Madini sasa kuanza usafishwa nchini

07Nov 2019
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe
Madini sasa kuanza usafishwa nchini

SERIKALI imesema itaanza kusafisha dhahabu nchini ili kuongeza thamani, hivyo kusaidia kuongeza pato la taifa na kuhifadhi fedha Benki Kuu (BoT) kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

Katika kutekeleza hilo, imesema itajenga kituo cha kuchakata dhahabu jijini Dodoma na Geita kwa ajili ya kusafisha dhahabu na kuongeza pato la taifa kutokana na madini hayo.

Akizungumza katika mkutano wa ufunguzi wa Wiki ya Asasi za Kirais (Azaki), Naibu Waziri wa Madini, Stanislaus Nyongo, alisema dhahabu inayopatikana hivi sasa ni asilimia 80. Hivyo wanahitaji isafishwe nchini na kufikia asilimia 99.9 ili BoT ipate fedha kutokana na dhahabu hiyo.

Mbali na fedha kupelekwa BOT, pia wakianza mchakato huo, watakuwa na uwezo wa kuanza kuuza kwa gramu tofauti kwa wadau na kuzidi kuongeza pato la taifa.

Alisema lengo la mipango mikakati hiyo ni kuongeza asilimia ya pato litokanalo na madini ambalo awali ilikuwa asilimia.3.5, lakini hivi sasa limefikia asilimia tano kutokana na usimamizi mzuri wa serikali ya awamu ya tano.

Hata hivyo, alisema hadi ifikapo 2025, ifike asilimia 10 la pato litokanalo na madini.

Naibu waziri huyo alisema awali pato la uchumi litokanalo na madini lilikuwa dogo, lakini toka wameweka usimamizi mzuri katika sekta hiyo na kupelekea kufikia asilimia hizo.

Kutokana na hilo alisema wameamua kuanza kusafisha dhahabu hapa nchini lengo likiwa kila pato linalopatikana pale wanapovuna dhahabu fedha inachukuliwa na serikali.

Hatua hiyo pia alisema imetokana na kuanzishwa kwa Tume ya Madini ambayo inaundwa na watu kutoka sekta tofauti ambayo inahusika kutoa leseni za wachimbaji wadogo.

Alisema lengo la kufanya hivyo ni pamoja na kutaka kuondoa ukiritimba uliokuwa ukileta kelele nyingi kwa wachimbaji wadogo.

"Tumeamua sasa kuunda tume hiyo lengo ni kuondoa malalamiko kwa wachimbaji jambo ambali hivi sasa tunakwenda vizuri," alisema Nyongo.

Habari Kubwa