Mabilioni yaokolewa matibabu ya figo nje

15Mar 2019
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Mabilioni yaokolewa matibabu ya figo nje

SERIKALI imesema imeokoa Sh. bilioni 3.4 ambazo zingetumika kugharamia matibabu ya wagonjwa wa figo 42 nje ya nchi tangu ianze kutoa matibabu hayo nchini.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, picha mtandao

Vilevile, imesema matumizi ya dawa za kutuliza maumivu mara kwa mara, ni miongoni mwa vitu vinavyochangia uharibifu wa figo.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, aliyasema hayo jijini Dodoma jana alipozungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Figo Duniani.

Alisema hadi sasa, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam na Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma, wagonjwa waliopandikizwa figo ni 42.
"Kati yao, 38 wamepatiwa huduma Hospitali ya Taifa Muhimbili na wanne Hospitali ya Benjamin Mkapa," alisema.

Alisema kuwa kama wangepelekwa nje ya nchi, ingeigharimu serikali Sh. bilioni 4.2 wakati huduma hiyo nchini inagharimu kiasi cha Sh. milioni 21 kwa kila mgonjwa, hivyo ingekuwa Sh. milioni 882, hivyo kiasi kilichookolewa ni Sh. bilioni 3.4.

Alisema upatikanaji wa huduma za upandikizaji figo nchini umepunguza gharama kubwa ambazo serikali ilikuwa inalipa kupeleka wagonjwa nje ya nchi.

“Huduma zimesogezwa kwa watu wengi zaidi tofauti na hapo awali," Dk. Ndungulile alisema na kuongeza kuwa Watanzania wengi wamekuwa wakitumia dawa kiholela bila ya kupima na kufuata ushauri wa daktari hususani dawa aina ya Diclofenac na za asili ambazo hazijathibitishwa.

“Unakuta mtu anaumwa kichwa, amechoka ametembea siku nzima anaenda kununua dawa za kutuliza maumivu, anameza na maumivu yanatulia, wakati alitakiwa kupumzika na kunywa maji mengi," alisema.

Kiongozi huyo wa serikali alisema wagojwa wa figo wanazidi kuongezeka nchini, akiwataka wananchi kujiwekea utaratibu wa kupima afya zao mara kwa mara na kuepuka matumizi ya dawa za kutuliza maumivu kiholela.

Alitaja visababishi vingine vya magonjwa ya figo kuwa ni pamoja na kutofanya mazoezi, uzito wa kupindukia, matumizi makubwa ya sigara na unywaji wa pombe.

Alisema takwimu zinaonyesha duniani kote, inakadiriwa watu milioni 850 wanasumbuliwa na magonjwa ya figo na kila mwaka, watu milioni 2.4 hufariki dunia kutokana na magonjwa hayo.

“Magonjwa ya figo yanashika nafasi ya sita miongoni mwa magonjwa yanayochangia idadi kubwa ya vifo duniani, Bara la Afrika hasa kusini mwa Jangwa la Sahara ni sehemu yenye wagonjwa wengi wa matatizo ya figo," alisema.

Dk. Ndungulile alisema magonjwa ya figo yamekuwa yakiongezeka barani Afrika kufikia wastani wa saba hadi 25 na utafiti uliofanyika kaskazini mashariki mwa Tanzania katika ngazi ya kaya mwaka 2014, ulionyesha ugonjwa sugu wa figo unaathiri asilimia saba ya Watanzania.

“Katika utafiti huo, ilionekana kwamba uelewa mdogo kuhusu magonjwa ya figo unachangia kwa kiasi kikubwa kupata ugonjwa sugu wa figo na idadi ya wagonjwa hawa imekuwa ikiongezeka kwa kasi kubwa ikiashiria ukubwa wa tatizo hili nchini," alisema.

Alisema wizara imefanikiwa kuhakikisha kunakuwa na dawa na huduma bora za usafishaji damu kwa wagonjwa wa figo, akibainisha kuwa hadi kufikia Desemba mwaka jana, kulikuwa na wagonjwa 1,050.

Alisema magonjwa ya kisukari na shinikizo la damu ni magonjwa yanayoongoza kwa kusababisha matatizo ya figo.

Dk. Ndugulile alisema serikali imedhamiria kuweka mashine za kusafisha figo (Hemodialysis) katika hospitali za rufaa za mikoa yote 28 ya Tanzania Bara.

Habari Kubwa