Madiwani Chadema wakimbilia CCM

25Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Arusha
Nipashe
Madiwani Chadema wakimbilia CCM

IDADI ya madiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambayo inaongoza Halmashauri ya Jiji la Arusha, imeendelea kupukutika baada ya madiwani watatu kujiengua kwa mpigo na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi(CCM).

Sambamba na madiwani hao, pia Katibu wa Chadema Wilaya ya Arusha Mjini, Innocent Kisanyage, ametangaza kujiuzulu na kujiunga na CCM. Wote hao wamedai kuwa wanaunga mkono juhudi za Rais John Magufuli.

Madiwani hao wamejiengua ikiwa ni miezi mitatu tangu aliyekuwa Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro, kuondoka ndani ya chama na baadaye kufuatiwa na madiwani wengine tano mwishoni mwa Novemba, mwaka jana na kujiunga na CCM.

Waliotangaza kujiuzulu juzi na kata zao kwenye mabano ni Melance Kinabo (Themi), Zacharia Mollel (Oloirien) na James Lyatuu wa Unga Limited.

Hatua ya kujiengua kwa madiwani hao imeiporomosha Chadema ambayo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, iliibuka na ushindi hivyo kuwa na madiwani 34 pamoja na mbunge.

Kwa sasa Chadema imebakiwa na madiwani 16 akiwemo Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na yule wa Viti Maalumu Joyce Mukya, huku CCM ikiwa na madiwani 10 akiwamo Mbunge wa Viti Maalumu, Catherin Magige.

Wakizungumzia sababu za kujiengua Chadema na kuomba kujiunga na CCM, madiwani hao walisema wamechukua hatua hiyo, kwa lengo la kuunga mkono kazi zinazofanywa na Rais Magufuli.

"Mimi sioni ‘future’ (mustakabali) kwa kesho nikiwa ndani ya Chadema kwenye mpango mzima wa kuleta maendeleo katika Jiji la Arusha na taifa kwa ujumla. Kwa busara na maamuzi (uamuzi) yangu (wangu) nimeamua kuondoka," alisema Kinabo.

Alisema chini ya Rais Magufuli hivi sasa, upelekaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo unakwenda kwa uwiano sawa na wa kasi kubwa bila ubaguzi wowote.

Alisema mipango yote ndani ya Jiji la Arusha imekuwa ikisimamiwa vyema na Mkurugenzi wa Jiji, Dk. Maulid Madeni.

Naye Mollel alisema ameamua kung'atuka ndani ya Chadema ili kuongeza wigo wa fursa za maendeleo katika jiji la Arusha badala ya kuwa kikwazo cha utekelezaji kwa ufanisi.

Lyatuu kwa upande wake alisema amechukua uamuzi huo kwa lengo la kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazofanywa na Rais Magufuli katika kutekeleza ujenzi wa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwamo kununua ndege, ujenzi wa treni ya kisasa na mradi wa umeme wa Bonde la Mto Rufiji.

Habari Kubwa