Maelfu vyuo vikuu wajitokeza kuhakikiwa vyeti vya kuzaliwa

03Sep 2017
Mary Geofrey
Nipashe Jumapili
Maelfu vyuo vikuu wajitokeza kuhakikiwa vyeti vya kuzaliwa

WANAFUNZI 20,520 ambao ni yatima wanaohitaji mikopo ya masomo ya elimu ya juu mwaka 2017/18, wamejitokeza kuhakiki vyeti vya kuzaliwa na vifo, katika Ofisi za Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita).

Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Rita, Emmy Hudson.

Agosti 9, mwaka huu, Rita kwa kushirikiana na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), walitangaza kuhakiki nyaraka za wanafunzi wanaohitaji mikopo ambao wazazi wao wamefariki.

Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Rita, Emmy Hudson, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, alieleza kuwa, kati ya wanafunzi hao, 8,120 walituma maombi kwa barua pepe na 12,400 walipeleka kwa mkono mpaka Agosti 31.

“Idadi hii inaweza kuongezeka kwa sababu kila sekunde barua pepe zinapokelewa, tutatoa idadi kamili baada ya kufunga kazi hii,” alisema.

Aidha, wametangaza kuongeza siku saba kwa ajili ya kazi hiyo ili wanafunzi ambao hawajafika kuhakiki wafanye hivyo kabla ya kufungwa rasmi Septemba 7 mwaka huu.

Hudson aliwataka waombaji wa mikopo hiyo ambao hawajawasilisha vyeti vyao kwa ajili ya kuhakikiwa kufanya hivyo ndani ya siku saba.

“Baada ya terehe saba mwezi huu kupita, ofisi itashughulikia maombi yaliyotumwa kwa njia ya barua pepe au kuwasilishwa moja kwa moja katika ofisi zetu zilizopo kwa wakuu wa Wilaya na Rita Makao Makuu na kutoa majibu kwa waombaji,” alisema.

Kadhalika, alisema wananchi waliotuma maombi yao ya barua pepe wanaendelea kujibiwa na wale waliowasilisha katika ofisi zao Makao Makuu, wanaweza kufika katika ofisi zao kuanzia Septemba 2, mwaka huu na huduma ya uhakiki inaendelea.

Mkurugenzi wa HESLB, Abdulrazaq Badru, alikaririwa na waandishi wa habari akieleza vigezo vya wanafunzia ambao hawana wazazi wanatakiwa kuvitumiza ili wapate mikopo kuwa ni kuwasilisha nakala ya cheti au vyeti vya kifo vilivyodhibitishwa na Rita na kwa waliofadhiliwa wanatakiwa kuwasilisha barua kutoka kwa taasisi au mtu aliyemfadhili.

 Alisema mwanafunzi anatakiwa kuambatanisha fomu ya maombi iliyosainiwa na kamishna viapo, wakili au hakimu na nakala za vyeti vya taalum zilizogongwa muhuri na kamishna wa viapo na wakili au hakimu.

 

Habari Kubwa