Mabilioni yamwagwa kwa vikundi vya watu wenye walemavu

03Dec 2021
Marco Maduhu
DODOMA
Nipashe
Mabilioni yamwagwa kwa vikundi vya watu wenye walemavu

AFISA ustawi wa jamii mwandamizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu Joyce Maongezi, amesema Serikali imekuwa ikitoa fedha za mikopo asilimia mbili za Halmashauri  kwa walemavu ili kuwainua kiuchumi.

Afisa ustawi Mwandamizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu- Walemavu Joyce Maongezi akizungumza wakati wa kufunga Kongamano la maadhimisho siku ya watu wenye ulemavu duniani Jijini Dodoma.

Maongezi amebainisha hayo leo wakati akifunga Kongamano la kuadhimisha siku ya watu wenye ulemavu duniani Jijini Dodoma, ambalo limekutanisha waandishi wa habari, wahariri, watu wenye ulemavu, na Taasisi zinazotetea watu wenye ulemavu, lililoandaliwa na Shirika la Internews Tanzania.

Amesema katika mwaka wa fedha (2018-19) Serikali ilitoa kiasi cha fedha Sh.bilioni 3.4 kwa vikundi vya watu wenye ulemavu 873, ambapo jumla ya watu wenye ulemavu 7,035 walinufaika na fedha za mkopo huo.

Aidha, amesema katika mwaka wa fedha (2019-20) walitoa kiasi cha Sh.bilioni 4.8 kwa vikundi 1,033 vya watu wenye ulemavu, ambapo jumla ya watu wenye ulemavu 8,347 walinufaika na mikopo hiyo.

"Serikali tutaendelea kutoa fedha za mikopo kwa watu wenye ulemavu, kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri hapa nchini asilimia mbili,ili kuwainua kiuchumi kwa kuendesha maisha yao" amesema Maongezi.

Kwa upande wake Mratibu wa mafunzo kutoka Shirika la Internews, Shabani Maganga ,amesema wameendesha Kongamano hilo, ili kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu watu wenye ulemavu ndani ya jamii, na kuona namna ya kuzitafutia ufumbuzi changamoto ambazo zinawakabili katika nyanja mbalimbali.

Habari Kubwa