto sita.

 

Moshi Ali, mkulima wa mpunga, anasema ukame wa mwaka huu umesababisha kutopata hata debe la mpunga.

 

"Uhaba wa mvua ni tatizo, maji ya RUWASA (Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini) nayo ni tatizo, njaa inatunyemelea. Wakulima hatujavuna kitu msimu uliopita, mwaka huu kama unavyoona jua linawaka, mvua tulitarajia inyeshe kuanzia mwanzoni mwa Novemba lakini hadi leo (Novemba 12, mwaka huu) hakuna kitu, uzalishaji wa chakula umepungua," anasema.

 

Diwani wa Makorongo, Petro Mollel anakiri kuwapo tatizo la uhaba wa maji na chakula katika eneo lake la utawala lililosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.

Anaiomba serikali kufanya alichokiita kuiangalia kwa jicho la tatu hali hiyo kwa kuwa wananchi wengi katika kata yake wameshindwa kuvuna mazao kutokana na uhaba wa mvua.

Anataja hatua anazoona zinatakiwa kuchukuliwa na serikali kipindi hiki ni pamoja kuwapelekea maji wananchi kutoka vyanzo vingine vya maji na kuwapatia chakula cha bei nafuu, hatua ambazo serikali imezichukua katika maeneo mengi yaliyoathiriwa na ukame, zikiwamo Halmashauri za Longido na Monduli mkoani Arusha.

*ITAENDELEA KESHO

Habari Kubwa