Madagascar yaweka amri kutotoka nje ongezeko la corona

06Jul 2020
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Madagascar yaweka amri kutotoka nje ongezeko la corona

Rais wa Madagascar, Andry Rajoelina ametoa amri ya kutotoka nje kwa wakazi wa mji mkuu wa Antananarivo na eneo la Analamanga kufuatia ongezeko jipya la maambukizi ya virusi vya corona, miezi miwili baada ya masharti hayo kuondolewa.

Rais wa Madagascar Andry Rajoelina.

''Hakuna magari yatakayoruhusiwa kuingia ama kutoka katika eneo hilo kuanzia leo Jumatatu hadi Julai 20 na masharti makali yatawekewa wanaotoka nje,''

''Ni mtu mmoja mmoja katika kila familia atakayeruhusiwa kwenda barabarani kati ya saa 10 na saa 12 asubuhi na saa 6 mchana'', ilisema taarifa hiyo.

Hatua hizo zimechukuliwa kutokana na kusambaa kwa mlipuko huo na kuongezeka kwa visa vya Covid-19, iliongezea.

Madagascar ilikuwa imezoea kuandikisha visa vichache kwa siku vya ugonjwa huo lakini sasa ,taifa hilo katika siku za hivi karibuni limethibitisha idadi kubwa ya wagonjwa wa Covid 19 kila siku , ambapo wagonjwa 216 waliripotiwa siku ya Jumamosi baada ya watu 675 kupimwa.

Tangu virusi hivyo vilipogunduliwa katika kisiwa hicho Machi 20 , taifa hilo lilikuwa na jumla ya wagonjwa 2,728 ikiwemo watu 29 waliofariki kufikia siku ya Jumapili.

Aprili , Rais wa nchi hiyo alizindua dawa ya Mitishamba ambayo alidai inazuia na kuponya virusi hivyo vya corona.

Rajoelina amekuwa akikuza dawa hiyo kwa lengo la kuiuza katika nchi za kigeni, akiitaja kuwa 'dhahabu ya kijani' itakayobadili historia ya taifa hilo.

Manufaa ya dawa hiyo ya Covid Organics, inayotokana na mmea wa pakanga - mmea unaotibu malaria pamoja na mitishamba mingine hayajathibitishwa na utafiti wa kisayansi.

Chanzo: BBC 

Habari Kubwa