Magendo ya mil. 246/- yanaswa mpakani

16Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Tarime
Nipashe
Magendo ya mil. 246/- yanaswa mpakani

KITUO cha Forodha cha Sirari mkoani Mara, kimekamata mapipa 386 yenye lita za ujazo 96,500 yenye malighafi ya kutengeneza pombe kali ya thamani ya Sh. milioni 246.6.

Malighafi hizo zilizokuwa zikisafirishwa bila kibali kwenda nje ya nchi zikitokea Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Meneja  wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kituo hicho, Martin Kawonga, alisema shehena ya kwanza ya aina hiyo, ilikamatwa mwishoni mwa  mwaka jana 2018, ikiwa na mapipa 336 yenye ujazo wa lita 84, 000 yenye thamani ya Sh. 201,600, 000 na usiku wa kuamkia juzi, maofisa operesheni hao walikamata tena mapipa 50 yenye lita 12,500 ya thamani ya Sh. milioni 30.

“Mtuhumiwa huyu Thomas Makara ni sugu katika biashara za magendo. Mwaka jana tulimkamata na magendo ya thamani ya Sh. milioni 201. 6 na kumtaifisha kisha tulimfikisha mahakamani. Leo (juzi) tena alfajiri saa 9:00 tumemkamata akiwa na mapipa 50 ya dawa za kutengenezea pombe kali yenye lita za ujazo 12,500 kila pipa likiwa na ujazo wa lita 250,” alisema.

Kawonga alifafanua kuwa mapipa hayo yalikamatwa yakiwa yamefunikwa juu yake na malighafi za mifuko ya chokaa 165, magodoro 18, pumba za mchele magunia manane na sabuni za unga mifuko 20 ambayo kila mmoja ni kilo 15 bila kibali cha TRA yakisafirishwa kwenda Kenya.

Alisema katika operesheni ya juzi walimkamata tena mfanyabiashara huyo ambaye ni raia wa Kenya  akisafirisha magendo hayo kwa kutumia lori lenye namba za usajili T 798 DCS aina ya Mitsubishi mali ya Nassoro Mrimi, mkazi wa Sirari.

Meneja huyo alisema dereva wa gari hilo ambaye hakufahamika jina lake, alitoroka kwenda kusikojulikana na anaendelea kusakwa na Jeshi la Polisi.

Kawonga alisema magendo yaliyokamatwa juzi yametaifishwa kwa mujibu wa sheria na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa polisi.

Habari Kubwa