Madeni yalivyokwamisha serikali miaka mitatu

14Jun 2018
Na Mwandishi Wetu
DODOMA
Nipashe
Madeni yalivyokwamisha serikali miaka mitatu

SERIKALI imepandisha makusanyo yake kutoka wastani wa Sh. bilioni 850 kwa mwezi kabla ya Novemba 2015 hadi kufikia wastani wa Sh. trilioni moja kwa mwezi, kwa mujibu wa taarifa za kila baada ya miezi mitatu zinazotolewa na Mamlaka ya Mapato (TRA).

Hata hivyo, pamoja na jitihada zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano kuimarisha makusanyo ya nchi kwa kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato, bado kuna utekelezaji usioridhisha wa miradi ya maendeleo inayoidhinishwa na Bunge.

Wakati Bajeti Kuu ikisomwa bungeni jijini Dodoma baadaye leo, imeelezwa na serikali kuwa utekelezaji duni wa bajeti ya maendeleo katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita unatokana na kiwango kikubwa cha makusanyo kutumika kulipa Deni la Taifa na mishahara ya watumishi wa umma.

Taarifa zilizowasilishwa bungeni wakati wa Bunge la Bajeti linaloendelea jijini Dodoma, zinaonesha utekelezaji wa bajeti ya maendeleo kwa mwaka huu wa fedha (2017/18) umekuwa chini ya asilimia 50 karibu kwa wizara zote huku baadhi ya wizara zikiwa hazijapewa hata senti moja.

Jitu Soni, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, aliliambia Bunge Jumatatu iliyopita kuwa kamati yake imebaini kuwa kati ya mafungu yote 47 ya wizara mbalimbali yaliyostahili kupata fedha za maendeleo mwaka huu wa fedha, ni mafungu 16 tu yaliyokuwa yamepata fedha kwa zaidi ya asilimia 50 hadi Machi 31, mwaka huu.

Soni aliweka wazi kuwa kamati yake imebaini kiasi kikubwa cha fedha zinazokusanywa na serikali kinatumika kulipa Deni la Taifa, akibainisha kuwa hadi Februari mwaka huu, serikali ilikuwa imelipa Sh. trilioni 5.54. Kati yake, Sh. trilioni 4.094 ni madeni ya ndani na Sh. trilioni 1.446 ni madeni ya nje.

"Kulingana na Tathmini ya Uhimilivu wa Deni (Debt Sustainability Analysis), deni letu ni himilivu kwa asilimia 34.4 ukilinganisha na ukomo wa asilimia 56," Soni alisema.

"Hata hivyo, ukilinganisha makusanyo ya ndani yanayotokana na kodi na malipo ya Deni la Taifa, utaona kuwa mpaka Desemba 2017, makusanyo ya ndani yalikuwa Sh. trilioni 7.678 na malipo ya Deni la Taifa mpaka Februari ya Sh. trilioni 5.54, ni kwamba kiasi kikubwa cha makusanyo ya ndani kinakwenda kulipa Deni la Taifa," alifafanua.

Wakati Bunge likibainisha hayo, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2016/17 iliyowasilishwa bungeni Aprili 11, mwaka huu, ilionesha malengo ya makusanyo ya serikali kwa mwaka huo wa fedha yalifikia asilimia 94 ya lengo, lakini fedha za miradi ya maendeleo zinazotolewa ni chini ya asilimia 50.

 

KAULI YA SERIKALI

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango akizungumzia changamoto hiyo jijini Dodoma hivi karibuni, alisema inasababishwa na sehemu kubwa ya makusanyo kutumika kulipa madeni ya serikali na mishahara kwa watumishi wa umma.

Alisema serikali inakusanya wastani wa Sh. trilioni 1.3 kwa mwezi lakini kati yake, Sh. bilioni 550 hutumika kulipa mishahara ya watumishi wa umma, Sh. bilioni 600 hutumika kulipa Deni la Taifa na kiasi kinachobaki hutumika kutekeleza miradi ya maendeleo.

"Kwa hiyo, kwenye Sh. trilioni 1.3 umebakiwa na Sh. bilioni 200 ambazo ndizo unatumia kuendesha serikali," alisema Dk. Mpango na kueleza zaidi:

"Lakini humo namo kuna shughuli nyingine ambazo hazikwepeki. Kwa mfano, askari wetu shupavu wanalala nje, lazima serikali tuwape posho ya chakula, ndipo na sisi tunaweza kuendeleza vurugu huku bungeni, tukabishana, tukalala nyumbani kwa amani.

"Kuna mishahara ya majaji lazima ilipwe na marupurupu yao mengine, kuna viongozi wetu nao hawalali. Niwahakikishie ni kawaida kabisa kumpigia Rais simu saa nane usiku, saa tisa tuko macho. Hawa viongozi wamebeba dhamana kubwa, lazima serikali iwahudumie. Kwa hiyo, unaponiuliza hizi nyingine zinaenda wapi, ninaweza nikaendelea na kuendelea."

Mtaalamu huyo wa uchumi na fedha alibainisha kuwa serikali ya awamu ya nne ilikuwa inakusanya wastani wa Sh. bilioni 850 kwa mwezi, lakini tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani Novemba 5, 2015, imekuwa ikikusanya wastani wa Sh. trilioni 1.3 kwa mwezi.

"Kwa hiyo, ni rahisi sana kuhesabu hicho kinachoingia mfukoni, lakini ni muhimu kuangalia kinachotoka, zinatoka zinakwenda kwenye nini?

"Ulipaji wa Deni la Taifa inategemea, kwa mwezi inaweza ikatoka Sh. bilioni 600, tumewahi kwenda mpaka Sh. bilioni 900 kutegemeana na madeni hayo yanaiva wakati gani.

"Mwezi huu unaweza ukalipa Sh. bilioni 600 na kidogo, mwezi ujao ukalipa Sh. bilioni 700, ni kwa sababu ya tofauti ya ile mikopo inaiva wakati gani.

"Ukichukua wastani wa Sh. bilioni 550 mishahara, ukaongeza Sh. bilioni 600 kwa ajili yakulipia Deni la Taifa, tayari Sh. trilioni 1.1 umeitumia kwa hivyo vitu viwili ambavyo huwezi kuvikwepa," Dk. Mpango alifafanua.

 

HALI ILIVYO WIZARANI

Kwa mujibu wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, wizara yake iliidhinishiwa Sh. bilioni nne kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo mwaka huu wa fedha, lakini hadi Machi 31, mwaka huu, hakuna hata senti moja iliyokuwa imetolewa.

Kutokana na hali hiyo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji haikwenda kukagua mradi wowote ulio chini ya wizara hiyo kwa kuwa miradi yote haikupelekewa fedha, hivyo kulikwamisha Bunge kutekeleza wajibu wake wa kikatiba wa kuisimamia na kuishauri serikali.

Katika mwaka wa fedha 2015/16, Sh. bilioni 19.4 zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, lakini hakuna hata shilingi moja iliyokuwa imetolewa hadi Machi 31, 2016.

Kwa upande wa iliyokuwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, kati ya Sh. bilioni 32 zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo mwaka 2015/16, ni Sh. bilioni 5.1 (asilimia 15) pekee ndiyo zilizotolewa hadi kufikia Machi 31, 2016.

Pia, kati ya Sh. bilioni 101.527 zilizoidhinishwa kutekelezaji miradi ya maendeleo katika sekta ya kilimo mwaka 2016/17, ni Sh. bilioni 3.369 (asilimia 3.32) zilizokuwa zimetolewa hadi Mei 4, mwaka jana.

Kwa mwaka 2016/17, Fungu 99 (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi), hadi Mei 4, 2017, kati ya Sh. bilioni 15.873 zilizoidhinishwa kutekeleza miradi ya maendeleo, ni Sh. bilioni 1.252 (asilimia 7.9) zilizokuwa zimepokewa kutoka Hazina.

Kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Dk. Mary Nagu, alisema kuwa ukosefu wa fedha uliathiri upimaji wa maeneo ya kilimo na kuyapatia hati miliki, usambazaji wa pembejeo za kilimo, ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji na ujenzi na ukarabati wa maghala.

Katika serikali ya awamu ya nne, wizara hizo mbili zinazogusa zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania, zilikuwa zimetenganishwa kabla ya Rais John Magufuli kuziunganisha mwaka 2015 na baadaye kuzitenganisha tena Oktoba 7, 2017.

 

MAJI NA UMWAGILIAJI

Hadi Machi 31, 2016, Sh. bilioni 81.425 (asilimia 19.06) zilikuwa zimepokewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa mwaka 2015/16.

Vilevile, kati ya Sh. bilioni 53.594 zilizoidhinishwa kwa ajili ya maendeleo ya Tume ya Umwagiliaji mwaka huo wa fedha, ni Sh. bilioni 5.131 (asilimia 9.6) zilizokuwa zimepokewa hadi Machi 31, 2016.

Kwa mwaka 2016/17, Bunge liliidhinisha Sh. bilioni 915.194 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya sekta ya maji. Hadi Machi 31, 2017, Sh. bilioni 181.209 (asilimia 19.8) zilikuwa zimetolewa.

Kati ya Sh. bilioni 181.209 zilizotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya sekta hiyo, Sh. bilioni 95.507 ni za Mfuko wa Maji zilizopatikana kupitia makato ya Sh. 50 kwa kila lita ya mafuta ya petroli na dizeli.

Kwa mwaka 2017/18, hadi Machi 31, mwaka huu, Fungu 5 (Tume ya Taifa ya Umwagiliaji) lilikuwa limepokea Sh. bilioni 2.468, sawa na asilimia 12.3 ya Sh. bilioni 24.159 zilizoidhinishwa kwa ajili ya maendeleo ya tume hiyo.

Pia, hadi Machi 31, mwaka huu, Fungu 49 (Wizara ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji) lilikuwa limepatiwa Sh. bilioni 123.191, sawa na asilimia 22 ya Sh. bilioni 623.607 zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

 

OFISI MAKAMU RAIS

Kwa mujibu wa Mohamed Mchengerwa, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, hadi Machi 26, mwaka huu, Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais - Muungano na Mazingira haikuwa imepokea hata senti moja kati ya Sh. bilioni moja zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya miradi miwili ya maendeleo.

Miradi hiyo ni ya ujenzi wa Ofisi na Makazi ya Makamu wa Rais (Zanzibar) na Ujenzi na Ukarabati wa Ofisi ya Makamu wa Rais Luthuli II (Dar es Salaam).

Pia, hadi Machi 8, mwaka huu, hakuna hata senti moja ya fedha za ndani zilizokuwa zimetolewa kati ya Sh. bilioni mbili zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya Mfuko wa Mazingira mwaka huu wa fedha.

Kwa mwaka 2016/17, Bunge liliidhinisha Sh. bilioni 10.973 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya wizara hiyo. Hata hivyo, hadi Machi 15, 2017, ni Sh. bilioni 1.238 (asilimia 11.3) zilizokuwa zimepokewa.

 

Jedwali Na. 1: Mtiririko wa fedha za mradi ya maendeleo ya baadhi ya wizara kwa kipindi cha robo tatu ya kila mwaka wa fedha kuanzia 2015/16 hadi 2017/18.

 

Mwaka Wizara  Zilizotengwa,  Zilizopokewa Asilimia    

2015/16 Elimu  Bil. 582.67/- Bil. 360.9/- 61%   

2016/17 Elimu Bil. 897.658/- Bil. 500.4/-  55%   

2017/18 Elimu  Bil. 916.841/- Bil. 594.6/-  65%   

2015/16 Kilimo Bil. 32  Bil. 5.1 15   

2016/17 Kilimo Bil. 101.527/- Bil. 3.369/-  3.32%    

2017/18 Kilimo Bil. 150.253/- Bil.27.231/-  18%   

2015/16 Mifugo Bil. 19.4/- 0 0%   

2016/17 Mifugo Bil. 15.873 Bil. 1.252/- 7.9%   

2017/18 Mifugo Bil. 4/- 0  0%   

2015/16 Utalii Bil. 7.709/- Bil. 1/- 12.9%    

2016/17 Utalii Bil. 17.747/- Mil. 156.69/- 8%    

2017/18 Utalii Bil. 51.8/- Bil. 27.9/- 53.9%    

2016/17 Katiba Bil. 37.459/- Bil. 3.523/- 9%   

2015/16 Katiba Bil. 15.381/- Bil. 13.209/- 85%   

2015/16 Viwanda Bil. 35.387/- Bil. 1.602/- 4.5%    

2015/16 Habari Bil. 3/-  Bil. 1/- 33.3%    

2016/17 Habari Bil. 3/-  Mil. 190.32/- 6.3%   

2015/16 Ndani  Bil. 79.689/- Bil. 4.626/- 5.8%    

2016/17 Ndani Bil. 47.923/- Bil. 13/- 28%   

2016/17 Fedha  Bil.791.998/- Bil. 18.898/- 2.3%   

2017/18 Fedha  Trl. 1.429/- Bil.81.257  5.7 %

CHANZO: Taarifa za Kamati za Kudumu za Bunge

 

MALIASILI, UTALII

Wizara ya Maliasili na Utalii iliidhinishiwa na Bunge Sh. bilioni 97.2 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo mwaka 2017/18. Hata hivyo, hadi Machi 31, mwaka huu, ni Sh. bilioni 27.9 (asilimia 53) zilizokuwa zimepokewa.

Mei 21, mwaka huu, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, alisema bungeni kuwa miradi iliyoathirika kutokana na upatikanaji usioridhisha wa fedha ni pamoja na wa kujenga uwezo wa mapori ya akiba na kikosi dhidi ya ujangili.

Mwaka 2015/16, wizara hiyo iliidhinishiwa na Bunge Sh. bilioni 7.709 kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Hata hivyo, hadi Machi 31, 2016, ilikuwa imepokea Sh. bilioni moja (asilimia 12.9).

Kwa mwaka 2016/17, Bunge liliidhinisha Sh. bilioni 17.747 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wizara hiyo, lakini hadi Februari 28, mwaka huu, ni Sh. milioni 156.688 asilimia nane) zilizokuwa zimepokewa.

 

KATIBA NA SHERIA

Sh. bilioni 23.237 ziliidhinishwa na Bunge kwa ajili ya maendeleo ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka 2017/18. Kati yake, Sh. bilioni 18 ni fedha za ndani na Sh. bilioni 5.237 ni fedha za nje.

Kwa mujibu wa Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi, hadi Machi 31, mwaka huu, Sh. bilioni 10.478 zilikuwa zimepokewa zikiwamo fedha za ndani Sh. bilioni 9.261 (asilimia 51) na fedha za nje Sh. bilioni 1.217 (asilimia 23).

Kwa mwaka 2015/16, wizara hiyo iliidhinishiwa Sh. bilioni 15.381 kutekeleza miradi ya maendeleo. Kati yake, Sh. bilioni 13.319 zilikuwa fedha za ndani na za nje zilikuwa Sh. bilioni 2.062.

Hadi Aprili 30, 2016, wizara hiyo ilikuwa imepokea Sh. bilioni 13.209, sawa na asilimia 85 ya fedha zote zilizoidhinishwa na Bunge kutekeleza miradi ya maendeleo.

Mwaka uliofuata, wizara hiyo iliidhinishiwa na Bunge Sh. bilioni 37.459, ili kutekeleza miradi ya maendeleo. Kati yake, Sh. bilioni 13.919 ni fedha za ndani na Sh. bilioni 23.54 ni fedha za nje.

Hata hivyo, Prof. Kabudi aliliambia Bunge mjini hapa Aprili 25, mwaka jana kuwa hadi Machi 31, 2017, wizara ilikuwa imepokea Sh. bilioni 3.523, sawa na asilimia tisa ya fedha zilizoidhinishwa kuteleza miradi ya maendeleo.

 

ELIMU

Katika mwaka wa fedha 2015/16, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliidhinishiwa na Bunge Sh. bilioni 582.67 kwa ajili ya maendeleo. Kati yake, Sh. bilioni 418.3 zilitengwa kwa ajili ya kugharamia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, hata hivyo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Peter Serukamba, alisema bungeni Mei 26, 2016 kuwa kamati yake ilibaini kuwa, katika robo tatu ya mwaka wa fedha (yaani hadi Machi 31, 2016), wizara ilikuwa imepokea Sh. bilioni 360.9, sawa na asilimia 61.9 ya fedha iliyoidhinishwa.

Alisema kamati yake ilikagua mradi wa kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ambao ulikuwa Sh. bilioni 418.3 na kubaini kuwa, hadi Machi 2016, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ilikuwa imepokea Sh. bilioni 245, sawa na asilimia 55.9 ya fedha iliyoidhinishwa.

Kwa mwaka uliofuata, wizara hiyo iliidhinishiwa Sh. bilioni 897.658 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na hadi Machi 31, 2017, Sh. bilioni 500.4 (asilimia 55) zilikuwa zimetolewa.

Hata hivyo, mgawanyo wa fedha hizo za maendeleo unaonesha Sh. bilioni 427 (asilimia 48) zilikuwa za kugharamia mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na Sh. bilioni 470 (asilimia 52) ni miradi halisi ya maendeleo ya sekta ya elimu inayotekelezwa na wizara ukiwamo ujenzi wa miundombinu ya shule na vyuo.

Randama ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2016/17 Fungu 46, ilionesha kuwa kati ya Sh. bilioni 427 zilizoidhinishwa kwa ajili ya HESLB, Sh. bilioni 344 zilikuwa zimetolewa hadi kufikia Machi 31, 2017, sawa na asilimia 80 ya fedha hizo.

Pia ilionesha kuwa hadi Machi 31, 2017, Sh. bilioni 156.4 zilikuwa zimetolewa na Hazina, sawa na asilimia 30 ya Sh. bilioni 470 zilizoidhinishwa kwa ajili ya miradi mingine ya maendeleo ya wizara hiyo.

 

VIWANDA, BIASHARA

Katika mwaka 2015/16, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, iliidhinishiwa Sh. bilioni 35.387 kutekeleza miradi ya maendeleo. Hata hivyo, hadi Machi 31, 2016, Sh. bilioni 1.602 zilikuwa zimepokewa, sawa na asilimia 4.5 ya fedha zote zilizoidhinishwa na Bunge.

Kwa mwaka uliofuata, wizara hiyo iliidhinishiwa na Bunge Sh. bilioni 40 kutekeleza miradi ya maendeleo, lakini hadi robo tatu ya mwaka inakamilika Machi 31, 2017, ni Sh. bilioni 7.567 zilizokuwa zimepokewa, sawa na asilimia 18.92 ya fedha zote zilizoidhinishwa.

 

WIZARA YA HABARI

Katika wa mwaka wa fedha 2015/16, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iliidhinishiwa na Bunge Sh. bilioni tatu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, sawa na kiwango kilichoidhinishwa kutekeleza miradi hiyo mwaka 2016/17.

Hata hivyo, hadi Aprili 30, mwaka huu, serikali ilikuwa imetoa Sh. bilioni moja tu, sawa na asilimia 33.3 ya fedha zote zilizoidhinishwa.

Kutokana na changamoto hiyo ya ukosefu wa fedha, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii (Serukamba) alisema miradi ya wizara hiyo ikiwamo ya Ujenzi wa Ofisi za Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita), Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika na Ujenzi wa Ukumbi wa Wazi wa Maonesho ya Sanaa haijatekelezwa.

Serukamba alisema miradi mingine ni Ujenzi wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya, Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, Programu ya Habari kwa Umma na Upanuzi wa Usikivu wa Shirika la Utangazaji (TBC).

Pia, hadi Februari 28, 2017, wizara ilikuwa imepokea Sh. milioni 190.32 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, sawa na asilimia 6.3 ya Sh. bilioni tatu zilizoinidhinishwa na Bunge kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya wizara hiyo mwaka 2016/17.

 

MAMBO YA NDANI

Bunge liliidhinisha Sh. bilioni 79.689 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka 2015/16. Hata hivyo, hadi Machi 31, 2016, wizara ilikuwa imepokea Sh. bilioni 4.626, sawa na asilimia 5.8 ya fedha zilizoidhinishwa.

Kwa mwaka 2016/17, wizara hiyo iliidhinishiwa Sh. bilioni 47.923 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na hadi Machi 31, 2017, Sh. bilioni 13 zilikuwa zimepokewa kutoka Hazina kutekeleza miradi ya maendeleo, sawa na asilimia 28 ya fedha zote zilizoidhinishwa na Bunge.

 

ARDHI

Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, wizara yake iliidhinishiwa Sh. bilioni 3.458 (fedha za nje) kwa ajili ya kutekeleza mradi wa Umilikishaji Ardhi kwa mwaka 2015/16.

Hata hivyo, hadi Machi, 2016, Sh. milioni 745.281 zilikuwa zimepokewa na wizara, sawa na asilimia 21.5 ya fedha zote za maendeleo zilizoidhinishwa.

Kwa 2016/17, Bunge liliidhinisha Sh. bilioni 25 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wizara hiyo. Kati yake, Sh. bilioni 15.301 ni fedha za ndani na Sh. bilioni 10 ni fedha za nje.

Hadi Mei 15, 2017, Sh. bilioni 4.201 (asilimia 27) zilikuwa zimetolewa kati ya fedha za ndani zilizoidhinishwa.

 

TAMISEMI

Kwa mwaka 2016/17, Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) iliidhinishiwa na Bunge Sh. trilioni 1.602 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Hata hivyo, hadi Februari 28, 2017, ofisi hiyo na taasisi zake ilikuwa imepokea jumla ya Sh. bilioni 183.668 kutoka Hazina, sawa na asilimia 11.49 ya fedha zote zilizoidhinishwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Kwa mwaka 2017/18, ofisi hiyo iliidhinishiwa Sh. bilioni 417.257 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, lakini hadi kufikia Februari 28, mwaka huu, ni Sh. bilioni 216.104 (asilimia 52) zilizokuwa zimetolewa.

 

WIZARA YA FEDHA

Bunge liliidhinisha Sh. bilioni 791.998 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Wizara ya Fedha na Mipango mwaka wa fedha 2016/17. Kati yake, Sh. bilioni 723.15 ni fedha za ndani na Sh. bilioni 68.848 ni fedha za nje.

Hata hivyo, hadi Machi 31, 2017, wizara hiyo ilikuwa imepokea Sh. bilioni 18.898, sawa na asilimia 2.3 ya fedha zote zilizoidhinishwa na Bunge.

Kwa mwaka 2017/18, wizara hiyo iliidhinishiwa Sh. trilioni 1.429 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, lakini hadi Aprili mwaka huu, ni Sh. bilioni 81.257 (asilimia 5.7) zilizokuwa zimetolewa.

 

NINI KIFANYIKE

Katika mahojiano na Nipashe jijini Dodoma wiki iliyopita, Waziri Kivuli wa Fedha na Mipango, Halima Mdee, alisema ili kukabiliana na changamoto iliyopo ya utekelezaji duni wa bajeti ya maendeleo, serikali inapaswa kuruhusu taasisi za nje kuja kufanya tathmini ya kifedha (credit rating).

Mdee ambaye pia ni Mbunge wa Kawe (Chadema), alisema anaamini kwa kuruhusu taasisi huru kufanya tathmini ya kifedha nchini, kutaisaidia Tanzania kupata mikopo yenye riba nafuu badala ya mikopo ya masharti magumu ya kibiashara inayopewa kwa sasa.

"Kwa hali ilivyo sasa, ninaona kuna haja kuruhusu taasisi huru zije kutufanyia 'credit rating', ili itusaidie kama taifa kujua deni letu halisi likoje," Mdee alisema na kufafanua zaidi:

"Kwa kutofanyiwa credit rating, benki nyingi za kimataifa zenye mikopo ya riba nafuu zitaendelea kuogopa kutukopesha kwa sababu hazina uhakika kama tutalipa au la. Matokeo yake tutaendeela kukopa kwa masharti magumu ya kibiashara."

Mdee pia alisema ipo haja kufanya marekebisho kwa Sheria ya Deni la Taifa ambayo ina miaka zaidi ya 40 tangu kutungwa kwake.

Waziri kivuli huyo pia alisema kuwa kutokana na kupaa kwa Deni la Taifa, serikali sasa inapaswa kuwa makini zaidi katika ukopaji mpya, akieleza kuwa inapaswa kukopa kutekeleza miradi ambayo ina uhakika itarejesha fedha.

"Sheria yenyewe ya Deni la Taifa imepitwa na wakati. Ni sheria ya miaka ya 1970. Hoja yetu hapa ni kwamba tuwe na sheria inayoitaka serikali kukopa pale tu inapotaka kutekeleza miradi yenye uhakika wa kurejesha fedha na kulipa deni," alisema.

 

Habari Kubwa