Mabula alia kuchelewa fedha miradi NHC Chato

15Sep 2021
Munir Shemweta
Chato
Nipashe
Mabula alia kuchelewa fedha miradi NHC Chato

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula, amekagua miradi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Chato mkoani Geita na kusikitishwa na kusuasua kwa utekelezaji wake kunakosababishwa na ucheleweshaji wa fedha.

Dk. Mabula alikagua miradi mitatu inayotekelezwa na NHC ambayo ni mradi wa mnada wa mifugo Buzirayombo wenye thamani ya Sh. bilioni 4.8, ujenzi wa shule maalum ya Mbuye wenye thamani ya Sh. bilioni 5.14 pamoja na mradi wa nyumba 20 za watumishi wa Hospitali ya Rufani ya Kanda - Chato wa thamani ya Sh. bilioni 1.139.

 

Akizungumza baada ya kukagua miradi yote mitatu jana, akiwa katika ziara ya siku mbili mkoani Geita, Dk. Mabula alisema miradi hiyo ni muhimu na inapaswa kukamilika kwa wakati ili ianze kutumika.

 

"Haitakuwa na maana serikali kuwekeza fedha nyingi kwenye miradi ya mnada wa mifugo, shule maalum na nyumba za watumishi wa sekta ya afya na kuachwa bila kukamilika jambo ambalo halitaleta maana," alisema.

 

Meneja wa NHC Mkoa wa Kagera, Maneno Mahenge, alimwambia Naibu Waziri kuwa NHC imekuwa likisuasua kutekeleza kwa kasi miradi katika wilaya hiyo kutokana na kutopatiwa fedha za miradi kwa wakati.

 

Alisema shirika hadi sasa limetumia takribani Sh. bilioni 1.02 kwenye mradi wa mnada wa mifugo, Sh. milioni 985 katika Shule Maalum ya Mbuye na Sh. milioni 275 kwa ajili ya utekelezaji mradi wa nyumba za watumishi katika Hospitali ya Rufani ya Kanda na fedha zote hizo bado halijalipwa.

 

Naibu Waziri pale panapokuwa na tatizo lolote katika utekelezaji miradi ya NHC    ni lazima ushirikiano uwapo baina ya mwenye mradi na mkandarasi kwa lengo la kuepuka ucheleweshaji.

 

"Kama taarifa hazifiki kwa wakati basi miradi itasimama na haileti picha nzuri na ukiangalia hapa tatizo kubwa ni mawasiliano na taarifa zikiwapo basi kazi itaenda vizuri," alisema.

 

Dk. Mabula aliahidi kukutana na wenye miradi ili kupaa ufumbuzi na hatimaye ikamilishwe haraka na kuanza kutumika.

 

Katika hatua nyingine,  Naibu Waziri Mabula alisema uhakiki kwa wamiliki wa ardhi nchini hauna lengo la kuwanyang'anya umiliki wa ardhi maeneo yao bali ni kutaka kuwatambua kwa majina.

 

Akizungumza na watumishi wa sekta ya ardhi na viongozi wa wilaya ya Chato, Dk. Mabula alisema kuna baadhi ya viwanja wamiliki wake hawajulikani na uhakiki unaoendelea sasa nchini una lengo la kumtambua na kuainisha kila mmiliki na eneo lake.

 

"Kuna viwanja vimepimwa zamani na wamiliki wake hawaonekani. Tunataka  kujua wamiliki ni kiasi gani na tunahitaji uhakiki kuwatambua Watanzania kupitia utajiri wao kwenye sekta ya ardhi," alisema Dk. Mabula.

Habari Kubwa