Mabadiliko ya uongozi hospitali za rufani yaja

02Mar 2021
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe
Mabadiliko ya uongozi hospitali za rufani yaja

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, ameagiza kufanyike kwa mabadiliko ya uongozi wa timu za uendeshaji wa hospitali zote 28 za rufani za mikoa kulingana na nafasi ya kila kiongozi alivyoshiriki kusababisha hasara kuanzia kwa mganga mfawidhi wa hospitali.

Waziri aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari, na kueleza kuwa amekuwa akipokea malalamiko mengi toka kwa wananchi kuhusu kukosekana kwa dawa na vipimo katika vituo vya kutolea huduma za afya katika ngazi zote kinyume cha matarajio.

Alisema ili ukweli ujulikane na haki itendeke, wizara iliunda kamati ya wataalamu kutoka wizara na taasisi za sekta mbalimbali ili kufuatilia hospitali za rufani 28 za mikoa kwa kipindi cha miezi 18 kuanzia Julai 2019 hadi Desemba 2020.

“Lengo lilikuwa ni kubaini changamoto zinazochangia upatikanaji duni wa dawa na vipimo licha ya kuongezeka kwa mtaji wa dawa,” alisema.

Waziri alisema jumla ya bidhaa za dawa na vipimo 25-30 kati ya nyingi zilizopo kwenye orodha ya bidhaa za afya kwa kituo husika zilifanyiwa ufuatiliaji kuanzia ununuzi, mapokezi na matumizi.

Alisema amepokea taarifa ambayo imethibitisha uwapo wa uzembe na kutojali katika usimamizi wa mfumo wa ugavi wa bidhaa za afya, viashiria vya hujuma, wizi na udokozi wa bidhaa hizi.

Alisema upungufu huo unachangiwa na utendaji wa mazoea wa baadhi ya viongozi wasio waadilifu na wasiowajibika katika kusimamia rasilimali kuanzia ngazi ya taifa, mkoa, Halmashauri pamoja na watumishi mmoja mmoja katika maeneo yao ya kazi.

“Jumla ya thamani ya fedha ambazo imethaminishwa kwa mapungufu haya inakadiriwa kuwa siyo chini ya Sh. bilioni 26.7 kwa kipindi hiki kifupi kwa bidhaa hizo chache.

Alisema kwa mujibu wa matokeo ni dhahiri kuwa na usimamizi dhaifu wa mifumo ya udhibiti wa mali ya umma, dalili za hujuma, wizi na uwajibikaji usiofaa wa bidhaa ya viongozi katika ngazi zote za uongozi hadi kwa mtumishi mmoja mmoja.

“Sababu hizi ni mojawapo ya mambo yanayosababisha kukosekana kwa bidhaa za afya au kutotosha na mtaji kudidimia. Kufuatia hali hii Februari 28, mwaka huu, niliitisha kikao na waganga wakuu wa mikoa yote, waganga wafadhili wa hospitali zote za rufani za mikoa pamoja na menejementi ya wizara wakiwamo wawakilishi kutoka Ofisi ya Rais (TAMISEMI) niliwaeleza matokeo ya taarifa ya ufuatiliaji uliofanyika,” alisema.

Alisema baada ya kuwaeleza aliwasikiliza na wengi wao walikiri upungufu uliobainishwa na kamati.

Waziri alisema kutokana na hali hiyo amemwagiza Katibu Mkuu wa afya kuchukua hatua za nidhamu kwa kila mtumishi ama mtu yeyote aliyekwenda kinyume na sheria, kanuni na taratibu za ununuzi na ugavi wa bidhaa za afya.

“Aunde kamati kwa kushirikiana na ofisi ya Rais ya TAMISEMI kufanya mapitio ya mikataba ya washiriki wa bidhaa za afya nchi nzima na kushauri ipasavyo juu ya hatua stahiki za kuchukua,” alisema.

Waziri alisema kuratibu zoezi la maboresho ya miongozo ya ushiriki na ofisi ya TAMISEMI na makatibu tawala wa mikoa kwenye kuimarisha ufuatiliaji na uangalizi wa uendeshaji wa hospitali hizo.

Aidha, ameagiza ndani ya siku 14 kuanzia jana Katibu Mkuu kumpatia taarifa ya utekelezaji inayojibu masuala yote yaliyoibuliwa kwa kuwa yametokea wakati halmashauri na mikoa wapo waganga wakuu wa halmashauri na mikoa husika wanaowakilisha wizara katika kusimamia huduma za afya.

“Vilevile hapa wizarani wapo wataalamu wabobezi ikiwamo kurugenzi zinazohusika na usimamizi na ufuatiliaji wa uendeshaji wa hospitali hizo hususani idara ya tiba na huduma za uchunguzi pamoja na idara ya mfamasia mkuu wa serikali,” alisema.

Waziri ameagiza yafanyike mapitio ya ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya bodi zote za ushauri wa hospitali za mikoa na kubaini kwa nini zimeshindwa kutimiza wajibu wao wa kumshauri sambamba na majukumu yao kwa mujibu wa tangazo la serikali namba 308 la mwaka 2014.

Habari Kubwa