Mabilioni ya NSSF yalivyopotea

08Apr 2021
Salome Kitomari
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mabilioni ya NSSF yalivyopotea

RIPOTI ya CAG imeonyesha kuwa kampuni tanzu ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), limetengenza hasara ya zaidi ya Sh. Bilioni 4.72 kwa mwaka 2019/20 kupitia uwekezaji uliofanyika katika viwanda vya kuzalisha Sukari vya Mbigiri na Mkulazi.

Charles Kichere, Mdhibiti mpya na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Aidha, NSSF imeshindwa kukusanya kiasi cha Sh. Bilioni 28.8 ambazo zilitolewa kama mikopo kwenye Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS), vipatavyo 134 hadi kufikia Juni 30,2020.

“Nilibaini kuwa, vyama 14 vilivyokopeshwa Sh. bilioni 14 havifanyi marejesho ya mikopo. Hali hii inasababisha hasara kwa NSSF na ukosefu wa fedha za kugharamia kazi zingine,”

Katika ukaguzi wa ufanisi juu ya utekelezaji wa mradi wa uzalishaji wa Sukari Mbigiri walibaini kuwa mbolea na dawa za kuulia wadudu zenye thamani ya Sh. 241,889,000 zilitolewa ghalani ila hapakuwa na maelezo ya namna ambavyo mbolea hii ilitumika.

Amesema miwa iliyopita muda wake wa mavuno ilionekana katika vitalu mbalimbali kwenye  shamba la Mbigiri ikiwa imeharibika na kupoteza thamani yake ya kiuchumi.

Pia, makisio ya hasara iliyotokana na gharama za uzalishaji wa miwa hiyo ni kiasi cha Sh. 379,338,245.

CAG alibainisha kuwa visima vinne katika shamba la Mbigiri kitalu E3, D2, E4 na F4 vilichimbwa lakini havitumiki kwa sababu havina uwezo wa kutoa maji ya kutosha kwa shughuli za umwagiliaji.

“Pia, nilibaini kuwa mkandarasi aliondoka eneo la kazi licha ya kuwa alishalipwa Sh. 81,500,000 sawa na asilimia kumi ya gharama zilizoainishwa kwenye mkataba,”alisema.

Kampuni ya Mkulazi ilishindwa kusimika mtambo wa kuchakata sukari kwa wakati na kusababisha benki ya Azania kusitisha kutoa mikopo kwa wakulima wa nje kiasi cha Sh. 1,797,050,000 ambazo zingewawezesha wakulima hao kukidhi gharama mbalimbali za kuzalisha miwa.

Habari Kubwa