Mafuwe amwaga machozi, uwezo wa mwanafunzi mwenye ulemavu

09Dec 2021
Godfrey Mushi
KILIMANJARO
Nipashe
Mafuwe amwaga machozi, uwezo wa mwanafunzi mwenye ulemavu

MBUNGE wa Hai mkoani Kilimanjaro (CCM), Saashisha Mafuwe, ameshindwa kuzuia hisia zake na kujikuta akibubujikwa machozi, baada ya kumuona Minael Yohana, ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tano wa Shule Jumuishi ya Walemavu ya St. Francis Assis, akiwa hana baadhi ya viungo ikiwamo miguu na mikono-

- lakini ana uwezo wa kuandika kama mtu mwenye mikono.

Baada ya kubaini kipaji chake katika elimu, Saashisha, bila ya kumung’unya maneno, aliagiza wasaidizi wake haraka kumletea kitimwendo cha kisasa, Minael ili kumsaidia kwenda darasani na kurudi katika bweni analolala shule anayosoma.

Saashisha, amemkabidhi mwanafunzi huyo kitimwendo hicho leo wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika. Mkuu wa Wilaya ya Hai, Juma Irando, ndiye aliyekabidhi kiti hicho kwa niaba ya Mbunge huyo.

“Bado nitaendelea kutambua mchango wa jamii ya watu wenye ulemavu katika kuchangia maendeleo ya Jimbo letu na maendeleo yao kwa ujumla. Najua kuna uhitaji mkubwa wa huduma za utengamao kwa watu wenye ulemavu.

“Katika mwendo wa utekelezaji wa ahadi zangu, mpaka sasa nimegawa vitimwendo 15 kwa watu wenye ulemavu waliopo Kata za Machame Mashariki, Machame Kaskazini, KIA, Bomang’ombe na Muungano.

Shule ya St.Francis Assis iliyopo katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Hai, inamilikiwa na Shirika la Watawa la Bibiti yetu lililopo chini ya Kanisa Katoliki, Jimbo la Moshi.

Katika taarifa yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Saashisha, amesema miongoni mwa mambo muhimu, ambayo wazazi na walezi walio na watoto wenye ulemavu, wanahimizwa kwa sasa ni kutowaficha ndani, badala yake watoe taarifa kwa viongozi serikali ili wapate elimu.

“Tunawanahimiza hivyo kutokana na ukweli kwamba, watoto wenye ulemavu nao wana haki ya kupata elimu kama walivyo wengine wenye viungo kamili, hivyo kuwaficha ni kuwakosesha haki hiyo ya msingi.

“Hata hivyo, ushiriki wa jamii ni muhimu katika kuhakikisha huduma za utengemao zinaimarika, kwa vile masuala ya watu wenye ulemavu ni mtambuka. Hivyo jitihada za pamoja zinahitajika ili kufikia malengo yaliyoainishwa katika miongozo ya kitaifa na kimataifa kwenye suala la elimu.”

Akizungumza baada ya kukabidhiwa msaada huo, Mkurugenzi wa Shule ya St. Francis Assis, Mtawa Consolatha Mosha, amemshukuru Mbunge huyo kwa kumwezesha Minael kufikia ndoto zake za kielimu kwa kumuongezea miguu, huku akimtaka kila wakati anapozungumza na wananchi kugusia mahitaji ya wenye ulemavu.

Habari Kubwa