Machinga wanavyoweka rehani maisha ya watembea kwa miguu

01Nov 2020
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe Jumapili
Machinga wanavyoweka rehani maisha ya watembea kwa miguu
  • *Kila baada ya sekundi 24, kifo kinarekodiwa

"ELFU tano viatu, elfu kumi mikoba ya kinamama, elfu tatu tu kila utakaposhika..." Sauti za wajasiriamali wadogo, maarufu machinga', zinasikika eneo la Nyerere Square mjini Dodoma wakinadi bidhaa zao kwa wateja.

Ni majira ya jioni, biashara ikiwa imechangamka kwenye eneo hilo lililoko katikati ya Jiji la Dodoma. Barabara kuu ya Nyerere inapita kwenye eneo hilo ikitumiwa na madereva wa mabasi madogo ya abiria, pikipiki na bajaj.

Katika udadisi wake, Nipashe inabaini bidhaa za wajasiriamali hao zinatandazwa juu ya mitaro kupitia maji machafu na zingine pembezoni mwa barabara, maeneo ambayo ni mahususi kwa watembea kwa miguu.

Ufuatiliaji zaidi unabaini kwamba siyo eneo la Nyerere Square tu lililokumbwa na kadhia hiyo, bali maeneo mengi ya katikati ya jiji hilo jipya sasa yamegeuka soko la bidhaa za machinga.

Maeneo hayo mbali na Nyerere Square ni pamoja na Msikiti wa Nunge, maeneo yote ya Barabara za Independence Square na Uhindini na barabara zote za jiji zinazoelekea Soko la Sabasaba.

Shida kuu inayojitokeza kutokana na utaratibu huo mpya wa kufanya biashara, iko kwa watembea kwa miguu ambao njia zao zimevamiwa na machinga, hivyo kulazimika kutumia barabara za magari.

Kinachoshuhudiwa sasa jijini Dodoma nyakati za jioni, ni milio ya honi za magari na pikipiki dhidi ya watembea kwa miguu wanaohatarisha maisha yao kwa kupita kwenye barabara za vyombo hivyo vya moto kutokana na njia za watembea kwa miguu kutandazwa bidhaa za machinga.

KIFO KILA SEKUNDE 24

Wakati hali ikiwa hivyo jijini Ddooma, Ripoti ya Shirika la Afya Dunia (WHO) kuhusu Usalama Barabarani ya Mwaka 2018, inabainisha kuwa watu milioni 1.35 hufariki dunia kila mwaka kutokana na ajali barabarani.

Takwimu hizo za WHO zinamaanisha kwamba kila siku kuna vifo vya watu 3,699, sawa na vifo 154 kila saa na kifo cha mtu mmoja kila baada ya sekunde 24.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa nusu ya vifo hivyo vya ajali za barabarani huwapata watembea kwa miguu na ajali za pikipiki.

Kwa mujibu wa shirika hilo, idadi kubwa ya watu wanaopoteza maisha katika ajali hizo inatoka nchi za kipato cha chini kulinganishwa na nchi zenye kipato cha juu.

Chanzo cha vifo hivyo kinatajwa kuwa ni uzembe wa madereva na watembea kwa miguu pamoja na kukosekana kwa maeneo mahususi kwa watembea kwa miguu na waendesha baiskeli.

Katika uchunguzi wake, Nipashe imebaini kwamba licha ya baadhi ya barabara jijini Dodoma kujengwa zikiwa na njia maalum za watembea kwa miguu, njia hizo hazitumiwi na walengwa, badala yake machinga wanazitumia kupanga bidhaa zao.

Kutokana na hali hiyo watembea kwa miguu jijini wanalazimika kutumia barabara za magari, hivyo kuhatarisha maisha yao hasa ikizingatiwa kwa sasa kuna ongezeko la magari na watu kufuatia serikali kuhamishia shughuli zake Dodoma.

KAULI ZA WANANCHI

Alex Mathias, mkazi wa Chang’ombe jijini, anasema mara kadhaa amenusurika kugongwa na gari kutokana eneo alilopaswa kupita katika Barabara ya Sabasaba kutandazwa bidhaa za wafanyabiashara, hivyo kulazimika kutembea kwenye barabara ya magari.

Mathias anaona kwamba ipo haja kwa uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kusimamia matumizi ya barabara kwa watembea kwa miguu ili kuepuka ajali za barabarani dhidi ya kundi hilo.

Cecilia Pius, mkazi mwingine wa jiji hilo, anashauri uongozi wa jiji kuwajibika katika hilo kwa kuhakikisha utenga maeneo maalum ambayo machinga watapanga watatandaza bidhaa zao badala ya kuzigeuzi soko njia za watembea kwa miguu.

USHUHUDA WA MADEREVA

Zynabu Masoudi, dereva wa basi dogo la abiria jijini, anasema uzoefu wake wa miaka 12 katika kazi hiyo unampa jawabu la sababu kuu ya vifo vingi vya ajali za barabarani iko kwa watumiaji wenyewe wa barabara.

"Kwa mfano, umeingia Barabara ya Nyerere pale Nyerere Square, kwanza unalazimika kwenda mwendo mdogo lakini pia honi haziishi maana pembeni wanakotakiwa kupita watembea kwa miguu, kumepangwa bidhaa, watembea kwa miguu wanaingia kwenye barabara za magari, Hapo tayari kunakuwa na shida," analalama.

Dereva huyo pia anashauri barabara za watembea kwa miguu kutambuliwa na kuwe na katazo kwa wafanyabiashara kuweka bidhaa zao kwenye maeneo hayo ili kudhibiti vifo vitokanavyo na ajali za barabarani.

"Ninafikiri Jiji watunge sheria ndogo ili kulinda barabara za watembea kwa miguu, hizi ni muhimu maana maeneo hayo pia wengine wanatumia kufanya mazoezi ili kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza," anashauri.

'TATIZO NI VITAMBULISHO'

Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara wa Soko la Sabasaba, Emmanuel Mtenga, anasema baadhi ya wafanyabishara wamekuwa wanatandaza bidhaa zao kwenye maeneo yasiyo rasmi kwa kisingizio cha kuwa na vitambulisho vya ujasiriamali vinavyotolewa na serikali.

Anasema watahakikisha wanatoa elimu kuhusu usalama barabarani na kuwahamasisha wafanyabishara kuheshimu maeneo yasiyo rasmi kwa shughuli zao za biashara.

“Ni kweli baadhi yetu tuna vitambulisho lakini tunavitumia kinyume cha kanuni na sheria zilizopo ndani ya Halmashauri ya Jiji, wengine wanafanya biashara kwenye maeneo hatarishi," anabainisha.

Victor Sijila, mfanyabiashara wa Sabasaba jijini, anasema kuwa na vitambulisho vya machinga kusiwe sababu ya kukiuka sheria na kanuni zilizowekwa na halmashauri kwa kufanya biashara holela bila mpangilio.

“Kuna wafanyabiashara wamepanga bidhaa zao kwenye maeneo hatarishi na hakuna sababu ya kukaidi kuondolewa kwenye maeneo haya ambayo siyo rasmi kwao kufanyia biashara,” anasema..........kwa habari fuatilia epaper.ippmedia.com

Habari Kubwa