Madaktari bingwa watoa mafunzo huduma za saratani, upandikizaji   

16Jul 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Madaktari bingwa watoa mafunzo huduma za saratani, upandikizaji   

WATAALAMU kutoka Hospitali ya Chuo Kikuu Oxford nchini Uingereza, wameanza kutoa mafunzo kwa madaktari bingwa wa damu, saratani na wauguzi jinsi ya kuhudumia wagonjwa wa saratani na watakaopandikizwa uloto.

Mtaalam wa Tiba ya Magonjwa ya Saratani kutoka Hospitali ya Chuo Kikuu cha OXFORD nchini Ungereza, Finn Tysoe, akitoa mafunzo wa wataalam mbalimbali wa MNH leo.

Hatua hiyo ni mwendelezo wa maandalizi ya kutoa huduma ya upandikizaji uloto kwa mara ya kwanza nchini, matibabu ambayo yalikuwa hayapatikani kutokana na kutokuwapo wataalamu au ukosefu wa vifaa vya kutolea huduma husika.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo, Ushauri na Utafiti,  Dk. Faraja Chiwanga, alisema mafunzo hayo ambayo yameanza kutolewa Muhimbili yanahusisha madaktari bingwa 20 wa magonjwa ya damu na saratani na zaidi ya wauguzi 30.

 Alisema Juni, mwaka huu, Muhimbili ilipeleka wataalamu 11 India katika Hospitali ya Apollo kwa kipindi cha mwezi mmoja, ili kujifunza kwa vitendo jinsi ya kufanya upandikizaji wa uloto.

"Uwapo wa huduma hii utasaidia wananchi wengi kutibiwa nchini, kujenga uwezo kwa wataalamu wa ndani na itapunguza mzigo kwa serikali kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa sababu gharama za kufanya upasuaji nchini zitashuka kwa zaidi ya asilimia 50 kwa mgonjwa mmoja," alisema Dk. Chiwanga.

Alisema wagonjwa wenye tatizo hilo walikuwa wakipelekwa nje ya nchi na kutibiwa kwa gharama ya Sh. milioni 200, hivyo kwa MNH mgonjwa atagharimiwa chini ya asilimia 50.

Dk. Chiwanga alisema wataalamu hao ni pamoja na madaktari bingwa watatu wa magonjwa ya damu, wataalamu wa maabara watatu, wahandisi watatu mmoja wa ufundi, ujenzi na vifaa tiba na mtaalamu wa fedha ili kufanya uchambuzi wa gharama halisi za huduma hiyo na mtaalamu wa ununuzi kufanya uchambuzi yakinifu wa dawa na vitendanishi.

Alisema wataalamu hao wanatarajia kurejea nchini mwishoni mwa mwezi huu kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mwisho ya kutoa huduma hiyo mwishoni mwa mwaka huu.

"Tayari wauguzi watatu, wataalamu wa saratani ya watoto watatu, mfamasia mmoja na wataalamu wengine wawili wa damu wamepata mafunzo ya huduma hiyo katika Hospitali ya Apollo, India kwa kipindi cha miezi mitatu," Dk. Chiwanga alisema.

NAMNA YA KUPANDIKIZA

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Lawrence Maseru, Dk. Chiwanga alisema huduma hiyo hufanyika kwa kupandikiza chembechembe mama za kuzalisha damu ambazo hupatikana kwenye uloto au chembechembe mama kutoka kwenye kitovu cha mtoto mchanga au kondo la nyuma la mama.

"Njia ambayo hutumika mara nyingi ni ile ya upandikizaji wa chembechembe mama za damu (HSCT) kutoka kwenye uloto.

Upandikizaji huu unaanza kwa kumwandaa mgonjwa ambaye chembechembe zake za damu zina tatizo kama saratani, selimundu au wale ambao mifupa yao inashindwa kuzalisha damu," alisema mtaalamu huyo.

Alifafanua kuwa upandikizaji huo hufanyika kwa kuwapa tiba maalum ili kuua chembechembe zote zenye matatizo kisha kupandikiza chembechembe mpya zilizomo kwenye uloto kutoka kwa ndugu mwenye vinasaba vinavyofanana au chembechembe mpya zilizozalishwa kutoka kwa mgonjwa mwenyewe baada ya kupata tiba maalum.

Dk. Chiwanga alisema huduma hiyo ndiyo tiba pekee inayoweza kuponya wagonjwa wenye matatizo hayo.

Kwa mujibu wa takwimu za Muhimbili, wagonjwa takribani 130 hadi 140 wanahitaji huduma ya kupandikizwa uloto kwa mwaka na zaidi ya theluthi mbili ya wagonjwa hao hufariki dunia kwa kukosa huduma hiyo.

Habari Kubwa