Madiwani wa upinzani wasusia kikao

06Mar 2017
Yasmine Protace
KIBITI
Nipashe
Madiwani wa upinzani wasusia kikao

MADIWANI wa kambi ya upinzani Halmashauri ya Kibiti mkoani Pwani, wamesusia kikao cha Baraza la Madiwani na kuamua kutoka nje ya ukumbi.

Hata hivyo, kitendo hicho kimemsikitisha Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Khatib Chaurembo hasa kwa kuzingatia kuwa walichukua uamuzi huo baada ya kujisajili na kusaini posho.

Madiwani hao wa upinzani waliamua kususia kikao hicho baada ya Chaurembo kuamuru Diwani wa upinzani, Khalid Abdul, atolewe nje ya ukumbi kutokana na kuvunja kanuni za baraza hilo.

Badaa ya diwani huyo kutolewa nje, madiwani wenzake wa upinzani, waliamua kumuunga mkono kwa kutoka nje.

"Mimi nimemtoa nje Diwani Abdul kutokana na kuvunja sheria katika kikao, lakini nashangaa kuona madiwani wenzake wakitoka nje huku wakujua kususia vikao ni kosa, lakini pia wakiwa wamesaini posho," alisema.

Chaurembo aliongeza kuwa kitendo kilichofanywa na madiwani hao wa upinzani, si cha kiungwana.

Kutolewa nje kwa Diwani Abdul kulitokana na kutofautiana kauli na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo.

Awali, Diwani aliyetolewa nje alisema kuwa kuna baadhi ya madiwani hawalipwi posho wanapofika katika vikao na kwamba hali hiyo inawafanya waishi vibaya pale wanapokuwa katika vikao.

Hata hivyo, Mwenyekiti alisema kuna utaratibu wa kufuatilia posho zao na kuongeza kuwa wapo waliozikosa na walifuata taratibu na wakalipwa.

Habari Kubwa