Macho na masikio ya wafanyakazi wa umma na sekta binafsi kesho

30Apr 2022
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Macho na masikio ya wafanyakazi wa umma na sekta binafsi kesho

MACHO na masikio ya wafanyakazi wa umma na sekta binafsi yataelekezwa kesho kwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni Mgeni rasmi sherehe za Mei Mosi mwaka 2022 huku baadhi ya wafanyakazi wakiwa na matumaini makubwa ya kupata nyongeza ya mishahara. 

 Rais Samia ni mara ya pili kuhudhuria sherehe hizo tangu aapishwe kuwa Rais ambapo kwa mwaka jana akiwa jijini Mwanza kwenye Sherehe za Mei mosi alisema hawezi kuongeza mishahara ya wafanyakazi hadi mwaka huu wa 2022 kutokana na kuwepo vikwazo mbalimbali ikiwamo janga la Corona (Uviko-19).

 

Pia alisema alishindwa kuongeza mishahara kutokana na hatua anazopanga kuchukua za kufuta kodi na tozo zilizokuwa zinawabughudhi Watanzania zilizosababisha kupungua kwa mapato yatokanayo na kodi.

 

Wafanyakazi macho na masikio yatakuwa kwake ili kufahamu atazungumza nini kuhusu maslahi na mustakabali wa ajira zao hasa kuongeza kima cha chini cha mshahara katika sekta ya umma na ile ya sekta binafsi na kupandisha madaraja wafanyakazi wa umma.

 

Akizungumza na Nipashe leo, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU), Dk.Paul Loisulie, amesema matarajio ya wafanyakazi leo ni Rais Samia kutimiza ahadi yake.

 

“La kwanza na la muhimu kuliko yote ni Rais kutamka neno la kutekeleza ahadi yake ya mwaka jana kwamba tarehe 01.05.2022 mwaka huu atatangaza nyongeza ya mishahara. Tamko likija tofauti na ahadi ya mwaka jana wafanyakazi hawaelewa kabisa, sasa hivi wafanyakazi wana mategemeo makubwa sana,”amesema.

 

Pia amesema wanatarajia kusikia kauli ya Rais kuhusu mikakati ya Serikali kuboresha maslahi ya wafanyakazi katika maeneo mbalimbali kama vile bima ya afya, maboresho ya sheria mbalimbali, mafao ya kustaafu na mengine yafananayo.

 

“La kufurahisha ni kwamba wafanyakazi wana morali kubwa ya kushiriki kwenye maandamano kwa sababu wana matarajio,”amesema.

 

Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Deus Seif, amesema wanatarajia makubwa zaidi kutoka kwa Rais Samia kutokana na ndani ya mwaka mmoja ameonesha kutekeleza ahadi za walimu kwa asilimia 95 ikiwamo kupandisha madaraja na vyeo.

“Tumepata mafanikio mengi ndani ya Mwaka mmoja wa uongozi wake walipandishwa walimu 127,000, Juzi Waziri wa Utumishi(Waziri wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama) amepitishiwa bajeti ya kupandisha vyeo walimu 92,000 miongoni mwao walimu 60,000, lakini Julai mosi mwaka huu daraja la mserereko litagusa walimu 59,000 miongoni mwao walimu 52,000, kwa hiyo jumla ni walimi 260,000 kati ya 285,000, yaani asilimia 92.8 ya walimu wamenufaika kabla ya Mei mosi,”amesema.

Amesema kabla ya Mei mosi tayari wamenufaika na kwamba upandaji wa madaraja kwao ni zaidi ya nyongeza ya mishahara.

“Walimu katika hali ya ukweli kabisa sasa tunatakiwa tufundishe watoto wa watanzania maskini, tusimamie utoaji elimu bora kwa kuwa ni watumishi pekee walioguswa kwa asilimia 95 kuhusu maslahi yao, tuwatendee haki watoto wetu tukatimize wajibu wetu,”amesema.

Habari Kubwa