Madai ya talaka yaongezeka Pemba, Unguja

14Feb 2018
Rahma Suleiman
Nipashe
Madai ya talaka yaongezeka Pemba, Unguja

NAIBU Waziri wa Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Khamis Maalim, amesema kuwa kesi za madai ya talaka kwa wanandoa zimezidi kuongezeka katika Mahakama za Kadhi Unguja na Pemba.

Akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Konde, Omar Seif Abeid, katika kikao cha Baraza la Wawakilishi, aliyetaka kujua ni migogoro mingapi ya talaka na madai ya matunzo ya watoto iliyoripotiwa katika Mahakama za Kadhi kwa Unguja na Pemba, Naibu waziri huyo, alisema kwa madai ya takala kesi zilizofunguliwa Unguja ni 884 na kesi 440 zimetolewa uamuzi huku 444  zinaendelea.

Alisema kwa upande wa Pemba kesi za madai ya talaka zilizofunguliwa ni 334 na kesi 249 zimetolewa uamuzi, 85 bado zinaendelea.Akieleza kuhusu matunzo ya watoto, alisema takwimu zinaonyesha kesi zilizoripotiwa ni 35 kwa Unguja na kesi 17 zimetolewa uamuzi na kesi 18 bado zinaendelea.

"Kesi za matunzo ya watoto zilizoripotiwa Pemba ni 22 na kesi 18 zimetolewa uamuzi, nne bado zinaendelea,"alisema.Aidha alisema ili kulinda ndoa zisivunjike ovyo, ni jukumu la jamii  kuelimisha wanandoa waweze kustahamiliana ili ndoa hizo zisivunjike.  

Habari Kubwa