Maeneo 23 yaliyoguswa zaidi bajeti ya kwanza awamu ya 5

12Nov 2017
Sanula Athanas
Nipashe Jumapili
Maeneo 23 yaliyoguswa zaidi bajeti ya kwanza awamu ya 5
  • *Imo miradi ya majisafi Dar, reli ya kisasa, umeme, ndege ATCL

WAKATI Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli ikitimiza miaka miwili wiki iliyopita tangu ilipoingia madarakani Novemba 5, 2015, imebainika kuwa maeneo 23 ndiyo yaliyoguswa zaidi katika bajeti ya kwanza ya serikali hiyo, yaani ya mwaka wa fedha 2016/17.

Aliyekuwa mkuu wa mkoa ruvuma,dk binilith mahenge (wa pili kushuto) akivuka mto ruvuma kwa mtumbi. (picha ndogo) kazi ya utandazaji mabomba ya maji kutoka mtambo wa ruvu chini ikiendelea.

Magufuli aliingia madarakani kumrtihi mtangulizi wake, Jakaya Kikwete, baada ya kuibuka nja ushindi wa zaidi ya asilimia 58 katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015.

Wakati akiingia madarakani, Magufuli aliikuta bajeti ya mwisho ya serikali ya awamu ya nne (2015/16) ikiwa imetekelezwa kwa miezi minne na uongozi wa awamu ya nne, na akaendelea nayo hadi Juni 30, 2016.

Katika bajeti hiyo, bunge liliidhinisha Sh. trilioni 22.45, kati yake, Sh. trilioni 16.7 zilikuwa za matumizi ya kawaida, sawa na asilimia 74.3 na Sh. trilioni 5.76 (asilimia 25.7) ya bajeti ziliidhinishwa kugharimia shughuli za maendeleo.

Bajeti ya mwaka 2016/17 ilikuwa ya kwanza kupitishwa na bunge nchini katika awamu ya tano. Kwenye bajeti hiyo iliyofikia ukomo wake Juni 30, mwaka huu, serikali ilipanga kukusanya na kutumia Sh. trilioni 29.53.

Kati ya fedha hizo, Sh. trilioni 17.72 zilikuwa ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida, wakati Sh. trilioni 11.82, sawa na asilimia 40 ya bajeti nzima, ziliidhinishwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

Jumanne iliyopita, akiwasilisha bungeni mjini Dodoma Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2018/19 na pia Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya mwaka ujao wa fedha, Dk. Mpango alisema serikali ya awamu ya tano iliitekeleza bajeti yake ya kwanza ya mwaka 2016/17 kulingana na upatikanaji wa mapato.

MAKUSANYO
Dk. Mpango alisema mapato yaliyopatikana kutoka vyanzo vyote mwaka 2016/17 yalikuwa Sh. trilioni 23.635, ikilinganishwa na makadirio ya Sh. trilioni 29.539.

Alisema mapato ya ndani yalikuwa Sh. trilioni 16.639, sawa na asilimia 90.2 ya makadirio lakini yakiwa na ongezeko la asilimia 17.7 ikilinganishwa na makusanyo ya mwaka 2015/16.

Dk. Mpango alisema misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo ilifikia Sh. trilioni 2.474, sawa na asilimia 68.7 ya ahadi.

Alisema mikopo ya ndani ilikuwa Sh. trilioni 4.505, sawa na asilimia 83.8 ya lengo la kukopa trilioni 5.374 na mikopo ya nje ya kibiashara ilikuwa Sh. trilioni 1.227, ikiwa ni asilimia 58.4 ya malengo.

Waziri huyo alibainisha kuwa kiasi cha Sh. trilioni 1.221 kati ya mikopo yenye masharti ya kibiashara hakikutumika kwa mwaka 2016/17 kwa kuwa kilipokewa mwishoni mwa mwaka.

"Kiasi hiki cha fedha kitatumika kugharimia miradi ya maendeleo iliyokusudiwa katika mwaka 2017/18," alisema Dk. Mpango.

MATUMIZI
Waziri huyo alisema jumla ya Sh. trilioni 23.635 zilitolewa, ikiwa ni asilimia 80 ya makadirio ya mwaka 2016/17 na asilimia 6.5 zaidi ya matumizi hali ya serikali mwaka 2015/16 ya Sh. trilioni 22.099.

Alisema kati ya Sh. trilioni 23.635 zilizotumika, Sh. trilioni 17.136 zilielekezwa kwenye matumizi ya kawaida, sawa na asilimia 96.7 ya lengo na Sh. trilioni 6.498 zilitumika kugharimia miradi ya maendeleo, sawa na asilimia 55 ya lengo la mwaka.

"Kwa niaba ya serikali napenda kuwapongeza Watanzania walioitikia wito wa serikali wa kulipa kodi kwa hiari hususan ongezeko la mwitikio wa kutumia mashine za kieletroniki (EFD)," alisema Dk. Mpango na kuongeza:

"Mwaka 2016/17 tulishuhudia pia mwitikio na hamasa ya kipekee kwa wananchi kulipa kodi ya majengo. Haya kwa ujumla wake yanaonyesha uelewa wa Watanzania kuhusu wajibu wa kulipa kodi ili kuchangia maendeleo yao.

"Nawaomba Watanzania waendelee na moyo huo wa kizalendo na kuwahimiza wale ambao hawajapata mwamko kuanza kulipa kodi kwa hiari. Ni kwa njia hii pekee ndipo tutaweza kujenga msingi endelevu wa uchumi na ustawi wa jamii na kulinda heshima ya uhuru wetu."

MAENEO 23
Akizungumzia miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2016/17, Dk. Mpango alibainisha maeneo 23 ambayo imetekelezwa na serikali katika kipindi hicho.

Alisema maeneo hayo ni pamoja na kugharimia ujenzi wa awamu ya kwanza wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro kwa Sh. trilioni moja na ujenzi na ukarabati wa barabara kwa kutumia fedha za mfuko wa barabara kiasi cha Sh. bilioni 807.4.

Alisema maeneo mengine ni mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu Sh. bilioni 495.4, elimu msingi bila malipo Sh. bilioni 2,096.9, upanuzi wa miundombinu ya umeme vijijini Sh. bilioni 361.5, uboreshaji wa usafari wa anga kwa ununuzi wa ndege mpya mbili Sh. bilioni 103.4 na malipo ya awali ya ndege mpya nne Sh. bilioni 320.1.

Dk. Mpango alitaja maeneo mengine yaliyotekelezwa katika bajeti hiyo kuwa ni uwekezaji wa miundombinu ya umeme Sh. bilioni 176.5, ununuzi wa dawa na vifaa tiba Sh. bilioni 165, uwekezaji kwenye miundombinu ya usambazaji maji mijini na vijijini Sh. bilioni 137.4 na upatikanaji wa pembejeo za kilimo Sh. bilioni 21.

Alisema miradi mingine ni upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam Dola za Marekani milioni 345, ununuzi wa asilimia 35 ya hisa katika Shirika la Simu Tanzania (TTCL) hivyo kuiwezesha serikali kumiliki TTCL kwa asilimia 100 (Sh. bilioni 14.9) na pia kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na rasilimali za taifa.

"Mafanikio mengine yaliyopatikana ni pamoja na kupata mradi mkubwa wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Chongoleani (Tanga) dola bilioni 3.5 …kupitia mradi huu taifa litanufaika na ajira, utaalamu na fursa za kibiashara," alisema.

MIRADI 8 SEKTA BINAFSI
Dk. Mpango alisema katika mwaka huo wa fedha, sekta binafsi ilitekeleza miradi minane ambayo ni pamoja na miradi mipya 1,160 ya maji katika vijiji 1,206 vya halmashauri 148, uchimbaji visima 11 mkoani Tabora, upanuzi wa huduma ya maji safi katika manispaa ya Dodoma na Singida.

Alisema mradi wa pili ni uanzishaji wa viwanda ikiwa ni pamoja na viwanda vya kuzalisha vifungashio vya Global Packing (T) Ltd na Madoweka Co. Ltd, viwanda vya kuzalisha bidhaa za ujenzi vya Goodwil Ceramics Ltd na Waja General Co. Ltd (vyote Pwani) na kiwanda cha kusindika nyama cha Paul Kisivani (Arusha).

Dk. Mpango alisema mradi mwingine ni kukamilika kwa ukarabati na upanuzi wa vyumba saba vya upasuaji na kuongeza idadi ya vyumba kufikia 20 kwenye jengo kuu la upasuaji katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Pia kukamilika kwa ukarabati katika jengo la watoto pamoja na kuweka mfumo wa hewa 'medical gas piping, kununuliwa mashine moja ya kisasa ya CT-Scan, mashine 14 za upasuaji, mashine mbili kubwa za usafishaji wa vifaa, vifaa vya usikivu na lifti mbili kwa ajili ya majengo ya Kibasila na Sewahaji.

Waziri huyo aliutaja mradi wa nne kuwa ni kukamilika kwa ukarabati mkubwa na ujenzi wa vituo vya afya vinane vilivyopo Kanda ya Ziwa na kuifanya idadi ya vituo vinavyotoa huduma ya upasuaji wa matatizo yatokanayo na uzazi pingamizi pamoja na upatikanaji wa damu salama kufikia 171 uliokwenda sambamba na ununuzi wa magari 67 ya kubebea wagonjwa.

Alisema mradi mwingine ni utunzaji na uhifadhi wa vyanzo vya maji ambapo mipaka ya vyanzo vya maji 10 imewekwa katika mabonde ya Rufiji, Ruvuma na Pwani ya Kusini, Ziwa Rukwa na Wami/Ruvu.

Dk. Mpango aliutaja mradi wa sita kuwa ni ujenzi wa Bwawa la Kidunda ambalo hatua iliyofikiwa ni kukamilika kwa usanifu wa bwawa na barabara ya Ngerengere - Kidunda (km 76) pamoja na sehemu ya malipo ya fidia kwa wananchi 2,603 waliohamishwa kupisha ujenzi wa bwawa na barabara.

Alisema mradi mwingine ni uchimbaji wa visima virefu Kimbiji na Mpera ambapo visima 15 kati ya 20 vilivyokuwa vimepangwa vimekamilika.

Dk. Mpango alisema mradi wa nane ni mtandao wa mabomba ya majisafi jijini Dar es Salaam ambapo shughuli za ujenzi wa matanki saba, kulaza mabomba makubwa yenye urefu wa kilomita 69 na madogo ya usambazaji maji kwa urefu wa kilomita 361 umekamilika na hivyo kuanza kuunganishiwa maji kwa wateja katika maeneo ya Mbezi, Kiluvya, Tegeta na Bagamoyo.

Habari Kubwa