Madereva 10 wa mabasi wafungiwa

02Apr 2021
Paul Mabeja
DODOMA
Nipashe
Madereva 10 wa mabasi wafungiwa

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amewafungia kwa muda wa miezi mitatu madereva 10 wa mabasi ambao wamekuwa wakikiuka sheria ya usalama barabarani kwa kuendesha kwa mwendo wa kasi vyombo vya usafiri.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene.

Aidha, ameliagiza Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani kuwachukulia hatua madereva hao ikiwamo kuwapeleka mahakamani kwa makosa hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dodoma, Simbachawene aliwataja madereva hao ni Allan Msangi ambaye huendesha gari lenye namba za usajili T605 DJR kutoka Kampuni ya Kapricon ambalo hufanya safari zake katika mikoa ya Dar es Salaam na Kilimanjaro  na hutembea kwa kilomita 125 kwa saa.

Waziri huyo alimtaja dereva mwingine ni Hussein Dudu kutoka kampuni ya Kimotco Intertrade, ambaye huendesha gari lenye namba za usajili T520 CXE, ambalo hufanya safari Arusha-Musoma na hutumia mwendokasi wa kilomita 126 kwa saa.

Mwingine ni Selemani Selemani, ambaye huendesha gari lenye namba za usajili T 313 DSO kutoka kampuni ya Al Saedy ambalo hufanya safari zake katika njia ya Dar es Salaam-Kilombero na hutumia mwendokasi wa kilomita 103 kwa saa.

Alimtaja dereva mwingine ni Athumani Mzava ambaye huendesha gari lenye namba za usajili T 391 kutoka kampuni ya MB Coach ambalo hufanya safari zake katika njia ya Dar es Salaam-Arusha na hutumia mwendokasi wa kilomita 107 kwa saa.

Waziri Simbachawene alimtaja dereva mwingine ni Juma Simba, ambaye huendesha gari lenye namba za usajili T 340 DPW kutoka Kampuni ya Baraka Classic ambalo hufanya safari zake katika maeneo ya Dar es Salaam- Masasi na hutumia mwendokasi wa kilomita 107 kwa saa.

Dereva mwingine aliyesimamishwa ni Salum Salum ambaye huendesha gari lenye namba za usajili T 121 DEA kutoka Kampuni ya Maning Nice ambalo hufanya safari zake Dar es Salaam - Tunduma na hutumia mwendokasi wa kilomita 110 kwa saa.

Mwingine ni Frank Masawe, ambaye huendesha gari lenye namba za usajili T 694 DRB kutoka kampuni ya Machinga ambalo hufanya safari zake katika Mikoa ya Dar es Salaam - Mtwara na hutumia mwendokasi wa kilomita 95 kwa saa.

Pia alimtaja dereva mwingine kuwa ni Innocent Thomas ambaye huendesha gari lenye namba za usajili T 225DTB kutoka kampuni ya Ester Luxury ambalo hufanya safari zake katika mikoa ya Dar es Salaam-Moshi na hutumia mwendokasi wa kilomita 107 kwa saa.

Kadhalika, Waziri Simbachawene alisema dereva mwingine ni Nassib Nasoro ambaye huendesha gari lenye namba za usajili T 565 BED kutoka kampuni ya NBS Classic ambalo hufanya safari zake katika mikoa ya Tabora na Kigoma na hutumia mwendokasi wa kilomita 109 kwa saa.

Vile vile, alimtaja dereva mwingine ni Maiko Mkindi ambaye huendesha gari lenye namba za usajili T 675 DHY kutoka kampuni ya Kilimanjaro Express ambalo hufanya safari zake katika Mikoa ya Dar es Salaam na Arusha na hutumia mwendokasi wa km 100 kwa saa.

“Kwa mamlaka niliyonayo nawafungia madereva hawa kwa muda wa miezi mitatu nawaagiza wamiliki wa mabasi haya ambayo madereva wamekiuka sheria ya usalama barabarani kuhakikisha wanachukua hatua stahiki kwa madereva wao,” alisema Simbachawene.

Aliliagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha kuwa linawapeleka mahakamani madereva hao ili iwe fundisho kwa wengine.

Habari Kubwa