Machinjio yaliyogharimu mil. 980/-  hayatumiki

26Apr 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Machinjio yaliyogharimu mil. 980/-  hayatumiki

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad, amebaini kutokutumika kwa machinjio ya Nyakato jijini Mwanza licha ya mradi huo kukamilika, ukigharimu Sh. milioni 980.989.

Katika ripoti yake ya ukaguzi wa mwaka wa fedha 2017/18, Prof. Assad anabainisha kuwa mradi huo ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kupunguza uchafuzi wa Ziwa Viktoria unaotokana na majitaka.Anabainisha kuwa Mradi wa Maji Safi na Majitaka Awamu ya II ulitiwa saini kupitia mkataba namba ME-011/2015-16/W/05 wa jumla ya Sh. 980,988,900 kwa ajili ya ukarabati wa machinjio ya Nyakato jijini Mwanza kuanzia Julai 22, 2016 hadi Novemba 24, 2017.Katika ripoti yake hiyo, Prof. Assad anabainisha kuwa Halmashauri ya Jiji la Mwanza na watekelezaji wa mradi huo, walitia saini mkataba wa makubaliano kwamba baada ya kukamilika kwa machinjio, Halmashauri ya Jiji la Mwanza itaweka mashine za kuchinjia ili machinjio yatumike.“Timu yangu ya ukaguzi ilifanya ziara tarehe 24 Desemba 2018 na kubaini kwamba machinjio yamekamilika na kukabidhiwa Halmashauri ya Jiji la Mwanza tarehe 15 Agosti, 2018 kwa barua yenye kumbukumbu Namba. LVEMPII/CWMCAIB/VOL.I/73, lakini machinjio hayo hayajaanza kutumika,” CAG Assad anabainisha katika ripoti hiyo.Anaongeza kuwa Halmashauri ya Jiji la Mwanza haijafunga mashine za kuchinjia, jenereta la kutumia gesi na vifaa vingine muhimu vya umeme na pia eneo la machinjio hayo halijawekwa uzio kwa ajili ya usalama.

Habari Kubwa