Maeneo hatarishi kuishi Dar haya

08Nov 2016
Chauya Adamu
Dar es Salaam
Nipashe
Maeneo hatarishi kuishi Dar haya

TUME ya Sayansi na Teknolojia (Costech) imebaini maeneo hatarishi kwa kuishi katika kata 29 jijini Dar es Salaam, na kupendekeza serikali iwahamishe wakazi wa maeneo hayo kuepuka baa linaloweza kujitokeza.

Ikishirikiana na wataalamu wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) kupitia mradi wa ‘Ramani Huria’, tume hiyo imeainisha maeneo hayo ambayo mara nyingi yamekuwa yakisababisha adha kubwa kwa wakazi wake hasa nyakati za mvua.

Kutokana na utafiti wake, Costech imebaini maeneo hayo ambayo mengi ni ya mabondeni, yameorodheshwa na kuonekana kuwa hatarishi kutokana na kugharimu maisha ya wakazi na kuwa chanzo cha magonjwa ya milipuko kikiwamo kipindupindu.

Akizungumza na Nipashe jijini jana mara tu baada ya uzinduzi wa mradi huo, Msimamizi Mkuu wa mradi huo, Innocent Maholi, alisema kutokana na utafiti uliofanyika katika kata 29 jijini Dar es Salaam, wamegundua katika wilaya za Temeke, Kinondoni na Ilala kuna maeneo mengi ambayo ni hatarishi kwa kuishi, hivyo ipo haja serikali kuwahamisha wakazi wa maeneo hayo.

“Mradi huu ulifanyika katika kata 29 hapa jijini Dar es Salaam, tumebaini maeneo mengi ya mabondeni ni hatarishi kwa kuishi na tunaiomba serikali kutumia ramani hii kuwajulisha wananchi kuwa maeneo haya ni hatarishi. Siyo kipindi cha mvua tu, bali hata nyakati za kawaida zinaweza kuithiri jamii,” alisema Maholi.

Alisema tume iliishirikisha jamii kwa kiasi kikubwa kujua historia ya maeneo hayo na kwamba kutokana na ramani ya mwanzo ya mwaka 1994 ambayo ndiyo inayotumika hadi leo, kuna haja serikali kutumia ramani mpya iliyogundua maeneo hatarishi ili kuepuka balaa na usumbufu kwa wananchi.

Alisema ramani hiyo inaonyesha maeneo ya mabondeni likiwamo Bonde la Msimbazi na maeneo ya Tandale ambayo imejengewa mitaro inayojaa na kusababisha maji mengi kuingia katika nyumba za wakazi hao na kusababisha kero.

Alisema ramani hiyo inaonyesha namna ya kulijenga upya jiji la Dar es Salaam kwa kuwa inaonyesha jinsi ya kusafisha maeneo hayo hasa mitaro na maeneo ambayo yanaweza kujengwa miundombinu mingine ikiwamo ya maji, barabara na umeme.

Mtaalamu wa Mipango Miji aliyeshiriki katika mradi huo, Deogratius Minja, alisema lengo la mradi huo ni kuwafahamisha wananchi maeneo mazuri kwa kuishi na kwamba ili kuepukana na magonjwa, wamefanya utafiti kufahamu mifumo ya utoaji taka katika kata 36 jijini na kubaini kuna haja ya kuifanyia matengenezo.

Alisema kutokana na idadi ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam kukua kila siku, walilazimika kufanya utafiti huo ulioanzia Machi mwaka jana hadi Oktoba 9, mwaka huu na kwamba kila mkazi anatakiwa kuwaona viongozi wa serikali za mitaa ili afahamu maeneo hayo na kuondokana na adha ya mafuriko pamoja na magonjwa ya milipuko.

Alisema mradi huo ulitokana na Benki ya Dunia (WB) kuona jinsi wananchi wanavyoteseka nyakati za mvua kila mwaka na ilitoa wazo hilo ili kukabiliana na tatizo hilo na wamepanga kuufikisha mradi huo kwenye mikoa mingine nchini kukabiliana na changamoto ya mafuriko.

Mbali na kata ya Tandale, maeneo mengine hatarishi yaliyoorodheshwa katika ramani hiyo ni pamoja na ya kata za Mzimuni, Kigogo, Vingunguti, Ndugumbi, Mburahati, Mabibo, Magomeni pamoja na maeneo yote yaliyopitiwa na Mto Msimbazi.

Habari Kubwa