Madiwani washauri fedha ujenzi wa mgahawa zipelekwe kwenye maendeleo

23Jan 2020
Shaban Njia
KAHAMA
Nipashe
Madiwani washauri fedha ujenzi wa mgahawa zipelekwe kwenye maendeleo

BAADHI ya Madiwani wa Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama Mkoani Shinyanga, wamemshauri Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Michael Matomora kubadilisha matumizi ya fedha za ujenzi wa mgahawa kiasi cha shilingi Milioni 20 kuzipelekea kwenye miradi ya Maendeleo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ushetu Juma Kimisha akizungumza katika kikao cha baraza la madiwa cha kujadili rasimu ya mpango na bajeti ya matumizi ya kawaida na mpango wa maendeleo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021 hadi 2022/2023.

Hayo yamebainishwa leo na madiwani kwenye kikao cha baraza la madiwani cha kujadili rasimu ya mpango na bajeti ya matumizi ya kawaida na mpango wa maendeleo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021 hadi 2022/2023.

Pili Sonje, Diwani wa Ushetu  amesema fedha iliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Mgahawa wa Halmashauri zinatakiwa zielekezwe kwenye miradi ya maendeleo hasa kwenye kata ambazo miradi ilianzishwa kwa nguvu za wananchi na haijakamilika.

Diwani wa kata ya Ushetu Pili Sonje akitoa ushauri kwa Mkurugenzi wa kubadilisha bajeti ya fedha za ujenzi wa Mgahawa wa Halmashauri ya Ushetu.

“Mwenyekiti, kuna Kata ya Ushetu, Chona na Mpunze hazijapata fedha kutoka kwenye mapato ya ndani kwenye bajeti hii, ila zimepata fedha kutoka Serikali kuu, mimi nashauri fedha zilizotengwa kwenye ujenzi wa Mgahawa tuzigawanye ziende kwenye Kata hizi” amesema Sonje na kuongeza kuwa;

”Kwenye Kata zetu Mwenyekiti, tuna miradi mingi iliyoibuliwa na wananchi hasa ile ya Afya na Elimu haijakamilika kwa sababu ya ukosefu wa fedha, tukizigawa fedha hizi na kuzipeleka kukamilika miradi ambayo haijakamilika tutakuwa tumewatendea haki wananchi,"amesema

Ameongeza kuwa kama hoja ni Migahawa iliyopo kuwa michafu na haifai kwa watumishi kuendelea kuitumia, ni vema maafisa afya wa Halmashauri kutoa elimu ya umuhimu wa usafi kwenye migahawa iliyopo ili watumishi waitumie na fedha iliyotengwa iende kwa wananchi.

Nae Diwani wa Bulungwa viti Maalumu, Ester Matone amesema kuwa, mapato ya ndani hayatoshi kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa mgahawa wa Halmadhauri nakuongeza miradi iliyoibuliwa na wananchi ipo mingi na haijakamilika kwasababu ya uhaba wa fedha.

Hata hivyo Ofisa Mipango wa Halmashauri hiyo, Andrew Hagamu amesema kuwa, lengo la kutenga fedha na kujenga mgahawa wa Halmashauri ni moja ya chanzo mojawapo cha mapato kwani mgahawa huo utakodishwa kwa mzabuni ambae atakuwa analipa mapato.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Ushetu Wendere Lwakatare amesema kuwa,nikweli tunataka kujenga Mgahawa kwa ajili ya watumisha na nikwasababu tulipokea walaka kutoka juu wa kutotoka nje ya kituo cha kazi na kwenda kutafuta chakula wakati wa kazi.

Aidha amesema kuwa,watumishi wamekuwa wakinywa chai na kupata chakula kwenye migahawa ambayo sio safi na salama na kusababisha baadhi ya watumishi kuugua taifodi mara kwa mara na kushindwa kutoa huduma kwa wananchi pindi wawapo wagonjwa.

“Waheshimiwa madiwani,Tulipokea walaka ambao unatutaka tuwe tunapata chai na  chakula ndani ya eneo letu la kazi,Msione kama tunatupa fedha kwenye ujenzi wa Mgahawa,ila jinsi mtakavyoshauri sisi kama Halmashauri tutatekeleza” amesema Lwakatere.

Habari Kubwa