Mafuriko Dar yalivyoua tisa

17Apr 2018
Elizaberth Zaya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mafuriko Dar yalivyoua tisa

IDADI ya watu waliofariki dunia kutokana na athari za mvua katika Jiji la Dar es Salaam imefikia tisa, huku watu 10 wakijeruhiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema waliofariki ni wengi ni kwa kuangukiwa na kuta na kusombwa na maji.

Mambosasa aliwataja watu hao ni Grace (maarufu kama mama Elias, (30) na mwanae Adulrazak Ally(4), wakazi wa Segerea, waliofariki baada ya kuangukiwa na uzio wa ukuta wakiwa wamelala na kwamba katika tukio hilo watu wanne walijeruhiwa.

Wengine ni Mikidadi Hija (44), mkazi wa Goba, Mwanaidi Seif (24), mkazi wa Kigogo na Nasri Haji (9), mwanafunzi wa Shule ya Msingi Bokorani, mkazi wa Mbagala, Amina Said (28), mkazi  wa Kawe ambao wote hao walifariki kwa kuangukiwa na nyumba.

Mambosasa alimtaja mwingine aliyefariki ni Sadick Ally (36) ambaye aliteleza na kutumbukia katika daraja la mto Kizinga lililokuwa limejaa maji, huku wengine wawili ambao majina yao hayakufahamika mmoja mkazi wa Kawe na mwingine Kinyerezi, walifariki baada ya kusombwa na maji.

Pia alisema watu wengine sita walijeruhiwa kwa kuangukiwa na ukuta Buguruni na kujeruhiwa vibaya kisha walikimbizwa hospitali.

Akizungumzia zaidi hali ya mvua, Mambosasa alisema jana jeshi hilo lililazimika kutumia helikopta kuzunguka katika maeneo mbalimbali katika jiji hilo na walibaini maeneo mengi yakiwamo ya Kijichi, Mbagala, Buruguni, Jangwani, Kigamboni kujaa maji.

 “Nyumba nyingi ambazo ziko mabondeni maji yako nusu, lakini kitu cha kushangaza, tumepita tukaangalia nyumba nyingine maji yamefika dirishani, lakini watu hawajali, wanaendelea kufua nguo na kuanika, wanachukulia masihara,” alisema Mambosasa na kuongeza:

“Mimi naomba watu wote ambao wako mabondeni waondoke kwa sababu ni hatari na kuendelea kukaa humo ni kama kununua kifo.”

Hata hivyo, Nipashe lilipita katika maeneo mbalimbali ya jiji na kushuhudia barabara nyingi zikiwa zimejaa maji na kupitika kwa shida.

Pia katika eneo la Vingunguti Koloni, wananchi wa eneo hilo ambao nyumba zao ziko mbembezoni mwa mto Msimbazi walikuwa wameanza kubomoa nyumba zao na kusomba bati, tofali na mbao na kuhamishia shemenu nyingine.

Asha Shaban, mkazi wa eneo hilo aliliambia Nipashe kuwa wameamua kubomoa nyumba kwa hiari yao wenyewe baada ya kushuhudia baadhi ya nyumba zilizoko kandokando ya mto huo zikiwa zinasombwa na maji.

Alisema juzi baadhi ya nyumba karibu tano zilianza kumeguka na kuta zake kuanza kuangukia mtoni kutokana na kasi kubwa ya maji yaliyokuwa yakipita kwenye mto huo.

“Unajua hili eneo tulilojenga ni karibu na mto na baada ya kunyesha mvua kubwa nyumba zinatitia kwa chini  na kadri mvua zinavyoendelea kunyesha, mmomonyoko wa mto unazidi kusogea, na kama unavyoona usiku wa leo hatujalala na ndio maana tukaamua kubomoa ili tusikose kila kitu,” alisema Asha.

Kaimu Mwenyekiti wa Mtaa huo wa Kongole, Clemency Mwanja, alisema ni mara ya pili kutokea tatizo hilo  katika kipindi cha mvua japokuwa hakujawahi kushuhudiwa vifo.

Mjumbe wa serikali ya mtaa, Benedict Alfonce anayeshughulikia maafa, alisema jana pekee zaidi ya nyumba tano zilikuwa zimeanza kumegwa na mto.

Pia alisema wananchi hao mmoja mmoja walikuwa wameanza kuhamisha vitu vyao kupeleka kwa ndugu na jamaa zao.

Katika eneo la Tandale kwa Tumbo, nyumba nne zinadaiwa kuanguka na maji, huku wakazi wa nyumba hizo wakihifadhiwa na majirani.

Katibu wa mtaa huo, Jumane Juma, alisema kuwa tangu juzi walianza kuona dalili za kubomoka kwa nyumba hizo na kuwashauri wenye nyumba kuhama haraka.

“Bahati nzuri tulivyokuwa tunatembelea nyumba kuangalia usalama, tuliona nyumba hizo zimeanza kuonyesha dalili za kuanguka tukawashauri waondoke  na bahati nzuri walitusikiliza,” alisema Juma.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) katika Tovuti yake jana, vipindi vifupi vya mvua kubwa inayozidi milimita 50 katika saa 24 vinatarajiwa kuendelea leo na kesho.

Baadhi maeneo ambayo yalitajwa kuwa na mvua hizo ni Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Mafia, Morogoro, Lindi, Mtwara na Visiwa vya Pemba na Unguja.

Habari Kubwa