Madereva 1,000 mbaroni madai kukwepa kulipa faini

26Jan 2021
Christina Haule
Morogoro
Nipashe
Madereva 1,000 mbaroni madai kukwepa kulipa faini

ZAIDI ya madereva 1,000 wa magari ya aina mbalimbali wamekamatwa mkoani Morogoro, kwa madai ya kudaiwa madeni ya faini za makosa mbalimbali.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Fortunatus Musilimu, alisema madereva hao waliokamatwa kwenye operesheni iliyoanza kufanywa na polisi tangu Januari 18 hadi jana, ambapo jumla ya madereva 1,384 wameshakamatwa.
 
Kamanda Musilimu alisema operesheni hiyo ni endelevu ambayo inafanyika nchi nzima kwa magari ya aina zote kutoka mikoa mbalimbali.
 
Alisema hapo mwanzo madereva walikuwa wanapaswa kulipa madeni papo hapo wanapokamatwa na makosa, lakini kutokana na kuwapo malalamiko kuwa hawatendewi haki wakaruhusiwa kulipa baadaye.

“Malalamiko yao wengine wanakamatwa wakati hawana fedha kwa wakati huo, na wengine wanapokamatwa wanaenda kulipa vituo vya polisi vilivyo mbali huku wakiwa wanapaswa kuendelea na safari,” alisema.
 
Alisema serikali ya sasa ni sikivu ikasikia kilio chao na kuamua kuweka mfumo na utaratibu wa kuwapa siku saba za kuwawezesha kulipa madeni pale wanapokutwa na faini jambo ambalo limeonekana kupuuzwa.
 
Alisema madereva hao hawalipi faini hizo, hivyo Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kuendelea kuwatafuta.
 
Alisisitiza kuwa madereva wote wanaodaiwa faini za makosa ya usalama barabarani walipe na kwamba hawatapita kama hawatalipa.
 
Pia Musilimu alisema jumla ya pikipiki 396 zimekamatwa kutokana na makosa mbalimbali ya usalama barabarani ikiwamo kutovaa kofia ngumu, kubeba abiria zaidi ya mmoja (mshikaki).
 
Kamanda huyo alisema kati ya pikipiki hizo zilizokamatwa, 354 zimeandikiwa faini, 22 zilipewa onyo (PF.6) na 20 bado zipo kituoni baada ya madereva wa pikipiki hizo kukimbia wakati wa ukamataji.

 
 

Habari Kubwa