Madudu ya kutisha mtihani darasa la saba

23Nov 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Madudu ya kutisha mtihani darasa la saba

BARAZA la Mitihani Tanzania (NECTA), limetangaza matokeo ya darasa la saba, huku likieleza kuwapo kwa udanganyifu mkubwa, ikiwamo mwalimu wa taaluma akikutwa chooni akigawa majibu kwa wanafunzi.

Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Charles Msonde, alisema jana wakati akitangaza matokeo hayo mbele ya waandishi wa habari kuwa udanganyifu huo umefanywa na walimu wakuu wa shule 38, hivyo kusababisha matokeo ya wanafunzi 1,059 kufutwa.

Dk. Msonde alisema ufaulu kwa mwaka huu umeongezeka na kufikia asilimia 82.68, ikilinganishwa na mwaka jana uliokuwa asilimia asilimia 81.50.

Alisema watahiniwa 833,672 kati ya 1,008,307 wamefaulu kwa kupata asilimia 100 au zaidi ya alama 250 sawa na asilimia 82.68, kwamba wasichana ni 523,760 na wavulana ni 484,547.

“Kati yao waliofaulu kwa asilimia hizo wasichana ni 430,755 sawa na asilimia 82.24 na wavulana ni 402,917 sawa na asilimia 83.15. Mwaka 2019, waliofaulu walikuwa asilimia 81.50, hivyo kuna ongezeko la ufaulu kwa asimilia 1.18,” alisema Dk. Msonde.

UDANGANYIFU

Aidha, Dk. Msonde alieleza baadhi ya shule zilivyofanya udanganyifu wakati wa kufanyika mtihani, ikiwamo Shule ya Msingi Dominion, iliyoko mkoani Arusha.

Dk. Msonde alisema siku ya kufanyika mtihani, Oktoba 8, mwaka huu, Ofisa wa NECTA alishuhudia wanafunzi wa shule hiyo kwa nyakati tofauti, wakitumia choo kimoja bila kujali jinsia.

"Ofisa wetu alipoingia katika choo hicho alimkuta mwanamume akiwa amevaa mavazi ya upishi akiwa amekaa huku mkononi akiwa na majibu ya mtihani wa maarifa ya jamii, ambayo alikuwa akiwapa wanafunzi waliokuwa wakiingia katika choo hicho, alikuwa mwalimu wa taaluma, Shamsidini Ahmed wa shule hiyo,” alisema Dk. Msonde na kuongeza:

“Wakati akikamatwa, alitaka kupoteza ushahidi kwa kutaka kutumbukiza karatasi za majibu chooni lakini hakufanikiwa. Alikamatwa na kufungiwa kwenye ofisi,” alisema Dk. Msonde.

Baada ya mtihani kumalizika, alisema walipofungua mlango ili kumkamata hakuwapo, lakini dari na bati katika chumba hicho walikuta vimefumuliwa. Hata hivyo, alisema mwalimu huyo alikamatwa baadaye.

Alisema udanganyifu mwingine ulihusisha wakuu wa shule, askari mgambo na wasimamizi ambao waliandaa vikundi vya watu wakiwamo wahitimu wa sekondari, ambao walikuwa wakiwafanyia mtihani wanafunzi.

Dk. Msonde alitaja shule na idadi ya waliokamatwa kwenye mabado kuwa ni Halmashauri ya Gairo (11), Mvomero (12) mkoani Morogoro, Bariadi mkoani Simiyu, waliokamatwa ni (13) kutoka shule tatu tofauti.

“Halmashauri ya Sikonge mkoani Tabora (11), Halmashauri ya Moshi mkoani Kilimanjaro (5), Jiji la Arusha (5),  Halmashauri ya Tandahimba mkoani Mtwara  (7), Halmashauri ya Kiteto mkoani Manyara (4), Halmashauri ya Buchosa mkoani Mwanza (3).

Dk. Msonde alisema wakati wa usahihishaji walizibaini shule 19 zilizopo mikoa ya Simiyu, Geita, Morogoro, Arusha na Tabora zilikuwa na mfanano wa majibu, kwa kuwezeshwa na walimu wakuu na wasimamizi wa mitihani wa shule zao.

Alisema matokeo yenye udanganyifu yamefutwa na wanafunzi hao hawatafanya mtihani tena.

Katika mtihani wa kidato cha nne unaotarajia kufanyika kuanzia kesho, wamebaini kuwa mpaka sasa kuna shule 71 ambazo ziko katika mchakato wa kufanya udanganyifu na wamezipa onyo.

Aidha, alieleza kuwa NECTA imezuia matokeo ya watahiniwa 110 kutokana na matatizo mbalimbali yaliyowakuta, kupewa nafasi ya kuufanya tena mwakani

Habari Kubwa