Magaidi wote waliofanya shambulizi DusitD2 wameuawa

16Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Magaidi wote waliofanya shambulizi DusitD2 wameuawa

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amesema magaidi wote waliofanya shambulio katika hoteli ya kifahari ya DusitD2 na kusababisha vifo vya watu 14, wameuawa.

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta.

Kenyatta ametoa kauli hiyo leo Jumatano Januari 16, 2019 wakati akihutubia Taifa kuhusu operesheni ya kupambana na magaidi waliovamia hoteli hiyo, tukio hilo lililotokea jana Januari 15, 2019.

Rais amesema kuwa, “Sisi kama taifa tunaomboleza na tunawaombea majeruhi wapone haraka lakini pia tunaendelea kudumisha usalama nchini,”.

Aidha Rais Kenyatta amesema nchi yao ni ya amani na ina sheria na kwamba hawataweza kusahau wale waliohusika na shambulizi hilo na kwamba tayari ameshafanya mkutano na asasi za kiusalama juu ya namna ya kuwashughulikia magaidi hao.

Pia amesisitiza kuwa nchi iko salama kwa sasa na kuwataka wageni na wenyeji waendelee kusukuma gurudumu la maisha huku akiwaasa wakenya kusambaza ujumbe wa kutiana moyo katika mitandao ya kijamii.

Amebainisha kuwa watu 700 wameokolewa na vyombo vya ulinzi na usalama, kwamba operesheni hiyo imekamilika na magaidi wote wameuawa.

Rais Kenyatta amesema watu  30  waliojeruhiwa walipelekwa katika hospitali mbalimbali za mjini Nairobi.

Habari Kubwa