Mabasi mtegoni usafirishaji vipeto

11Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Mabasi mtegoni usafirishaji vipeto

MABASI ya abiria yanayofanya safari za mikoani, yamepigwa marufuku kubeba vifurushi bila kuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Onyo hilo lilitolewa juzi na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, alipokuwa akifungua Baraza la Wafanyakazi wa Shirika la Posta (TPC) jijini Dodoma.

Kutokana na kuwapo kwa mabasi hayo yanayobeba mizigo bila leseni, Nditiye aliiagiza TCRA kuanza msako mara moja kuyabaini yanayokiuka sheria hiyo na kuyachukulia hatua.

Nditiye alisema kwa mujibu wa Sheria ya TCRA, hakuna chombo chochote cha usafiri kinachoruhusiwa kubeba vipeto bila kuwa na leseni kutoka mamlaka hiyo na yeyote atakayekwenda kunyune atachukuliwa hatua za kisheria.

“Kwa muda mrefu baadhi ya mabasi ya kwenda mikoani yamekuwa yakisafirisha mizigo, barua, vipeto na hata vyeti mbalimbali bila kufuata sheria na taratibu. Sasa hii ni lazima ifike mwisho.

“Kuanzia sasa nimeiagiza TCRA kuanza kufanya msako dhidi ya basi moja hadi lingine. Ni lazima sheria zinazohusu uchukuzi zifuatwe na kuheshimiwa na niwajulishe wananchi kwamba usafirishaji wa vipeto na hata barua unafanywa na kampuni zilizosajiliwa na kupewa leseni na mamlaka ya mawasiliano,” alisema.

Katika kutekeleza hilo, Naibu Waziri aliiagiza TCRA kufanya ukaguzi kwenye vituo wakati mabasi yanapoanza safari na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria kama ambavyo Mamlaka ya Usafiri wa Ardhini (Latra) inavyofanya.

Usafirishaji wa vipeto na bahasha ndani na nje ya nchi hufanywa na kampuni zilizosajiliwa kisheria na kupewa leseni na Mamlaka ya Wawasiliano nchini.

Miongoni mwa kampuni hizo ni TPC kupitia kampuni yake tanzu ya Expedited Mail Services (EMS), CDS Couriers, DHL Global Forwarding, SkyNet Worldwide Express, Zip N Zap Courier, TNT Express, MSS Logistics and Courier na Aramex Tanzania Limited.

Habari Kubwa