Madaktari bingwa 11 Wachina watua nchini

26Jan 2022
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Madaktari bingwa 11 Wachina watua nchini

SERIKALI imepokea timu ya madaktari bingwa 11, kutoka Serikali ya China waliobobea katika magonjwa ya ubongo, mishipa ya fahamu, mifupa, dawa za usingizi, ganzi na moyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk Respicious Boniface (watatu kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya timu ya madaktari bingwa kutoka China, kulia kwake ni Dk Meng Yong kiongozi wa timu ya madaktari bingwa hao, kushoto kwake ni Dk Zhang Bo na wa kwanza kulia ni Dk Lou Yanhua. Wengine ni Muwakilishi wa Wizara ya Afya Dk Vumilia Liggyle wa kwanza.

Madaktari hao watafanya kazi nchini kwa miaka miwili, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya(MZRH).

Ujio wa madaktari hao nchini ni kupitia mkataba ulioingia Wizara ya Afya na Serikali ya China Septemba, mwaka jana wa ushirikiano wa kutoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi pamoja na kuleta madaktari bingwa kutoka nchini humo kutoa huduma katika hospitali za kibingwa nchini.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, wakati wa kuwapokea madaktari hao, Mwakilishi wa Wizara ya Afya, Dk. Vumilia Liggyle, alisema ushirikiano baina ya serikali hizo mbili ni wa kihistoria kwa sababu una zaidi ya miaka 50.

Alisema ushirikiano huo umekuwa ukiwanufaisha wataalamu kwenda nchini China kupata mafunzo na madaktari bingwa kutoka nchini humo kuja Tanzania kutoa huduma.

“Tumepokea jumla ya madaktari bingwa 11 kutoka China, watatoa huduma za kibingwa katika maeneo mbalimbali nchini kwa miaka miwili katika hospitali zetu nne za kibingwa,” alisema Dk. Liggyle.

Alisema ujio wa madaktari hao ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuhakikisha huduma zote za kibingwa zinapatikana nchini na kuifanya Tanzania kuwa kituo cha matibabu barani Afrika.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk. Respicious Boniface, alisema madaktari hao pia watafundisha wanafunzi.

“Ujio wa wataalamu hawa una tija kubwa kwa MOI na nchi kwa ujumla kwa sababu watafanya upasuaji kwa kushirikiana na madaktari bingwa wazalendo jambo ambalo litawezesha kubadilishana uzoefu na kupeana mbinu za kisasa.

“Pia watatoa mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi kwani moja ya malengo ya MOI ni kutoa mafunzo,” alisema Dk. Boniface.

Kwa upande wake, kiongozi wa timu ya madaktari bingwa kutoka China, Dk. Meng Yong, alisema ni heshima kubwa kupata fursa ya kufanya kazi Tanzania.

Alisema wanafuraha kuja kuwahudumia Watanzania kwa kipindi cha miaka miwili na pia watapata nafasi ya kubadilishana uzoefu na madaktari bingwa wenzao wa Tanzania na kujifunza mambo mengi.

Habari Kubwa