Mabalozi nchi za Kifaransa wakutana Dar

19Mar 2019
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Mabalozi nchi za Kifaransa wakutana Dar

MABALOZI wanaowakilisha nchi 14 nchini zinazozungumza Kifaransa duniani, wamekutana jijini Dar es Salaam kujadili mchango wa lugha hiyo katika maendeleo ya kiuchumi na kiutamaduni.

Balozi wa Uswisi nchini, Florence Tinguely, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kuhusu wiki ya kuadhimisha lugha na utamaduni wa Kifaransa katika nchi zinazoongea lugha hiyo, ambapo imehusisha balozi 13 wanao ziwakilisha nchi zao hapa nchini. Wengine kutoka kushoto ni Balozi wa Ubelgiji, Peter Van Acker, Balozi wa Ufaransa, Frédéric Clavier na Balozi wa Morocco, Abid Benryane. PICHA: HALIMA KAMBI

Wakizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, mabalozi hao walisema kuanzia jana ilikuwa maadhimisho ya Wiki ya Lugha ya Kifaransa ambayo yatakwenda sambamba na shughuli mbalimbali za kimaendeleo ikiwamo michezo.
 
Kiongozi wa Mabalozi hao, Abid Benryane, kutoka Morocco, alisema katika maadhimisho hayo kutakuwa na maonyesho ya picha, video, programu maalum, michezo mbalimbali ya kuonyesha namna gani lugha inaweza kuwaunganisha watu na kutumika kuleta maendeleo.
 
Alisema lugha ya Kifaransa ni ya tano duniani kwa kuzungumzwa na kwa sasa ina zaidi ya wazungumzaji milioni 300 duniani kote na ifikapo mwaka 2050 wanatarajiwa kufikia milioni 700.
 
Alisema lugha hiyo ni rasmi kwa nchi 32 na mashirika ya kimataifa kama Umoja wa Mataifa (UN), Nato, Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) na Umoja wa Afrika (AU).
 
“Ni lugha ya kufundishia na kujifunzia kwa zaidi ya watu milioni 80 katika nchi 36 na lugha ya nne kwenye mtandao na biashara. Asilimia 59 ya wazungumzaji wa lugha hii wanaishi Afrika na inatarajiwa watafikia asilimia 80 mwaka 2050,” alisema na kuongeza:
 
“Mwaka 2018 nchi zinazozungumza Kifaransa zilichangia asilimia 8.4 ya pato la taifa duniani na kwamba lugha hiyo inafungua milango ya ajira kwenye biashara  hasa kwa Afrika  na ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema.
 
Naye Balozi wa Ufaransa nchini, Frederic Clavier, alisema kwa Tanzania, Kifaransa kinazungumzwa na zaidi ya watu milioni 1.5 na kinatumika kwenye shule mbalimbali, hivyo kuongeza idadi ya Watanzania wanaojua lugha hiyo.
 
“Tanzania imepakana na nchi nne wanachama wa nchi zinazozungumza Kifaransa ambazo ni Rwanda, Burundi, Congo na Msumbuji. Mkoa wa Kigoma asilimia sita ya wakazi wake ni kutoka nchi hizo na kwa wastani wa nchi ni asilimia mbili,” alisema na kuongeza:
 
“Kupitia Bahari ya Hindi, Tanzania inaunganishwa na Madagascar, Mauritius, Shelisheli na Comoro. Pia zipo fursa mbalimbali za Watanzania wa aina zote kujifunza lugha na kuitumia kwa maendeleo ya kiuchumi kwa kuwa kwa kutumia intaneti wamejifunza na kusoma mambo mbalimbali ikiwamo kupata fursa za ndani na nje.”
 
Kwa upande wake, Balozi wa Uswisi nchini, Florence Mattli, alisema katika maadhimisho hayo, mambo yatakayojadiliwa ni uhuru wa kujieleza, elimu, haki za binadamu, maendeleo ya haki za kiuchumi, teknolojia ya mawasiliano na ubunifu.
 
Naye Rais wa walimu wanaofundisha Kifaransa Dar es Salaam (Dafta), Patrick Shole, alisema kupitia umoja huo wameongeza idadi ya wanaojua lugha hiyo na inatumika kwa wanafunzi wa shule za msingi hadi sekondari.
 

Habari Kubwa