Madereva masafa marefu walivyowekewa mkakati kukabiliana na corona

24Feb 2021
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Madereva masafa marefu walivyowekewa mkakati kukabiliana na corona

TANGU kuibuka kwa virusi vinavyosababisha ugonjwa wa corona (COVID- 19), dunia imekuwa katika harakati za kupambana na tatizo hilo huku kila nchi, taasisi na watu vinafsi wakichukua hatua mbalimbali juu ya kijikinga.

Magari yakiwa katika msururu mpakani kusubiri madereva kupimwa Corona. PICHA ZOTE ZA MAKTABA.

Nchini Tanzania, kwa mfano, miongoni mwa hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa ni pamoja na kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka, kutumia vitakasa mikono (sanitizers), kuvaa barakoa na hata kutumia njia za asili kama vile kujifukiza, maarufu kama nyungu, na kula vyakula vya kinga kama vile malimau, tangawizi na vitunguu swaumu.

Kwa ngazi ya kijamii, watu wamekuwa wakishauriwa kukaa kwa nafasi kutoka mtu mmoja hadi mwingine hasa kwenye mikusanyiko kama vile ibada, mikutano na sehemu zenye makutano ya watu wengi.

Taasisi mbalimbali pia zimekuwa zikitoa miongozi kwa wafanyakazi wao juu ya kijikinga na ugonjwa huo.

Moja ya taasisi hizo ni kampuni ya usafirishaji mafuta ya Primefuels Tanzania Limited ambayo imewaanzishia madereva wa masafa marefu utaratibu wa kusafiri na vifaa vya kujikinga na COVID-19 ili kuhakikisha wanakuwa salama wakati wote wawapo safarini.

Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu na Utawala wa Primefuels, Calvin Bhillon, alisema hayo hivi karibuni alipohojiwa na gazeti hili lilipotaka kujua kampuni inavyowalinda madereva wake na janga la corona hasa wanaovuka ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Bhillon alisema baada ya mlipuko wa pili wa corona kutangazwa duniani, baada ya ule wa kwanza kutokea mwaka jana, wiki mbili zilizopita walirejea katika utaratibu wa mwaka jana wa kuwapatia madereva vifaa vya kujikinga na ugonjwa huo, ili wavitumie pindi wawapo safarini.

“Kwa kuwa madereva wetu wanakwenda nchi mbalimbali, wiki mbili zilizopita tumeanza upya kuwapatia vifaa kama barakoa, vitakasa mikono ili wavitumie kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona,” alisema.

Bhillon alisema kampuni yao ina madereva 367 ambao wamekuwa wakifanya safari katika nchi mbalimbali za Afrika zikiwamo Burundi, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), Uganda, Malawi, Kenya, Rwanda na Zambia.

Utaratibu kama huo, alisema waliufanya mwaka jana wakati janga hilo la corona liliporipotiwa kwa mara ya kwanza mwezi Aprili.

Kwa mujibu wa Bhillon, tangu kutangazwa kwa janga hilo la corona, kumekuwa na utaratibu wa madereva kupimwa afya kwenye mpaka wa nchi husika anapoingia na kueleza kuwa ziko baadhi ya nchi ambazo hazipimi.

“Kipindi cha nyuma ilikuwa unapimwa mfano Dar es Salaam unakwenda na majibu ya vipimo, lakini baadaye walikuwa wanahitaji kufanya vipimo tena lakini kwa sasa wanapimwa wakiwa wanaingia kwenye nchi husika,” alisema.

Kuhusu gharama za vipimo vya corona, anasema kila nchi ambazo hutoa huduma hizo ina zake lakini wakilinganisha na kwingine Tanzania zipo juu.

Anaeleza kuwa kwa sababu utaratibu wa kuondoka na vyeti vya majibu ya corona kutoka Tanzania hauko tena, usumbufu ulioko ni ule wa dereva kusubiri majibu kwa siku mbili mipakani.

“Tangu mwaka huu uanze hatujapata kesi za madereva wetu kupimwa na kukutwa na corona, lakini kama kampuni tumeona ni vizuri wafanyakazi wachukue tahadhari,” alisema.

Bhillon alibainisha kuwa utaratibu wa kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa sabuni maji tiririka kila wakati pamoja na matumizi ya vitakasa mikono na kuzingatia umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu, uliwasaidia  madereva mwaka jana na ulipunguza  maambukizi miongoni mwao.

Alisema kampuni yao ilikuwa ikihakikisha kila dereva alipokuwa safarini lazima awe na vifaa kinga ndiyo maana baada ya mlipuko wa pili kutangazwa, wameamua kurejea upya utaratibu huo.

Bhillon alisema wito wao kwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki ambazo wanakwenda ni kwamba waondokane na dhana kuwa Tanzania kuna corona, watu hawapimwi na majibu yanayotolewa ni ya uongo.

“Serikali ya Tanzania kupitia balozi zake wafikishe ajenda hii kwenye nchi za majirani zetu, ili kuhakikisha unyanyapaa kwa Watanzania wanaokwenda kwenye nchi hizo haupo tena mwaka huu kama ilivyojitokeza mwaka jana.

“Kulikuwa na unyanyapaa hasa kwa madereva wetu na usumbufu wa askari wakati mwingine wamekuwa wakiwakataza hata kushuka kwenye magari kupata huduma yalijitokeza kipindi cha nyuma,” alibainisha.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania, Chuki Shabani, naye alishauri majibu ya corona kutoka nchi moja yaheshimiwe na nchi nyingine ili kuondoa usumbufu kwa madereva wanaosafirisha bidhaa mbalimbali.

“Wito wetu kama vile ifanyikavyo mpaka wa Tanzania na Kenya, wakipimwa waondoke na majibu na yaheshimike na kama kuna kupimwa nchi nyingine kusiwe na gharama yoyote,” alisema.

Kiongozi huyo alisema mwanzoni mwa mwezi huu, lilitokea tukio la madereva wao watatu kufungiwa kwenye kontena baada ya kufika mpaka wa Burundi kwa madai kuwa wana virusi vya corona na baadaye walipelekwa hospitalini.

“Tulipokea malalamiko haya kwa madereva wetu wakitueleza kuwa walipofika mpakani walipimwa na wakaambiwa kwamba wana corona sasa walitupigia wakawa wanalalamika kuwa wameonewa kwa sababu wakati wote wa safari walikuwa na utingo wao wakiwa wanakula na kulala pamoja kwenye gari na kuhoji mbona wao ni wazima lakini madereva tu ndio waonekane na corona,” walilalamika.

Shabani anasema baada ya vipimo hivyo madereva hao wakiwa na wenzao wanane kutoka nchi nyingine walichukuliwa na kufungiwa kwenye kontena na baadaye walipelekwa hospitalini na mpaka hivi karibuni walikuwa wametoka.

UTARATIBU WA AWALI

Baada ya janga la corona kuripotiwa kwa mara ya kwanza mwaka jana, moja ya makundi ambayo yalitakiwa kuchukua tahadhari ni pamoja na madereva wa malori.

Mei mwaka jana, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (wakati huo), Ummy Mwalimu, alipokutana na madereva, aliwaambia wahakikishe wanakula vyakula ambavyo vitalinda kinga zao za mwili na wasiache kupiga nyungu.

Waziri Ummy alizungumza na kundi hilo mwezi huo wakati upimaji wa madereva wa kampuni za malori zinazosafirisha mizigo nje ya nchi ukifanyika katika Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii iliyoko Mabibo, Dar es Salam.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Maabara hiyo, Ambele Mwafulango, katika takwimu zake alizozitoa alisema kwa siku walikuwa wakiwapima madereva 200 walioko jijini Dar es Salaam na kwa wale walioko mikoani waliweka utaratibu maalum wa kuchukuliwa sampuli ambazo zilikuwa zinatumwa kwa ajili ya vipimo.

“Katika maabara hii ya Mabibo tuna mashine mpya tano ambazo ndani ya saa 24 zinapima vipimo 1,800, hii imetufanya kupima vipimo vingi zaidi ukilinganisha na ilivyokuwa katika maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii iliyoko ofisi za NIMR (Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu) jijini Dar es Salaam. Tulikuwa na mashine mbili ambazo zilikuwa zinapima vipimo 300 hadi 400 jambo ambalo lilikuwa linachelewesha utendaji wetu wa kazi,” alisema.

Serikali iliweka utaratibu maalum kwa ajili ya madereva wa malori wanaosafirisha mizigo nje ya nchi kwa kufanyiwa vipimo vya corona kabla ya kusafiri ili kuhakikisha hawana maambukizi na kuwaepusha na usumbufu wawapo safarini.

Habari Kubwa