Madaktari Saudia Arabia wapiga kambi Muhimbili

15Mar 2019
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Madaktari Saudia Arabia wapiga kambi Muhimbili

JOPO la madaktari kutoka Saudi Arabia wameweka kambi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kutoa matibabu kwa watoto.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, Hemed Mgaza, alisema madaktari wametoka katika hospitali mbalimbali za nchi hiyo ambazo zimebobea katika magonjwa ya watoto.

Alisema mbali na kutoa huduma kwa watoto, jopo hilo pia linatoa mafunzo kwa madaktari kutoka katika hospitali mbalimbali nchini.
"Madaktari hawa huwa wanakuja kila mwaka na safari hii mbali na kuja kutoa huduma ya matibabu, wamekuja pia kutoa mafunzo kwa madaktari wa Tanzania katika hospitali mbalimbali nchini, ambao wanahudumia katika wodi za uangalizi maalum," alisema.

Balozi huyo aliongeza: "Mafunzo haya ni muhimu sana kwa sababu, kundi la wagonjwa wa namna hii linahitaji uangalizi wa hali ya juu na wa kitaalamu zaidi kuokoa maisha yao. Kwa hiyo, tunashukuru kwamba yatakuwa na tija kwa nchi yetu.”

Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Mohamed Bakari, alisema Tanzania ina mpango mkubwa wa kuhakikisha inawekeza zaidi kwa wataalamu wabobezi katika sekta ya afya.

“Tanzania tuna mpango mkubwa wa kuhakikisha tunawekeza zaidi katika wataalamu wabobezi katika maeneo mbalimbali ya utoaji huduma kwenye sekta ya afya.

"Kwa mfano, kwa Muhimbili ni eneo ambalo ni mtaji wetu wa kuzalisha wataalamu hao na hapa ndipo panaweza kuleta tafsiri nzuri namna ambavyo serikali imejizatiti kuongeza nguvu katika suala hilo.

"Tunafanya juhudi hizi ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora zaidi za kiafya hususani ambazo ni za kibobezi na ndiyo maana tunaendelea kufanya juhudi mbalimbali za kufanikisha hilo, ikiwa ni pamoja na timu mbalimbali kama hizi za wataalamu wanaokuja nchini kwetu kutuongezea utaalamu," Prof. Bakari alisema.

Aliishukuru serikali ya Saudi Arabia kwa mchango huo na ushirikiano wao hususani katika sekta ya afya, huku akiahidi kwa watahakikisha ushirikiano huo unakuwa wa kudumu.